loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tumsaidie Bashungwa kufikia azma ya Rais

HIVI karibuni Rais John Magufuli alitengua uteuzi wa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Josephat Kakunda baada ya kutoridhishwa na utendaji kazi wake.

Baada ya kutengua uteuzi wa Waziri huyo, Rais alimteua Innocent Bashungwa kuwa waziri wa wizara hiyo. Bashungwa awali alikuwa Naibu Waziri wa Kilimo.

Hiyo ni mara ya pili kwa Rais Magufuli kutengua uteuzi wa waziri katika wizara hiyo. Mwaka jana alitengua uteuzi wa Waziri Charles Mwijage kabla hajamteua Kakunda kushika nafasi hiyo.

Sababu za kumuondoa Kakunda, Rais Magufuli alitaja kuwa ni kushindwa kutafuta soko la korosho baada ya serikali kuzinunua zote na kuziweka kwenye maghala, wanunuzi wa zao hilo walipotaka kununua kutoka kwa wakulima kwa bei wanayoitaka wao, ambayo ni ya chini.

Changamoto kwa wakulima ni kama vile majibu yake yanapatikana katika Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, hivyo kuna uhusiano mkubwa katika wizara hizi.

Nakubaliana na mipango ya Waziri Bashungwa katika kuimarisha wizara hiyo, kwamba ni pamoja na kuimarisha viwanda na pia kuwepo na ushirikiano katika ya wizara hizo mbili. Sekta ya kilimo inabeba ajira ya zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania.

Akikabidhiwa wizara hiyo juzi, Waziri Bashungwa alisema haamini kushindwa katika utendaji kazi ambapo amejiwekea mikakati kadhaa ya kuanza nayo.

Nia ya Rais Magufuli ni kuifikisha nchi katika uchumi wa kati kupitia viwanda, hivyo namuelewa anapojitahidi kuhakikisha wizara hiyo inasimamia kazi zake.

Naungana na Waziri Bashungwa katika mikakati yake ambayo ni pamoja na kutaka Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Viwanda (TIRDO) na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo(SIDO) kuja na mkakati kuwawezesha wakulima kupata nyenzo ya kuboresha thamani katika mazao yao.

Kuna mazao mengi yanayolimwa hapa nchini lakini yanasafirishwa kama yalivyo na kwenda kuuzwa katika nchi nyingine, yanapofika huko yanaondolewa ughafi, kufungashwa na kuuzwa kwa nembo ya nchi zao.

Kwa kusafirisha mazao yakiwa ghafi si tu tunapoteza uhalisia kwamba yanazalishwa hapa nchini, lakini pia tunapoteza nafasi za ajira pamoja na kupoteza vitu vingine ambavyo vinapatikana ndani ya zao hilo ambavyo ni fedha pia.

Kwa taasisi hizo kujipanga na kuwa na mikakati kutawezesha kuongeza viwanda hapa nchini lakini pia kuwapatia nyenzo ambazo zitawawezesha wakulima kuzalisha zaidi, kuondokana na kilimo cha jembe la mkono kisicho na tija.

Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji inabeba mzigo mkubwa katika kufikia uchumi wa kati ambao anatupeleka Rais Magufuli.

Lakini pia Waziri Bashungwa amezungumzia mkakati wa ushirikiano kati ya idara ya masoko katika wizara hiyo na ile ya Kilimo.

Hii itamsaidia pia mkulima atakapozalisha atakuwa na uhakika wa kupata soko la mazao yake.

Kama ambavyo imetokea katika zao la korosho, wakulima wametimiza jukumu lao la kulima lakini changamoto inakuja katika uuzaji, jambo lililosababisha serikali kununua korosho zote na kutafuta soko ili kuwakomboa wakulima.

Kukiwa na mfumo mzuri kati ya Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda na Biashara itakuwa mkombozi na itakata mzizi wa tatizo hilo la soko la mazao. Kuna mazao mengi yanayozalishwa kwa wingi nchini lakini hakuna soko la uhakika.

MOJA ya shabaha ya kuundwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ...

foto
Mwandishi: Regina Mpogolo

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi