loader
Picha

Mateso mabasi mwendokasi yataisha lini?

USAFIRI wa mabasi yaendayo haraka maarufu mabasi ya mwendokasi, umekuwa tegemeo kubwa la usafi ri katika wilaya za Kinondoni na Ubungo Dar es Salaam.

Kwa sasa mabasi hayo yanatoa huduma katika ruti za Gerezani- Kimara, Gerezani –Morocco, Feri–Kimara na Feri-Morocco na ruti ya pembezoni ya Kimara-Mbezi Luis.

Lakini katika siku za karibuni, huduma ya mabasi hayo imekuwa na kero nyingi na Watanzania wamekuwa wakilalamika hadharani na kwenye mitandao ya kijamii.

Moja ya kero hizo ni uchache wa mabasi hayo wa mara kwa mara vituoni, hivyo kuzusha vurugu vituoni, ambapo abiria huingia kwa vurugu ndani ya mabasi hayo na kujazana kupindukia. Katika baadhi ya vituo, abiria hutumia madirisha badala la milango kuingia ndani.

Abiria wamekuwa wakikanyagana, kuibiana, kugusana maungo ya mwili, kukosa hewa, kuumizana na kuambukizana magonjwa.

Watu wanajazana vituoni na kukaa muda mrefu bila kuona gari na mfano mzuri ni vituo vya Kimara na Kariakoo, ambavyo vina watu wengi.

Hivyo, tunaiomba serikali kutafuta ufumbuzi wa haraka wa matatizo ya mtoa huduma wa sasa wa mradi huo (UDART) na moja ya matatizo yake ni uchache wa mabasi.

Inaelezwa kuwa kuna mabasi 70 aliagiza mtoa huduma huyo nje, na yanaozea bandarini kwa mwaka mmoja sasa, kwa madai hajalipa kodi. Kwa nini mabasi hayo 70 yaozee bandarini Dar es Salaam, wakati wakazi wa jiji hili hili, wanakanyagana kwenye mabasi kwa uchache wa mabasi?

Kwa nini mabasi hayo 70 yasiruhusiwe kutoa huduma na mtoa huduma huyo alipishwe kodi hiyo pole pole hadi iishe?

Mbona mwaka jana tulishuhudia wadaiwa sugu wa kodi, wakipewa muda wa miezi sita kulipa malimbikizo ya madeni yao bila riba?

Kuna nini kwenye mradi huu wa mwendokasi?. Tunakumbuka kuwa viongozi mbalimbali, wamewahi kutembelea mara kadhaa mradi huu na kutoa ahadi kem kem za kumaliza matatizo ya mwendokasi.

Baadhi yao ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tamisemi, Seleman Jaffo.

Tunahoji mbona matatizo ya mwendokasi bado yapo pale pale? Wakazi wa Dar es Salaam wanaotumia mabasi ya mwendokasi, wataendelea kuteseka hadi lini? Wasubiri hadi lini? Ni nani atasikia kilio chao? Kuna nini kwenye mradi huu wa mwendokasi?

Hivyo, kinachotakiwa ni mamlaka zinazohusika, zisaidie UDART kutatua haraka matatizo, hata kama kuna mwekezaji mwingine mpya, anatarajiwa kuletwa karibuni.

Tusikubali mradi huu uendelee katika hali ya sasa, bali tuuboreshe zaidi kwani umebadilisha usafiri wa jiji kwa kuufanya kuwa wa kisasa na wa kimataifa. Tusikubali kurudi nyuma!.

WAUMINI wa dini ya Kiislamu nchini jana na leo wameungana ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi