loader
Picha

Bandari Mtwara kuongeza uwezo

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA) kupitia Bandari ya Mtwara itakuwa na uwezo wa kuhudumia tani zaidi ya milioni moja za mizigo kwa mwaka kutoka tani 400,000 za sasa, mara ujenzi wa gati namba mbili utakapokamilika mwishoni mwa mwaka huu.

Bandari hiyo ambayo imeelezwa kuwa lango kuu la biashara au uchumi kwa ukanda wa kusini mara baada ya kukamilika kwa gati hiyo, imejipanga kuwahudumia sio tu wateja wa ndani ya nchi bali na wa nchi jirani za Malawi, Zambia na Msumbiji.

Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu bandarini hapo jana, Meneja wa Bandari ya Mtwara, Juma Kijavara alisema kukamilika kwa ujenzi wa gati namba mbili kutaifanya bandari hiyo pia kuwa na uwezo wa kuhudumia tani zaidi ya milioni mbili kwa mwaka katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Alisema bandari hiyo tangu ijengwe enzi za ukoloni mwaka 1953, ilivunja rekodi kwa kusafirisha tani 377,590 za mizigo katika Mwaka wa Fedha wa 2016/2017, huku mwaka 2018/19 ilisafirisha tani 363,286 na mwaka 2014/15 ilisafirisha tani 296,577.

Tofauti na gati zingine zilizopo nchini na nchi jirani, gati namba mbili linalojengwa katika Bandari ya Mtwara lina kina cha asili cha mita 13 maji yanapokupwa, jambo linaloifanya bandari hiyo kuwa bora katika ukanda wa kusini ikilinganishwa na kina cha mita 9.5 cha bandari za nchi jirani.

Akieleza kuhusu ujenzi huo, Mhandisi wa bandari hiyo, Norbert Kalembwe, alisema unatekelezwa na wakandarasi kutoka China ambao ni Kampuni za China Railway Construction Engineering Group (CRCEG) na China Railway Major Bridge Engineering Group Co. Ltd (CRMBEG) kwa gharama ya Sh bilioni 137.4 ambazo ni fedha za serikali, lakini pia wakandarasi hao wanafanya kazi chini ya mhandisi msimamizi ambayo ni Kampuni ya Inros Lackner ya Ujerumani.

Kwa mujibu wa Kijavara, shehena kubwa ya mizigo inayohudumiwa na bandari hiyo ni zao la korosho ambalo ndiyo zao kuu la biashara kwa mikoa ya kusini ya Mtwara, Lindi na Ruvuma. Shehana zingine ni saruji inayozalishwa na kiwanda cha Dangote.

“Gati hili linalojengwa lina urefu wa mita 300 na ujenzi umefikia asilimia 52, likikamilika litakuwa na uwezo wa kuhudumia meli zenye ukubwa wa tani 65,000 ikilinganishwa na gati la awali lenye uwezo wa kuhudumia meli zenye uwezo wa tani 45,000, lakini pia litakuwa na eneo la kuhifadhia mizigo lenye ukubwa wa mita za mraba 79,000 na uwezo wa kuhudumia tani zaidi ya milioni moja kwa mwaka,” alieleza.

Pamoja na kuhudumia shehena za mafuta yanayokuja kwa ajili ya mikoa ya Lindi na Mtwara, Meneja huyo alisema bandari yake pia imejipanga kusafirisha tani 500,000 za makaa ya mawe kwa mwaka, tani zaidi ya 50,000 za jasi na tani zaidi ya 300,000 za saruji kwa mwaka inayozalishwa na kiwanda cha Dangote.

Ofisa Utekelezaji wa bandari hiyo, Ibrahim Ruzuguma, alisema Bandari ya Mtwara inapokea wastani wa meli tatu za mizigo kwa wiki, hivyo kwa mwezi inapokea meli 12 ikiwemo meli moja ya mafuta kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ambayo inakuja bandarini hapo kila mwezi.

Kwa kuwa bandari ni sehemu ya uchumi wa nchi, Ofisa Ulinzi wa Bandari ya Mtwara, Khalid Kitentya, alisema wamewekeza akili, taaluma na fedha na katika kufanya hivyo, kitengo cha ulinzi bandarini hapo siyo tu kwamba kina jukumu la kuzuia uhalifu ukiwemo wizi wa mali za wateja na vitu vingine, bali pia kuhakikisha uchumi wa nchi uko salama.

Mkoa wa Pwani umebaini kuwa maonesho ya bidhaa zinazozalishwa viwandani ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera, Mtwara

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi