loader
Picha

Mkapa apongeza ubunifu waliosoma Ndanda

Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa anatarajiwa kuungana na wahitimu wengine wa shule kongwe ya Sekondari Ndanda ya Masasi, Mtwara kuitembelea shule hiyo Septemba 27, mwaka huu kwa ajili ya Siku ya Wahitimu wa shule hiyo iliyoanzishwa miaka 91 iliyopita.

Mkapa alisoma Ndanda kwenye miaka ya 1950, amethibitisha kuwa ataungana na wahitimu wengine wa shule hiyo Septemba 27.

Ametoa ahadi hiyo alipokutana na kuzungumza na viongozi wa Umoja wa Wahitimu wa Shule ya Sekondari Ndanda (UWAHISSENDA) waliokwenda kuutambulisha umoja huo ofisini kwake jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Amesema, kwa kuwa alisoma Ndanda, anajiona ana wajibu wa kuungana na wana umoja wengine walioanzisha wazo la kuitembelea shule yao ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wa shule katika maisha yao.

“Hili ni wazo la kupongezwa sana. Hongereni kwa ubunifu na uthubutu wa kutambua umuhimu wa kule mlikopata elimu. Ni wachache sana wanaokumbuka mambo kama haya,” amesema Mkapa.

Kwa wahitimu hao, hii itakuwa mara ya pili kwenda Ndanda, kwa kuwa mwaka jana walikwenda kwa mara ya kwanza na kuzindua umoja huo wakiwa shuleni hapo na kukabidhi vitabu vyenye thamani ya takribani Sh milioni 5, wakapanda miti, wakazungumza na wanafunzi wa sasa na pia kushiriki katika shughuli shuleni hapo, ikiwa ni pamoja na kufyatua matofali.

Mwenyekiti wa umoja huo, Yohana Kasawala amemshukuru Rais Mstaafu kwa kuridhia kuwa mwanachama mpya na kukubali kuungana na wanafunzi wengine wa zamani kwenda shuleni hapo.

Ametoa mwito kwa wahitimu wengine kuona fahari ya kusoma Ndanda na hivyo wajitokeze kufanikisha Siku ya Wahitimu Ndanda.

Umoja huo uliasisiwa mwaka 2015 kupitia mtandao wa kijamii wa Whatsapp na tayari una wanachama zaidi ya 150, wenye malengo ya kutanua wigo wa ukaribu hata baada ya kuhitimu masomo, kuinuana kiuchumi na pia kushiriki katika kuijengea uwezo shule yao.

“Daima umoja ni nguvu, utengano ni dhaifu, nasi tumeona ni vyema tukatumia mshikamano huu kama fursa ya kujiimarisha kiuchumi. Tuna ndoto nyingi…ni suala la muda tu, lakini mwelekeo wetu ni mzuri na kwa sasa tunafikiria kuanzisha kampuni ya mikopo midogo midogo yaani Microfince Company. Siku za usoni tunaweza kufikiria hata kuanzisha benki…,”amesema Kasawala.

Shule ya Ndanda, ilianzishwa mwaka 1928 na imeshatoa wahitimu zaidi ya 15,000 wakiwemo waliowahi kushika nyadhifa mbalimbali nchini akiwemo Rais Mkapa.

Wengine ni aliyewahi kuwa waziri mwandamizi katika Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Utawala wa Rais Jakaya Kikwete Hawa Ghasia, na Naibu Waziri wa Nishati kwenye Serikali ya sasa Subira Mgalu.

TIMU ya Taifa ya Soka ‘Taifa Stars’ inatarajiwa kushuka dimbani ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi