loader
Picha

TLS yashauri vyuo vikuu kufundisha madini, mafuta

CHAMA cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimevishauri vyuo vikuu nchini kuona umuhimu wa kufundisha masuala ya mazingira, madini na mafuta katika mitaala yao, ili kuijengea jamii uelewa mpana katika maeneo hayo.

Rais wa TLS, Dk Rugemeleza Nshala alisema hayo Dar es Salaam jana na kuongeza kuwa kwa kufanya hivyo, itasaidia kudhibiti mianya ya wizi kwa rasilimali hizo, huku jamii ikipata manufaa katika nyanja mbalimbali.

Akizungumza kuhusu mafunzo ya rasilimali zinazokwisha, kwa mawakili wa serikali, binafsi, wadau wa mazingira na madini kutoka serikalini yaliyofadhiliwa na nchi ya Canada, Dk Nshala alisema uelewa kuhusu masuala ya madini ni mdogo kwa sababu vyuo vingi hapo awali vilikuwa havifundishi masuala hayo na kuhamasisha kwa sasa kubadilika na kufundisha. Alisema kwa sasa nchi ina miradi mingi ya uchimbaji mafuta na madini, hivyo ni vyema kuwajengea uwezo wa kielimu wananchi wake ili kuhakikisha nchi inanufaika na rasilimali zake.

“Ni vyema kufanya jitihada za kuwajengea uwezo wa kielimu kuhusu masuala ya madini, mafuta na mazingira wananchi wetu ili waweze kufahamu haki zao na sheria zilizopo,” alisema Nshala na kuwataka wanafunzi pia kuona umuhimu wa kujikita katika maeneo hayo kwa manufaa ya baadae. Alisema ipo haja sasa kwa vyuo vingi hapa nchini kuanza kutoa elimu hiyo ili pengo la uelewa mdogo wa masuala ya mazingira na madini likazibwa.

Nshala alisema Watanzania wanaoishi maeneo ya madini wakifahamu sheria, kupigania haki zao, majukumu ya serikali za vijiji yakatekelezwa itasaidia rasilimali zilizopo kutumika kwa manufaa ya jamii.

Kwa upande wake, Mshiriki ambaye ni Mwanasheria kutoka Baraza la Mazingira (NEMC), Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, Naomi Joshua, alisema mabadiliko ya sheria ya mazingira ya mwaka 2017 yamechagiza uwezo wa shughuli za kimazingira hasa katika sekta ya madini. Alisema NEMC imekuwa ikijitahidi kufuatilia miradi mbalimbali na kuangalia athari za kimazingira na namna ya utekelezaji kabla ya kuanzisha kwa mradi.

“Wanaokwenda kinyume tumekuwa tukiwachukulia hatua na tutahakikisha utekelezaji wa miradi unafanyika bila kuathiri mazingira,” alisema Naomi. Alisema mafunzo hayo ana imani yatawasaidia wanasheria wengi kufahamu mambo mbalimbali kuhusu mazingira, madini na mafuta kabla na baada ya kusaini mikataba ya uchimbaji madini. Mwanasheria wa Serikali, Godfrey Nyamsenda alisema, ni vyema kulinda na kuangalia masuala ya mazingira kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ametoa maagizo ...

foto
Mwandishi: Lucy Lyatuu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi