loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Siku ya watu wenye ualbino duniani na uelewa wa jamii

JUNI 13, kila mwaka dunia huadhimisha Siku ya Kimataifa ya uelewa kuhusu watu wenye ualbino. Nchini maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika mkoani Morogoro.

Hata hivyo, siku hii inaadhimishwa huku matukio ya ukatili dhidi ya watu wenye ualbino yakiwa bado yapo barani Afrika, japo kwa Tanzania yamepungua tofauti na ilivyokuwa mwanzo.

Siku hii inaadhimishwa, licha ya maazimio mbalimbali yaliyopitishwa na vyombo vya kutunga sheria vya ndani ya nchi na vile vya kimataifa, bado vitendo vya unyanyapaa kwa watu wenye ualbino vimeendelea kukithiri.

Kutokana na hali hii, Mei 29 na 30, mwaka huu Shirika la Under The Same Sun (UTSS) liliandaa semina ya siku mbili ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari iliyofanyika mjini Morogoro. Kongamano hilo lililenga kukumbusha matumizi ya majina sahihi ya makundi ya watu wenye ulemavu, hususan watu wenye ualbino.

Katika semina hiyo, wahariri walipatiwa mafunzo kuhusu “uelewa kuhusu ualbino” na harakati za uelewa kuhusu ualbino duniani. Mwisho wa semina hiyo maazimio 12 yakafikiwa.

Miongoni mwa maazimio hayo ni pamoja na kutumia neno “Watu Wenye Ualbino” badala ya neno Albino wakati wa uandishi wa habari zinazohusu kundi hilo, pamoja na kuazimia kuripoti masuala ya watu wenye ualbino kwa pamoja. Mwaka 2013 Umoja wa Mataifa (UN) kupitia Baraza lake la Tume ya Haki za Binadamu, ulipitisha azimio kutaka watu wenye ualbino walindwe na kuepuka vitendo vya unyanyapaa dhidi yao.

Aidha, Machi 26, 2015, baraza hilo liliunda kamati maalumu na kuipa uwezo wa kuwa jopo huru kuchunguza na kupendekeza hatua za kuchukua dhidi ya vitendo vyovyote vinavyowahusu watu wenye ulemavu na wenye ualbino. Hii ilikuwa katika kujibu mwito uliokuwa unatolewa na mashirika ya kiraia kutambua kwa umuhimu wake, kundi la watu wenye ualbino na kutoa mahitaji maalumu.

Vyombo vyote viwili vya kimataifa; Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa, vimepitisha maazimio maalumu yanayowalinda watu wenye ualbino pamoja na kuzitaka nchi wanachama za umoja huo, kupitisha sheria kali kupitia mabunge yao, kuwashughulikia ipasavyo wanaojihusisha na ukatili na mauaji dhidi ya watu wenye ualbino. Katika jamii za Kiafrika, bado uelewa kuhusu watu wenye ualbino ni mdogo na kuna watu wanaoamini kwamba, miili ya watu wenye ualbino huwa na nguvu ya kuleta utajiri.

Jambo wasilolijua wengi au wanalijua lakini wanazembea kwa makusudi ni kwamba, watu wenye ualbino ni binadamu kama wengine ila wao wamepungukiwa melanini inayohusika na rangi ya ngozi, nywele na macho yao, au wanayo kwa kiwango kidogo sana.

Wengi pia hawajui kuwa, ualbino hutokea kwa wanyama na kwa mimea. Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya kitaalamu, melanini ni muhimu sana kwa mtu kwa kuwa ni kinga dhidi ya mnunurisho wa jua. Inaelezwa na wataalamu mbalimbali kuwa, hali ya ualbino hurithiwa kama wazazi wote wawili wana jeni inayoruhusu ualbino. Hii inawezekana hata kama wazazi wote wawili hawaoneshi dalili za ualbino wenyewe.

Hali hii inaendelea katika familia na inaweza kuonekana mara kwa mara au baada ya kizazi tu. Inategemea na kupatikana kwa jeni husika katika wazazi wote wawili. Hii ina maana kuwa, urithi wa hali ya ualbino unaweza kuendelea katika familia kwa vizazi kadhaa bila mtoto kuwa na ualbino.

Lakini pale ambako mume na mke wenye rangi ya kawaida walio na jeni hii wanapokutana watoto wanaweza kutokea wakiwa na hali ya ualbino. Jambo lingine katika jamii ni kuwa, hali ya ualbino mara nyingi huitwa ugonjwa ingawa hii inategema jinsi ya kufafanua “ugonjwa”. Mtu mwenye ualbino huzaliwa na hali ya pekee inayoweza kupunguza uwezo wake wa kuona vizuri ingawa hii si lazima.

Pia yuko katika hatari ya kupata saratani ya ngozi kutokana na athari ya nuru ya jua. Tukiacha matatizo ya macho na hatari ya saratani ya ngozi, mtu mwenye ualbino ni binadamu wa kawaida mwenye afya njema, ingawa anapaswa kujihadhari asikae kwenye jua muda mrefu bila kinga. Ualbino huo unaweza kuathiri watu wa kila rangi, lakini kwa sababu zisizoeleweka, utafiti unabainisha kuwa bado unapatikana zaidi Afrika Mashariki kuliko sehemu nyingine duniani.

Kwa mfano, nchini Tanzania wastani wa mtu mmoja kati ya watu 1,400 ana ualbino, wakati wastani wa kimataifa ni mtu mmoja kwa watu 20,000. Uelewa mdogo wa jamii kwa watu wenye ualbino na imani potofu (ushirikina) kuwa miili yao huwa na nguvu ya kuleta utajiri unaoelezwa kuwa chanzo kikubwa cha mauaji ya jamii ya watu wenye ualbino ili watumie viungo vya miili yao kupata utajiri jambo ambalo siyo kweli.

Utafiti unaonesha kuwa mauaji hayo yalishamiri kutokana na matakwa ya waganga wa kienyeji kuwaambia wateja wao kwamba viungo vyao hivyo huleta bahati ya kupendwa, maisha marefu na mafanikio katika biashara au uvuvi. Kuanzia mwaka 2000, vitendo hivi vilikithiri nchini na hasa nyakati za kuelekea kwenye uchaguzi mkuu, ambapo matukio kadhaa ya watu wenye ualbino kuuawa na kujeruhiwa kwa imani za kishirikina, yaliripotiwa.

Hali hii ililisukuma Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha sheria ya kuwalinda watu wenye ualbino, sheria ambayo hata hivyo wanaharakati wa haki za binadamu licha ya kupongeza bado wanaona ina upungufu kwa kuwa matukio ya kuuawa watu wenye ualbino yaliendelea kuripotiwa.

Tangu mwaka 2000, kumeripotiwa mashambulizi dhidi ya watu wenye ualbino zaidi ya 448 katika nchi 25 barani Afrika, vifo vilivyorekodiwa ni 172 na matukio 276 ya watu hao kujeruhiwa na sehemu ya viungo vya mwili kuondolewa. Baadhi ya matukio dhidi yao yanahusisha ukataji wa viungo vya mwili, ukatili dhidi yao, kubakwa na majaribio ya utekaji nyara.

Hata hivyo, baadhi ya mashirika yanayotetea watu wenye ualbino yanasema takwimu hizi ni sehemu tu ya matukio yaliyoripotiwa na kwamba kuna visa vingi havijaripotiwa. Ijapokuwa kwa sasa hali siyo mbaya kama mwanzo, bado visa kadhaa vimeendelea kuripotiwa ikiwemo tukio la Aprili 24, mwaka huu. Katika tukio hili, iliripotiwa kuwa, mwili wa mmoja wa watu wenye ualbino aliyekufa mwaka 2015 ulifukuliwa na baadhi ya mabaki kuchukuliwa na watu wasiojulikana.

Kaburi hilo lililofukuliwa lilikuwa la Aman Anywelwisye Kalyembe aliyekufa mwaka 2015 Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya na hadi sasa haijulikani mabaki ya mwili wake yamepelekwa wapi. Tukio hili limewafanya watu wenye ualbino nchini kumtaka Rais John Magufuli kuingilia kati wimbi la kufukuliwa kwa makaburi ya watu wenye ualbino. Chama cha Watu Wenye Ualbino Tanzania (TAS), kimeweka wazi kuwa watu wenye ualbino wameanza kuwa na hofu kwani hawajui nia na msukumo wa kufukuliwa kwa miili ya wenzao.

Katibu Mkuu wa TAS, Mussa Kibimba anasema malalamiko yao yanakuja mara baada ya matukio ya mfululizo ya kufukuliwa kwa makaburi mkoani Mbeya. Kibimba anasema mpaka sasa makaburi mawili yamefukuliwa mkoani Mbeya na haijajulikana sababu za kufukuliwa kwa miili yao na hata kujulikana masalio ya miili hiyo yanaenda wapi.

Anasema vitendo vya kufukuliwa makaburi hayo vimeibua hofu kwa watu wenye ualbino nchini. Watetezi wa haki za binadamu wanasema mashambulizi dhidi ya watu wenye ualbino yamepungua, lakini uvamizi sasa unaelekezwa katika kufukua makaburi yao. Matukio ya kufukuliwa makaburi yalianza kuripotiwa tangu mwaka 2016. 0685 666964 au bjhiluka@ yahoo.com

WAZIRI wa Nchi Ofi si ya Rais, Tawala za Mikoa ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi