loader
Picha

‘Ni hatari kumaliza misitu kwa kuigeuza mashamba’

WAKATI ninajiandaa kuandika makala haya niliwauliza Oscar Mbuza na Godfrey Lutego, wote wakazi wa Dar es Salaam ambao pia ni waandishi nguli wa habari, swali hili: Kwamba, takwimu zilizopo zinaonesha kuwa Tanzania hupoteza hekta 469,000 ya misitu kila mwaka, eneo ambalo ni sawa na mara tatu ya ukubwa wa jiji la Dar es Salaam. Unadhani ni kitu gani kinaongoza kwa kumaliza misitu? Mbuza alijibu: “Kinachomaliza misitu ni ukataji miti kwa ajili ya mbao na uchomaji mkaa.”

Lutego akajibu: “Kinachomaliza misitu nchini ni uchomaji wa mkaa.” Mtazamo huo wa Mbuza na Lutego ndio walio nao Watanzania wengi wakiwemo watunga sera na wawakilishi wa wananchi katika mihimili muhimu kama Bunge.

Lakini, endapo waandishi hao na watu wengine wenye mtazamo huo wangebahatika kuhudhuria warsha iliyoandaliwa kwa ajili ya maofisa kilimo, ardhi na misitu kutoka halmashauri 19 nchini, mtazamo wao leo kuhusu shughuli inayoongoza kwa kumaliza misitu nchini ungebadilika.

Katika warsha hiyo iliyofanyika mjini Morogoro mwishoni mwa wiki, washiriki walipata wasaa wa kusikia kuhusu utafiti uliofanywa hivi karibuni na ambao bado unaendelea, ukionesha kwamba kitu kinachomaliza misitu ni kilimo. Mkurugenzi Msaidizi wa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), Emmanuel Lyimo, aliyeshiriki utafiti huo, anasema asilimia 89 ya upotevu wa misitu nchini inatokana na shughuli za kilimo.

Anasema kwa mujibu wa utafiti huo, uvunaji mkaa huchangia uharibifu wa misitu kwa asilimia saba, ufugaji na moto kwa asilimia tatu huku ufyekaji misitu kwa ajili ya uanzishwaji wa mashamba mapya ya miti ukichangia kwa asilimia moja. Anasema utafiti wao uliofadhiliwa na Mfuko wa Critical Ecosystem Partnership Fund (CEPF) ulihusisha mahojiano na wananchi katika kujibu swali la nini kinasababisha uharibifu wa misitu sambamba na utumiaji wa picha za satellite na upigaji wa picha za kawaida katika maeneo 120 yanayohusisha wilaya 62 na mikoa 22 tofauti tofauti nchini.

CEPF ni muungano wa mashirika mbalimbali duniani yanayosaidia kuokoa maeneo ambayo ikolojia yake inakaribia kutoweka. Sekta nyingi zishirikishwe Lyimo anashauri wakati wa utengenezaji wa sera kuhusu matumizi ya ardhi, ni muhimu sekta mbalimbali zikashirikiana.

“Ni muhimu kuwe na ushirikiano wa sekta kama ya kilimo, sekta ya misitu, nishati, maji na sekta ya madini wakati wa kuandaa sera za matumizi ya ardhi,” anasemana kuongeza kuwa, hatua hiyo itasaidia kufanya sekta moja kutoingilia nyingine na kuiathiri. Mabadiliko ya tabianchi Kwa mujibu wa mtafiti huyo, endapo hakutakuwa na mkakati wa kukabiliana na tatizo la upoteaji wa misitu kutokana na kilimo, itakuwa vigumu pia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Tunaposhindwa kukabiliana na yanayosababisha mabadiliko ya tabianchi, tujue wananchi pia watakosa mazao (kutokana na ukame au mafuriko na na athari nyingine za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ongezeko la wadudu waharibifu wa mazao),” anasema. Anasema kilimo na misitu ni mambo yanayotegemeana kutoka na faida nyingi za misitu ikiwemo kuvuta mvua, kuhifadhi vyanzo vya maji na ekolojia ya eneo husika.

Mwaka huu jijini Dar es Salaam, Waislamu walilazimika kuombea mvua, hatua inayoonesha kwamba mvua zilichelewa sana kunyesha na kusababisha ukame unaochangiwa na uharibifu wa misitu na kusababisha mabadiliko ya tabianchi. Mvua zilizosubiriwa tangu Februari zilinaza kunyesha Mei huku baadhi ya wakulima wakilazima kupanda mbegu mara mbilimbili kutokana na kuozea ardhini kwa kukosa maji. Misitu zaidi kuvamiwa Anasema kuna maeneo walipita wakati wanafanya utafiti na kukuta watu wanachimba mizizi ya miti ili kuchoma mkaa.

“Hii inaonesha kwamba kama misitu iliyopo katika ardhi za vijiji itaisha kutokana na kubadilishwa kuwa mashamba, wananchi watahamia kwenye misitu inayomilikiwa na serikali kuu au ile ya halmashauri,” anasema. Taarifa ya Tathmini ya Misitu nchini ya mwaka 2015, inaonesha kuwa hekta milioni 21.6, sawa na asilimia 45 zinamilikiwa na serikali za vijiji na hekta milioni 15.48 (asilimia 35) zinamilikiwa na Serikali Kuu (TFS, TAWA na TANAPA).

Halmashauri zinamiliki hekta milioni 3.36 (asilimia 7), sekta binafsi hekta milioni 3.36 (asilimia 7), mataji wazi (General land) hekta milioni 2.4 (asilimia 5) na miliki nyingine ya misitu hekata milioni 0.48 (asilimia 1).

Misitu iliyo katika ardhi za vijiji ndio inayogeuzwa zaidi kuwa mashamba na ndio iko katika hatari zaidi ya kutoweka. Usimamizi shirikishi Lyimo anasema kitakachookoa misitu ya Tanzania, mbali na kuwa na sera zitakazodhibiti kilimo kisiendelee kumaliza ardhi za vijiji, ni pamoja na kuhakikishi vijiji vinakuwa na mipango ya matumizi bora ya ardhi na usimamizi shirikishi wa raslimali za misitu.

Anasema namna ya kuwafanya wananchi washiriki vizuri katika kulinda misitu yao ni pale wanapoona faida ya misitu hiyo kama inavyofanyika katika Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS). Anaishauri serikali kutenga bajeti kwa ajili ya kusaidia vijiji ambavyo vimekuwa na miradi mbalimbali ya kuhifadhi misitu ili pale miradi hiyo inapomalizika pesa hizo zisaidie katika kuifuatilia, kusimamia na kuiendeleza.

Lyimo anashauri nchi kujikita zaidi katika kilimo kinachotumia teknolojia katika maeneo ambayo tayari yametengwa kwa ajili kilimo na kuzalisha maradufu, ili kuepuka kuendelea kugeuza misitu kuwa mashamba. Kwa upande wake, Ofisa Misitu Mwandamizi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Emmanuel Msoffe anasema ipo haja ya kuangalia upya watu wanaomiliki maeneo ambayo yana misitu kutolazimishwa kuyageuza kuwa maeneo ya kilimo.

“Hapa Morogoro kuna watu wengi wanamiliki maeneo ambayo mengine yana misitu, lakini utaona wanaonekana kisheria kama hawayajaendeleza hadi watakapogeuza hiyo misitu kuwa ardhi kwa ajili ya kilimo. Kuna haja ya kuliangalia hili upya,” alisema. Mradi wa TTCS Mradi wa Kuleta Mageuzi ya Mkaa Tanzania (TTCS) uliojikita katika kuzalisha mkaa kwa njia endelevu unaanza kwa kuhakikisha kijiji kinakuwa na matumizi bora ya ardhi na hivyo msitu kujulikana ni upi na wapi maeneo ya kijiji kwa ajili ya shughuli zingine na makazi.

Kwa mujibu wa meneja wa mradi huo, Charles Leonard kutoka TFCG, mradi huo umelenga katika mambo matatu; kuhakikisha kunakuwa na usimamizi madhubuti wa raslimali za misitu, kuboresha maisha ya wadau katika mnyororo wa thamani na kuongeza juhudi za kulinda uharibifu wa mazingira. “Dhana kuu ya mradi ni kwamba, bado mahitaji ya mkaa ni makubwa nchini na itachukua miongo kadhaa watu kuhamia kwenye nishati mbadala kwa ajili ya kupikia hivyo lazima tuwe na uvunaji mkaa kwa njia endelevu,” anasema Leonard.

Akieleza hatua za mfumo huo wa kuzalisha mkaa endelevu, meneja huyo wa mradi anasema kinachoanza ni kukiwezesha kijiji kuandaa matumizi bora ya ardhi. “Mpaka sasa mradi umeviziwezesha vijiji 30 kuwa na matumizi bora ya ardhi ambapo takribani hekta 114,000 ziko katika mpango huo,” anasema. Hatua ya pili anasema, ni kutenga asilimia 10 tu ya msitu wa kijiji ambapo ndipo mkaa utakuwa unavunwa miaka yote huku asililia 90 ikiachwa kwa shughuli zingine.

Hatua ya tatu, Leonard anasema ni kutenga vitalu ndani ya msitu wa kijiji vyenye ukubwa wa mita 50 kwa 50 na ambavyo huvunwa kwa kuruka ruka, yani kikivunwa kitalu A, kinarukwa kitalu B. “Asilimia 10 ya msitu wa kijiji inatakiwa kutoa vitalu 1,000 ambapo vitalu 500 vinapaswa kuvunwa katika kipindi cha miaka 12. Hivi vikimalizika, vile vilivyokuwa vinarukwa vinaanza kuvunwa. Baada ya miaka 24 wanarudi tena kwenye vitalu vya awali kwani miti inakuwa imekuwa tayari kwa kuvunwa,” anasema.

Anasema miti katika eneo lililovunwa huota kwa njia ya asili kwa visiki kuchipua au kutokana na mbegu zilizokuwa zimevia kukua kutokana na kuzibwa na kivuli cha mti uliokatwa. “Tumekuwa tukifuatilia kwa kutumiwa watalaamu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), na kwa kweli miti hii ya miombo inaota vizuri sana katika maeneo yaliyokwishavunwa,” anasema.

Anasema uchomaji mkaa pia hufanywa kwa kutumia tanuri la kichuguu udongo lililoboreshwa linalotoa mkaa mwingi zaidi ya mara mbili ya tanuri la asili na ambalo mkaa wake ni mzito unaotumika kwa muda mrefu kupikia.

Wananchi pia hufundishwa kilimo hifadhi na kufungua mashamba darasa ili walime eneo dogo kwa mavuno mengi. Wanavijiji wavuna mamiloni Anasema mpaka sasa vijiji 22 katika wilaya tatu za Kilosa, Morogoro na Mvomero mkoani Morogoro vimejipatia Sh bilioni 1.4 kupitia mradi huo katika kipindi cha takribani miaka mitano. Anasema tangu uvunaji wa misitu umenza mwaka 2014, ingawa mradi ulianza mwaka 2012 wazalishaji wameshaingiza takribani Sh bilioni 1.2 huku halmashauri husika pia zikitia kibindoni zaidi ya Sh milioni 500.

Anafafanua kwamba mradi ulianza kwa kuhusisha vijiji 10 katika wilaya ya Kilosa kabla ya awamu ya pili kuongeza vijiji 20 na kuhusisha wilaya za Mvomero na Morogoro. Wanawarsha walitembelea vijiji viwili vinavyotekeleza mradi huo vya Matuli na Mlilingwa, Moroghoiro vijijini na kujionea namna vijiji hivyo ambavyo kabla ya mradi vilikuwa haviingizi pesa yoyote, sasa vimeingiza mamilioni.

Walijionea namna pesa hizo zinavyotumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo kama ujenzi wa shule, visima, kulipia bima za afya na pesa hizo pia kuutumika kulinda misitu. Mradi wa TTCS unasimamiwa kwa ushirikiano na mashirika matatu yasiyo ya kiserikali kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Uswisi. Mbali na TFCG, mashirika mengine ni Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (Mjumita) na Shirika la Kuendeleza Nishati Asilia (TaTEDO).

HIFADHI ya mazingira ni juhudi zinazofanywa na binadamu ili kuhakikisha ...

foto
Mwandishi: Hamisi Kibari

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi