loader
Picha

Historia na hali ya utalii wilayani Babati

MANYARA ni miongoni mwa mikoa ya Tanzania iliyojaliwa vivutio vingi vya utalii kuliko sehemu nyingi Afrika. Hata hivyo, mkoa huu una utalii mkubwa usiofahamika. Makala haya yanaelezea historia ya utalii mkoani Manyara takribani miaka 100 iliyopita wakati Babati ikiwa eneo maarufu la utalii nchini.

Fuatilia.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya kihistoria, matajiri na watu maarufu kutoka Ulaya na Marekani walifi ka Babati na baadhi yao wakafanya utalii wa picha, uwindaji pamoja na utalii wa utamaduni, lugha na maisha ya watu. Mwaka 1937 mchezaJI filamu maarufu, Mwingereza Baron Bror, aliyecheza filamu iliyoitaja Babati Manyara kama mbingu ya duniani (The Heaven on Earth) alikuwa mwindaji na mwongozaJI watalii Manyara.

Wateja wake wakubwa ni pamoja na mwana wa Mfalme wa Uingereza, baadae alikuwa Mfalme Edward wa VIII wa Uingereza. Mwaka 1925, Bror aliachana na mkewe. Alianzisha kampuni ya utalii iliyopitwa Tanganyika Guides Ltd. Mteja wake mkubwa wa utalii Babati alikuwa Major Richard Cooper (D’Cooper), raia wa Marekani aliyemiliki visima vya mafuta.

D’Cooper hatimaye alimiliki shamba kubwa la kahawa lenye ukubwa wa maili saba magharibi mwa mji wa Babati maarufu Singu Farm. Kaburi lake lipo Babati katika Kijiji cha Sigino. Alitalii Babati na Man-yara kwa miezi mitatu na kufurahia vivutio vya utalii. Alijenga uwanja wa ndege kupokea wageni kutoka Ulaya na Amerika waliokuja kutalii Manyara.

Karibu na Dabil tajiri wa ukoo wa Kifalme wa Scotland Venderbilt, alijenga nyumba ya kupumzika kubwa iliyopokea watalii kutoka Ulaya waliokuja Tanganyika. Inaelezwa pia kuwa, tajiri mwingine wa Scotland aliishi katika shamba kubwa la kahawa lililoko umbali wa maili mbili kutoka katika mji wa Babati na kuufanya mji huo kujaa wageni, watalii na wafanyabiashara wakubwa kutoka Amerika, Ulaya hasa Uingereza na Sweden.

Watalii walitembelea sana Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Hifadhi ya Jamii ya Burunge. Mwaka 1934, Hemingway aliyekuwa rafiki aliyetambulishwa kwa D’Cooper, alifika Babati kwa utalii wa uwindaji na alilala katika nyumba ya D’Cooper. Hermingway alielekea Gallapo kwenda katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire akiongozwa na waongozaji watalii wawili ambao ni Bror na Phillip Brixen.

Eneo la Bagara palijengwa klabu kubwa ya watalii karibu na Ziwa Babati iliyoitwa Fig Tree Club. Mwongozaji watalii, Blixen alikusanya wakulima wakubwa wa Babati mwaka 1929 akitokea safarini Congo na kumwalika Gavana wa Tanganyika kuja kuzindua utalii eneo lote la magharibi mwa Arusha yaani Manyara ya leo. Gavana alifika Singu kuzindua kanda mpya ya utalii ya Manyara kitovu kikiwa Babati.

Matajiri watalii waliendesha magari kutoka Dar es salaam kwenda Babati kutalii Manyara. Mmoja wao ni mwanamke, raia wa Sweden, Eva Dickson aliyeendesha gari kukatiza Jangwa la Sahara hadi Dar es Salaam hatimaye Babati kukutana na Bror mwongozaji watalii. Mkurugenzi Mkuu wa hoteli ya kitalii ya Good Life iliyoko mjini Babati, Richard Ngalewa, anakiri kuwepo vivutio vingi mkoani humo na kwamba, amevutiwa kuwekeza katika huduma ya chakula na malazi (hoteli).

Anasema hatua hiyo inayotokana na historia ya utalii mkoani Manyara anaosema kiuwekezaji, unafanya vizuri. Hoteli yake ipo eneo la Bagara Miyomboni karibu na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara na ni kichocheo cha maendeleo ya eneo hilo na pato la taifa hasa kutokana na hali nzuri ya hewa na mji kuwa karibu na makao makuu ya nchi (Dodoma) yenye kupokea wageni wengi wa ndani na nje ya nchi. Anasema utalii ni kitendo cha kutembelea maeneo yenye vivutio kinachovutia hisia, kinachoongeza uelewa (kujifunza), mapumziko.

Anavitaja baadhi ya vivutio vilivyoko Manyara kuwa ni pamoja na Mbuga ya Wanyama ya Tarangire, Ziwa Manyara, Mlima Hanang na Mlima Kwaraa. Uchunguzi wa makala haya umebaini kuwa, yapo pia maeneo ya kijiografia kama chanzo cha Bonde la Ufa, Ziwa Babati lenye viboko weusi na wekundu, samaki wa aina mbalimbali. Hili anasema ni ziwa zuri kwa kupanda mitumbwi ya kienyeji na lipo pia Ziwa Gidawar (ziwa la chumvi) na Kisima cha Mungu (The Well of God) kilichopo kijijini Sigino.

Vivutio vingine vinatajwa kuwa ni Bwawa la Tope lililopo Kiru lenye maajabu ya watu kukaa juu yake bila kuzama ingawa nondo ya futi 40 huzama eneo la Maswari, Ziwa Balangda (lenye magadi), mazalia ya wanyama jamii ya nyani yaliyopo Babati na mazalia ya fisi Sigino maarufu Kliniki ya Fisi (fisi huonekana huko kipindi cha kuzaa).

Vingine ni maporomoko ya maji ya Tururu michoro ya mapangoni yaliyopo Kijiji cha Ufana na Imbilili wilayani Babati pamoja na utalii wa kitamaduni kama kuwepo kwa makabila ya Wamasai, Wahadzabe na Wabarbaig wanaosifika kwa kudumisha mila na desturi zao, nyimbo, ngoma na vyakula vya asili.

Ofisa Utalii wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Francis Lazaro, anasema idadi ya watalii imekuwa ikiongezeka kutoka nje ya nchi kutokana na ubora na upekee wa vivutio vilivyopo Babati. Anasema mwaka jana watalii 186 walitembelea na watalii kutoka ndani ya nchi ni 64 wanaokwenda kutembelea Ziwa Babati lenye viboko na ndege wengi.

“Ziwa Babati,” anasema: “Limepewa kipaumbele cha kuwapeleka watalii kutokana na uwepo wa viboko 48…” Hii ni kwa mujibu wa Sensa ya Mwaka 2016 iliyofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (Tawiri).

Katika ziwa hilo watalii hupenda kutumia ngalawa katika safari zao. Mdau wa utalii wilayani Babati, Ally Msuya anasema utalii wilayani humo ulianzia katika familia yake. Kwamba, baba yake mzazi alikuwa mwindaji wa wanyama na mwajiriwa wa mmiliki wa visima vya mafuta wa D’Cooper.

Msuya alianza shughuli za utalii mwaka 1992 baada ya kubaini watalii wengi waliokuwa wakitembelea Babati walikuwa wanataka kutembelea Hifadhi za Wanyama za Tarangire na Ngorongoro. Shughuli ya kwanza ya kuwatembeza watalii hao katika maeneo hayo ilikuwa ni kutengeneza gari maalumu lililotobolewa juu ili watalii waweze kuona wanyama kwa urahisi.

Gari hilo lilikuwa la kwanza nchini kutobolewa juu likitokea Babati. Anasema licha ya kutototangazwa ipasavyo, bado utalii uliopo mkoani Manyara ni mkubwa ukilinganishwa na nchi nyingi za jirani.

Anafahamisha kuwa, mtoto wa Malkia Elizabeth wa Uingereza, Prince Charles, alikuwa na mashamba makubwa yenye umiliki kutoka kwa malkia huyo pamoja na uwanja wa ndege katika eneo ambalo kwa sasa limejengwa ofisi za Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Bawasa). “Nilikatishwa tamaa ya kuendeleza utalii niliouanzisha, lakini nashukuru serikali yetu ambayo sasa inasisitiza uwekezaji katika utalii, imenifufua nianze upya kwa kuwa kitu kinachowavutia watalii wengi wanaokuja Babati na katika huu mkoa kwa jumla ni kilimo na hali ya hewa hasa katika Wilaya ya Mbulu yenye milima na miinuko mbalimbali ya kuvutia,” anasema Msuya.

“Babati kuna vivutio vingi lakini ninachoshangazwa ni kuona vivutio vingi haviendelezwi… ukiangalia kwenye majengo ya zamani, kulikuwa na hoteli maalumu kwa ajili ya watu maalumu wakiwa wamevaa tai na viatu, bila kuvaa hivyo huruhusiwi kuingia katika hoteli hizo hata kama una fedha, majengo hayo yamebaki kwenye madaftari pekee na hayajulikani popote,” anasema.

Anaitaka serikali kuboresha miundombinu ya majengo ya kitalii yaliyokuwepo awali ili kuchochea utalii na kuongeza kipato katika halmashauri husika tofauti na hali ilivyo sasa ambapo vivutio vingine vya majengo vimebomolewa na kupoteza mandhari yake.

“Wilaya ya Babati na watu wake wasingekuwa masikini wa kipato kama walivyo kwani kila kitu kilichokuwa kikitokea katika sekta ya utalii ilikuwa na historia ya chimbuko la Babati,” anafafanua Msuya.

Naye Mwenyekiti taasisi maalumu ya kutangaza utalii mkoani Manyara, ijulikanayo kama Manyara Regional Tourism & Conservation Apex, (Taasisi ya Utalii Mkoa wa Manyara) Erick Nyoni, anabainisha kuwa kupitia taasisi hiyo iliyo katika hatua za mwisho za usajili Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, anasema taasisi yake itasaidia kutangaza fursa za utalii zilizopo.

Anasema hizo ni pamoja na kutoa ajira, kuanzishaji wa vyuo vya utalii, kukuza ushiriki wa matamasha mbalimbali ya utalii nchini na kupanga na kuitisha matamasha watakayoyaandaa ili kufahamika duniani kupitia kampuni mbalimbali za utalii. “Taasisi yetu ikisajiliwa tutafanya uzinduzi rasmi wa Tamasha letu la kukuza utalii ambapo tutawashirikisha watu mbalimbali wakiwemo viongozi, wadau wa utalii na wananachi kwa ujumla kukuza uelewa wa utalii wilayani Babati na hata mkoa kwa jumla,” anasema.

Kwa mujibu wa Nyoni, mikakati ya kuutangaza Mkoa wa Manyara kuwa kitovu cha utalii ni pamoja na kuandaa dokumentari ya vivutio vyote vya utalii mkoani humo na kuvitangaza kwa njia mbalimbali, kuanzisha na kumiliki tovuti ya kutangaza utalii na kuandaa mapokezi ya wageni nje ya nchi kwa niaba ya wadau wa utalii walio wanachama kwa njia ya kielektroniki (ebooking).

Mikakati mingine ni kutangaza kampuni za biashara za wadau (wanachama) ndani na nje ya Tanzania, kuiomba na kuishauri serikali kufungua geti Mamire ili wageni wapitie Minjingu na kutokea Mamire kuja mjini Babati, kuanzisha maonesho ya utalii ya Mkoa wa Manyara yatakayoitwa Manyara Tourism Trade Fair na kujenga Makumbusho ya Mkoa wa Manyara ili kuhifadhi urithi na historia ya mkoa huo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Fortunatus Fwema, anasema hatua ya kufufua utalii uliosahaulika itasaidia kuendeleza utalii utakaokumbukwa na kujulikana kwa vizazi vijavyo. “Katika kuvifufua vivutio hivi kutasaidia kuvilinda ili visiharibiwe na kuvirithisha vizazi vijavyo kwani faida za uwekezaji kwa wageni watakaoingia hapa ni kuongezeka kwa biashara za malazi, vyakula na vinywaji kwa hoteli ya kitalii na nyumba za kulala wageni,” anasema Fwema.

Anasema: “Wastani wa kipato kinachotokana na utalii kwa mwaka katika halmashauri hii ni asilimia tano hadi kumi kwa sasa, lakini tukivifufua tutafika wastani wa asilimia 50 hadi 70 kwa mwaka na baada ya miaka miwili ijayo, tunatarajia kufikia wastani wa asilimia 100, hii ni hatua nzuri ya kujivunia.” Anasema manufaa si kwa halmashauri, mkoa na taifa tu, bali pia wananchi wa kawaida watakaofungua migahawa na kuendesha biashara ndogo ndogo.

“Watalii wengine hupenda kuishi na wananchi wa kawaida, kula vyakula vya kawaida na hata vya asili, hawa wanaitwa ‘budget tourists) wasio na fedha nyingi, lakini wanapenda kutalii,” anasema. Fwema anatoa mwito kwa wananchi wakazi wa Babati, Mkoa wa Manyara na taifa kwa jumla, kuwa wakarimu kwa wageni na kuepuka kabisa kuwaona wageni kuwa ni maadui.

Mfanyabiashara ya nguo wilayani Babati, Akonay Boay, anasema idadi ya watalii ikiongezeka itasaidia wafanyabiashara wanaouza nguo kwa watalii kuuza kwa wingi hasa vitenge, kanga na batiki. “Tunanatarajia kupitia utalii hapa Babati, kutakuwepo biashara mpya kama uanzishwaji, uboreshaji na upanuzi wa hoteli za kitalii, migahawa, maduka ya kubadilisha fedha za kigeni, maduka ya vinyago, mikeka, vikapu kupitia ubunifu wa watu wa ndani,” anasema Boay.

HIFADHI ya mazingira ni juhudi zinazofanywa na binadamu ili kuhakikisha ...

foto
Mwandishi: Theddy Challe

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi