loader
Picha

Amunike- Hakuna wa kututisha

KOCHA wa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars, Emmanuel Amunike amesema ana matarajio makubwa ya kupata matokeo mazuri katika mechi ya leo dhidi ya Senegal.

Stars ipo mjini Cairo ikishiriki fainali za 32 za Michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa mara ya kwanza baada ya miaka 39, na leo itakuwa kwenye Uwanja wa Al Salaam nje ya mji wa Cairo kumenyana na Senegal katika mechi ya ufunguzi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Amunike raia wa Nigeria alisema anafahamu ugumu wa mechi iliyo mbele yake, lakini anaamini ameshamaliza kila kitu na kazi iliyobaki ni ya vijana wake.

“Mashindano haya sio rahisi, kila timu iliyofuzu ina uwezo ikiwemo Tanzania, hivyo tunatarajia kupata upinzani mkubwa kwasababu zimekutana timu zote nzuri na zina uwezo,” alisema.

Mechi hiyo inachukuliwa moja ya mechi kubwa kwenye michuano hii na ikisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka, huku wengi wakiipa nafasi kubwa Senegal, lakini nahodha wa Stars Mbwana Samatta amesema kila kitu kinawezekana na hakuna wa kuwatisha.

“Hakuna wa kututisha, kila kitu kinawezekana, tunachofanya ni kumheshimu kila mmoja tunayekutana naye, lakini sio kwamba tunaogopa, Senegal ni bora lakini na sisi ni bora pia ndio maana tumekutana kwenye michuano hii,” alisema.

Alisema, anajua hamu ya mashabiki nyumbani Tanzania ni kuona wakifanya vizuri nao hawatawaangusha.

“Hatutawaangusha, miaka mingi hatujacheza michuano hii tangu itokee kwa mara ya kwanza, tunajua wote nyumbani wana hamu ya kupata matokeo mazuri, watuombee tu, mwalimu keshamaliza kila kitu kama alivyosema tutapambana,” alisema.

Meneja wa Stars, Daniel Msangi aliliambia gazeti hili kuwa timu iko vizuri hakuna majeruhi zaidi ya Aggrey Morris ambaye ameondolewa kwenye michuano hiyo kutokana na kuumia.

“Wachezaji wote ambao mwalimu atapanga kuwatumia kesho (leo) wako fiti, hatuna majeruhi mwingine, kwa hiyo wenzetu huko nyumbani wasiwe na wasiwasi,” alisema Msangi.

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho, Afrika ...

foto
Mwandishi: Zena Chande, Cairo

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi