loader
Picha

Ummy azindua mpango wa masikio na usikivu

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amezindua mpango mkakati wa taifa wa miaka minne wa masikio na usikivu na kuahidi kuwa serikali itahakikisha huduma hizo zinatolewa hadi ngazi ya chini.

Akizungumza wakati wa kuzindua mkakati huo uliokwenda sambamba na kambi ya wazi ya kutolewa huduma kwa jamii ya wenye matatizo ya masikio na usikivu jijini hapa, Ummy alisema tatizo hilo lipo katika jamii ya Watanzania. “Pamoja na kuwa hakuna takwimu rasmi za kitaifa, lakini takwimu ndogondogo zinaonesha asilimia tatu ya watoto walio shuleni wana matatizo ya masikio na usikivu wa hatua mbalimbali, lakini pia liko kwa watumishi wa migodini na wale wanaofanya kazi kwenye viwanda,” alisema.

Alisema kutokana na tatizo hilo, serikali iliamua kuanza kutoa matibabu ya kibingwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo katika kipindi cha miaka miwili watoto 26 wametibiwa kwa gharama ya Sh milioni 35 huku mamia wakiwa kwenye foleni.

“Kabla ya kuanza kutoa tiba hiyo hapa nchini, serikali ilikuwa ikipeleka wastani wa watoto 13 kila mwaka ambapo kila mmoja alikuwa akigharimu kati ya Sh milioni 80 hadi 100, lakini sasa tumeweza kuokoa fedha kwa kutoa huduma hi,” alieleza. Alisema kutokana na uhitaji wa huduma hiyo ni mkakati wa serikali kuhakikisha huduma hizo zinatolewa katika ngazi za chini na hospitali zingine za mikoa na wilaya na kuutumia mkakati huo kama mwongozo.

Ummy alisema pia serikali imeweza kuongeza wataalamu na madakatari wa pua, koo na masikio kutoka wataalamu 11 waliokuwapo mwaka 2009 hadi kufikia kuwa na wataalamu 46 mwaka 2018, ingawa idadi hiyo bado ni ndogo. Aidha, Ummy alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa jamii kutunza masikio, kuwa na matumizi sahihi ya dawa, kuwa makini na vijiti vya kusafishia masikio ambavyo ni moja ya visababishi vya matatizo ya masikio na usikivu.

“Pia tujihadhari na matumizi ya spika za masikioni hasa kwa vijana, unaweza kuona unakwenda na wakati lakini kumbe tunatengeneza kizazi chenye matatizo ya masikio na usikivu,” alisema.

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba kutoka wizarani, Dk Grace Magembe alisema watatumia mkakati huo katika kupanua utoaji wa huduma za pua, koo na masikio. Mmoja wa waanzilishi wa taasisi ya Starkey, Bill Austin alisema matatizo waliyobaini katika kambi za wazi ni ya masikio na usikivu ambayo yanaweza kutibika endapo tu mgonjwa atapatiwa tiba mapema.

Taasisi ya Starkey Foundation for Ear and Hearing care, kabla ya kufanya Dodoma ilifanya kambi kama hiyo jijini mwanza ambapo watu zaidi ya 2,000 walipewa vifaa vya kusaidia usikivu.

Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa kushirikiana na Taasisi ya ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi