loader
Picha

Fursa daftari la wapigakura itumiwe kwa manufaa

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inafanya jambo jema sasa hasa ikizingatiwa kuwa, asiyeziba ufa, hulazimika kujenga ukuta.

Tume sasa inaziba nyufa au dalili za nyufa inazoziona katika suala la upigaji kura hususan kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura. Kabla ya kwenda mbali, ikumbukwe kuwa Tanzania inaelekea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa miezi michache ijayo na pia Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2010.

Ninasema NEC inafanya vizuri kuziba nyufa kwa kuwa imekuwa na mwendelezo wa vikao vyake ikikutana na wadau mbalimbali kama moja ya mikakati yake kupata mawazo ya wadau huku ikizidi kujipanga kwa ajili ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura unaotarajiwa kuanza Julai mwaka huu. Katikia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, vituo 37,814 katika mikoa 31 vitahusika kwa kazi hiyo.

Kifungu cha 15 (5) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na Kifungu cha 21 (5) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura ya 292, vinaitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura mara mbili baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu kabla ya kuingia uchaguzi mkuu mwingine.

Kimsingi, hii ni nafasi muhimu kwa wadau mbalimbali kutoa mchango wa mawazo yao mintarafu namna ya kunenepesha zaidi demokrasia nchini licha ya ubora uliopo na ndiyo maana, juzi NEC ilikutana na viongozi wa dini.

Hata hivyo, hii ni nafasi muhimu kwa wote wenye sifa za kujiandikisha katika uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura kufanya hivyo ili waingie na kuwa watu wenye sifa ya kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi wowote wa kisiasa nchini kwa mujibu wa taratibu.

Ikumbukwe pia kuwa, miongoni mwa sifa za mtu kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi wa kisiasa, ni pamoja na kuwa na akili timamu, kuwa mwenye umri usiopungua miaka 18 na kwa mujibu wa taratibu, uwe umejiandikisha kama mpigakura na kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura.

Hii ni kusema kuwa, kazi hii itakapoanza mwezi ujao, iwe ni fursa kwa wapenda demokrasia kujiona ‘wamesimama wapi’ mchakato halisi wa uchaguzi utakapoanza. Kujiandikisha katika daftari hili ni muhimu kwani hufungua milango kwa mtu kuchaguliwa au kumchagua mtu anayeona anafaa kuwa kiongozi katika jamii.

Kufanya hivi, kunaondoa kasumba ya baadhi ya watu kuwadanganya wagombea wao kwa kulundikana kwenye mikutano ya kampeni, kuwaimbia, kuvaa fulana na kupeperusha bendera za vyama vyao, lakini wakati huo watu hao wakiwa hawana sifa za kupiga kura hivyo, hawawezi kuwachagua kuwa viongozi.

Hali hiyo kwa mtazamo wangu, ndiyo huwafanya wagombea waliodanganyika na mlundikano wa watu kwenye mikutano ya kampeni wakiwamo watoto wa shule, kumbe wengi wakiwa na sifa za kupiga kura matokeo yake, wengine kuamua kujiliwaza kwa kilio kuwa kura zao zimeibwa. Wanasahau ukweli kuwa, kuwapo kwa demokrasia nchini na kuonekana inatendeka hakumaanishi tu, mgombea au chama fulani kushinda; kwamba inapotokea kinyume, yawe malalamiko ya kuonewa au kuibiwa kura; hapana.

Demokrasia kama ilivyo haki, ni pamoja na kushindwa katika ushindani uliopo na kukubali matokeo kisha, kumuunga mkono aliyeshinda. Hiyo ndiyo demokrasia yenye afya kwa kila mtu. Hili ndilo linanifanya niwahimize wanasiasa na vyama vyao kuhakikisha wanawashawishi na kuwahimiza wananchi wafuasi wao, kuhakikisha wanajiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa mujibu wa kanuni na taratibu zilizipo ili baadaye pia, wajiandikishe kuwa wapigakura katika uchaguzi husika.

Vikao hivi baina ya NEC na wadau mbalimbali wa uchaguzi nchini, ni muhimu wanaopata fursa, wavishiriki kikamilifu na kutoa dukuduku zilizopo ili zitafutiwe majawabu sahihi kwa kufuata taratibu sahihi na za kiungwana. Hili litaifanya Tanzania ipae zaidi katika uwanja wa demokrasia duniani. Ikumbukwe kuwa, uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 unaohusisha rais, wabunge na madiwani ni uchaguzi wa sita katika mfumo wa siasa wa vyama vingi ulioanza nchini mwaka 1992.

Uchaguzi Mkuu wa Kwanza katika mfumo huo ulifanyika mwaka 1995 ukifuatiwa na ule wa mwaka 2000 uliomweka Benjamin Mkapa kuwa Rais wa vipindi viwili akiwa Rais wa Awamu ya Tatu akitanguliwa na Ali Hassan Mwinyi na Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius K. Nyerere. Kisha, ukafuatiwa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 na wa mwaka 2010 uliomweka madarakani Jakaya Kikwete kuwa Rais wa Awamu ya Nne.

Uchaguzi mkuu wa tano katika mfumo huu wa siasa ulifanyika mwaka 2015 na kumweka madarakani Rais John Magufuli ambaye hadi sasa, Watanzania wanazidi kufaidi matunda ya kura zao kutokana na utumishi wake usiobagua wala kupendelea mtu wala kikundi cha watu kinachofanya mambo kiungwana na kwa mujibu wa taratibu, kanuni na sheria za nchi.

Mpango wa NEC kukutana na wadau mbalimbali unastahili kupongezwa na kuendelezwa kwani unawapa fursa wadau kupongeza, kukosoa na kuonesha njia sahihi pale penye dosari maana waungwana na walio makini siku zote huwa hawangalii waliangukia wapi, bali kama kweli walianguka, basi walijikwaa wapi. Ushiriki kamilifu wa wadau katika mchakato mzima wa uchaguzi, utatoa fursa kwao na vyama vyao kushiriki ipasavyo katika uchaguzi na hivyo, kuondoa visingizio na malalamiko kwa wanaopata kura zisizotosha kuingia madarakani maana hao mara zote ni kama mbaazi ambao kila unapokosa maua, unasingizia jua.

Ndiyo maana katika mkutano wa juzi, viongozi wa dini waliishauri Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuhakikisha inatatua changamoto zilizobainika kujitokeza katika mchakato wa uchaguzi wowote uliopita Kinachofurahisha ni kuwa, katika mkutano huo na viongozi wa dini, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage, anasema katika uchaguzi ujao Tume itasimama imara zaidi kuhakikisha sheria na taratibu zote za uchaguzi zinafuatwa. Kubwa zaidi, anafahamisha kuwa, NEC itaunda kamati ya maadili ili kushghulikia malalamiko ya wagombea.

Anasema wasimamizi wa uchaguzi wakiwamo wakurugenzi wanapaswa kuhakikisha wanatenda na kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria na kuzingatia haki kwa kuwa hakuna aliye juu ya sheria za nchi. Ndiyo maana wakati wapenda demokrasia wote nchini wanataka kuwapo na uchaguzi wa haki na ulio huru zaidi; wa uwazi kama ambavyo imekuwa ikifanyika, kuondoa msongamano vituoni, huku hekima ikitawala kwa watendaji wa tume, wagombea, vyama na wapigakura, ni vema pia uvunjaji sheria unaofanywa na yeyote hususan wagombea na vyama usipewe nafasi.

Sheria hizi zinazoweza kuvunjwa kwa kisingizio chochote na zikiachwa zikaleta athari kwa taifa, ni pamoja na kudhibiti wagombea au vyama kutoa lugha za matusi na uchochezi, na kutoruhusu mikusanyiko na maandamano yasiyo na baraka za kisheria. Hayo yanaweza kuibadili nchi kutoka kuwa ‘Tanzania Nyeupe’ yaani Tanzania ya Amani na kuifanya iwe ‘Tanzania Nyekundu’ yaani Tanzania ya vita na kumwaga damu. Hakuna Mtanzania halisi anayetaka Tanzania iwe Tanzania Nyekundu.

Wadau wachache wanaopata fursa ya kukutana na tume na hata wale wasiokutana nayo lakini wana uelewa na matashi mema kwa nchi, waendelee kuelimisha umma namna nzuri zaidi ya kufaidi matunda ya amani na uongozi bora kupitia ushiriki wao kamilifu na makini wa uchaguzi wa kisiasa.

Kila mmoja azingatie kuwa, kuwapo kwa demokrasia nchini hakumaanishi mtu au kikundi fulani cha watu kufanya atakavyo hata kuvunja taratibu, kanuni na sheria za nchi. Izingatiwe kuwa, kabla, wakati na baada ya uchaguzi, hakuna anayepaswa kuachwa avunje sheria za nchi kwa kisingizio chochote. Ndiyo maana ninasema: “Fursa daftari la wapigakura itumiwe kwa manufaa zaidi.”

TANGU maambukizi ya virusi vya corona yabishe hodi nchini Machi ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi