loader
Picha

CBCTC Chuo pekee cha utoaji mafunzo uhifadhi maliasili kwa jamii

UTALII ni sekta muhimu kwa ukuaji wa uchumi nchini Tanzania. Inachangia zaidi ya asilimia 17 ya pato la taifa. Katika mwaka wa fedha wa 2016/2017, sekta ya utalii ilichangia asilimia 17.5 ya pato la taifa huku ikiliingizia asilimia 25 ya fedha za kigeni.

Katika kipindi hicho, ilichangia ajira 500,000 za moja kwa moja na nyingine milioni moja za watu kujiajiri kwa shughuli mbalimbali zinazoigusa sekta hiyo. Kutokana na umuhimu wa sekta hiyo, Serikali imeendelea kupanga na kutekeleza sera mbalimbali kuendelea kuiinua, ikiwa ni pamoja na kuimarisha vyuo vinavyotoa elimu na mafunzo ya utalii nchini.

Chuo cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii (CBCTC) kilichopo katika kijiji cha Likuyu Sekamaganga, wilayani Namtumbo, mkoani Ruvuma kimeendeleza juhudi hizo za serikali kwa kutoa wahitimu wenye weledi katika sekta hiyo. Hivi karibuni kimefanya mahafali ya mafunzo kwa askari wanyamapori wa vijiji (VGS) huku mgeni rasmi akiwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu.

Akizungumza katika mahafali hayo, Kanyasu aliwaasa askari kulinda na kutunza rasilimali za taifa katika maeneo yao ili ziwe endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho. Kanyasu aliahidi kushughulikia changamoto zinazokikabili chuo hicho, ikiwamo miundombinu chakavu na kumalizia jengo la maktaba aliloweka jiwe msingi na kusema, serikali itahakikisha chuo hicho kinakuwa na sifa ya chuo cha kati.

Anasema kozi ya waongoza watalii inayoanzishwa katika Chuo cha Likuyu, mtaala wake utakuwa unafanana na vyuo vingine viwili nchini vivyotoa kozi hiyo alivyovitaja kuwa ni Chuo cha Pansiansi Mwanza na Mweka, Kilimanjaro.

“Serikali imejipanga kufungua utalii wa Kusini, hivyo kozi ya waongozaji watalii ni muhimu kuwa na silabasi moja ili kupata watu watakaokuwa na sifa ya kutoa huduma zinazofanana kwa watalii ili kuwafanya watalii kuendelea kufika Tanzania,’’ alisema Naibu Waziri Kanyasu.

Alisema serikali inafungua utalii Nyanda za Juu Kusini na Kusini kuhakikisha utalii unakuwa zao namba moja kwa ajili ya kuongeza mapato ya fedha za kigeni na uchumi wa Tanzania kwa sababu uchumi wa utalii bado upo wazi.

Alisema utalii si kuangalia wanyama na kupanda milima pekee, bali nchini Tanzania upo utalii wa aina nyingi ukiwemo wa ngoma, vyakula, nyumba za asili, zana za kilimo kama jembe la mkono linaloshangaza wageni wengi kutoka nje ya nchi. Kwa mujibu wa Kanyasu, changamoto kubwa iliyokuwa inaikabili sekta ya utalii nchini ni miundombinu hafifu.

Anasema Rais John Magufuli amenunua ndege, amejenga barabara za lami na hivi sasa anaboresha na kujenga viwanja vya ndege vilivyo muhimu kwa utalii. “Kazi yetu kubwa sasa kama Wizara ni kuangalia wapi tuwekeze ili watalii waje na kutuletea fedha za kigeni hivyo kuchangia mapato na kukuza uchumi wa Taifa letu’’, amesema Kanyasu.

Mkuu wa Chuo cha CBCTC, Jane Nyau anasema katika mahafali hayo kuwa, chuo hicho kilichoanzishwa mwaka 1995 ni pekee cha utoaji wa mafunzo ya uhifadhi wa maliasili kwa jamii barani Afrika. Anasema hapa nchini katika vyuo vya uhifadhi, hakuna chuo kinachotoa mafunzo yanayofanana na chuo hicho hali hiyo ndiyo inakifanya kuwa ni chuo cha kipekee nchini. Katika mahafali ya kozi namba 64/2019 ya askari wanyamapori wa vijiji (VGS), wanachuo 20 wamehitimu mafunzo ya askari wanyamapori wa vijiji kwa miezi mitatu.

Anasema licha ya chuo hicho kutoa kozi za mafunzo hayo ya askari wanyamapori wa vijiji na mafunzo ya viongozi wa serikali na kamati za maliasili za vijiji kwa mwezi mmoja, kuanzia Julai 2019 chuo hicho kitaanza kutoa kozi ya astashahada ya awali ya waongozaji watalii kwa muda wa mwaka mmoja. “Kozi hii itatolewa kuendana na mkakati unaoendelea wa serikali wa kukuza utalii katika Ukanda wa Kusini, mtaala wa kozi hiyo umeshakamilika na tayari umeshathibitishwa na Baraza la Usimamizi wa Vyuo vya Ufundi (NACTE),” anasema Nyau.

Akizungumzia mafunzo yaliyohitimishwa, Mkuu wa chuo anasema, mafunzo hayo yametolewa chini ya ufadhili wa Shirika la Wildlife Conservation Society (WCS) na askari hao wamepatiwa mafunzo kupitia utekelezaji wa mkakati mpya wa kulinda shoroba mbili zilizoko katika maeneo yao. Anazitaja shoroba hizo kuwa ni Ruaha kupitia Piti hadi Katavi na ya pili ni inayotoka Ruaha kupitia Rungwa na Ipole.

Licha ya mafunzo ya VGS, Nyau anayataja mafunzo yanayoendelea ya viongozi na wajumbe wa kamati za maliasili na vijiji pamoja na baadhi ya wenyeviti na wananchi toka vijiji mbalimbali na kwamba, mafunzo hayo yanafadhiliwa na WWF yakishirikisha washiriki 40 kutoka Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori. Anazitaja jumuiya hizo kuwa ni Mbarang’andu, Kimbanda, Kisungule katika Wilaya ya Namtumbo, Chingoli na Nalika wilayani Tunduru; pamoja na baadhi ya wananchi na wenyeviti kutoka vijiji vya Likuyu, Mchomoro, Mtelemwahi, Lusewa, Likusanguse, Sasawala, Amani, Matepwende, Msisima na Ligunga.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Chuo huyo, mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa chuo hicho mwaka 1995 ni kutoa mafunzo kwa wananchi 4,633, kuanza ujenzi wa maktaba na chumba cha kompyuta kwa kutumia fedha za ndani. Kwa sasa zinahitajika Sh milioni 23.4 kukamilisha ujenzi huu. Mengine ni kupitia ufadhili wa USAID, chuo kimefanikiwa kuandaa mtaala wa kozi ya waongoza watalii na kudurusu mpango mkakati wa kuandaa mpango wa biashara wa chuo.

Anayataja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kutoa mafunzo ya kitaaluma kwa wakufunzi na kutoa vifaa vya mafunzo na mfumo wa umeme ambavyo ni genereta moja, kompyuta mpakato, viona mbali, mahema 16 na vitabu 40 kwa ajili kozi ya waongoza watalii. Pamoja na mafanikio hayo, Nyau anazitaja changamoto zinazokikabili chuo hicho kuwa ni upungufu mkubwa wa watumishi na uchakavu wa majengo yakiwemo mabweni, uchakavu wa magari, nyumba za watumishi, jiko na bwalo la chakula.

Anasema karibu majengo yote yalirithiwa kutoka kwa wakimbizi wa Msumbiji miaka ya 1980 na kwamba, tangu wakati huo hayajawahi kufanyiwa ukarabati. Mratibu wa shughuli za uhifadhi kwa jamii (WCS), Anna Kimambo anasema WCS imefadhili mafunzo hayo kutokana na changamoto ya uvamazi katika maeneo ya uhifadhi hivyo, yanalenga kutekeleza kwa vitendo kanuni ya uhifadhi ya maeneo ya shoroba iliyopitishwa mwaka 2018 ili kulinda maeneo ambayo hayajaharibiwa sana.

Kaimu Mkurugenzi wa Wanyamapori Tanzania, Canisius Karamaga, anasema CBCTC Namtumbo kimewekwa na serikali ili kutoa mafunzo kwa wahifadhi na kutoa elimu kwa askari wa wanyamapori vijijini hivyo chuo hicho kinatoa elimu katika maeneo yaliyo nje ya mfumo rasmi wa uhifadhi. Anasema chuo hicho kinasaidia hifadhi kwa jamii na shoroba ambapo maeneo hayo yote ni ardhi za vijiji kwa kuwa yanaunganisha hifadhi moja kwenda nyingine na kwamba, iwapo shoroba hizo zitafungwa, wanyama watakuwa wanazaliana ndani ya kizazi hivyo watatoweka.

“Wanyama wanavyobadilishana vinasaba kati ya hifadhi na hifadhi, hapo ndipo tunapopata uhifadhi endelevu na rasilimali endelevu ndipo panapoleta umuhimu wa kuhifadhi maeneo yaliopo nje ya mfumo rasmi wa uhifadhi chini ya vijiji,’’ anasema Karamaga.

Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Sophia Kizigo anasema robo tatu ya wilaya hiyo ni hifadhi ikiwemo eneo la Pori la Akiba la Selous na kwamba, katika shoroba inayounganisha Selous na Niassa Msumbiji, kuna hifadhi tatu ndani ya Wilaya ya Namtumbo ambazo ni Mbarang’andu, Kisungule na Kimbanda.

Anasema Wilaya ya Namtumbo inahusika katika mradi mkubwa wa umeme wa Rufiji kwa sababu Mto Luegu unaochangia asilimia 19 katika Mto Rufiji, vyanzo vya mto huo vinaanzia Selous, hivyo wilaya hiyo ina kazi kubwa ya kulinda vyanzo vya maji vya mto huo ili mradi wa umeme uwe endelevu. Mawasiliano ya Mwandishi wa makala haya ni baruapepe: albano.midelo@gmail. com. Simu 0784765917

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ametoa maagizo ...

foto
Mwandishi: Albano Midelo

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi