loader
Picha

Gati Bandari Mtwara litakavyofungua fursa za kiuchumi Kusini, nchi jirani

UCHUMI wa Mkoa wa Mtwara kwa miaka mingi umekuwa ukitegemea kilimo cha zao la korosho kama zao kuu la biashara. Kupitia korosho, wananchi wamefanya mambo mbalimbali makubwa na ya kimaendeleo ukiwemo ujenzi wa nyumba za kisasa na biashara mbalimbali.

Kwa kuwa dhana ya uchumi ni mtambuka kati ya shughuli ya kiuchumi na nyingine, Serikali imeona ni vyema iwekeze katika ujenzi wa gati jipya na la kisasa katika Bandari ya Mtwara ili kuunganisha mkoa huo na mikoa mingine.

Hii itaufungua zaidi kiuchumi mkoa huo na kuunganisha kibiashara na nchi jirani za Kusini zikiwemo za Malawi, Msumbiji, Zambia na Namibia. Ujenzi wa gati namba mbili katika bandari hiyo ni sehemu ya mpango wa serikali kupitia Mamlaka ya Usimamzi wa Bandari Tanzania (TPA) kuziboresha na kuziimarisha bandari zake zote nchini ili zihimili ushindani wa kibiashara katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na kusini mwa Afrika.

Gati hilo namba mbili linajengwa na serikali kwa gharama ya Sh bilioni 137.4 na litakamilika ndani ya mwaka huu. Kukamilika kwake kutaiwezesha bandari hiyo kuhudumia tani za mizigo zaidi ya milioni moja kwa mwaka kutoka tani laki nne za sasa. Meneja wa Bandari ya Mtwara, Juma Kijavara, anasema sifa pekee ya gati hilo ni kwamba, limejengwa mahali ambapo kuna kina kirefu cha maji cha asili kinachofikia mita 13 wakati maji yanapokupwa jambo linalowezesha meli zenye uzito mkubwa kutia nanga wakati wowote.

Kijavara anabainisha kuwa moja ya shehena kubwa ya mizigo inayohudumiwa na bandari hii ni zao la korosho. Anaitaja bidhaa nyingine inayofuatia kuwa ni saruji inayozalishwa na Kiwanda cha Dangote pamoja na mafuta yanayoingizwa kupitia bandari hiyo kwa ajili ya Mkoa wa Lindi na Mtwara.

“Gati hili litakuwa na urefu wa mita 300 na likikamilika litakuwa na uwezo wa kuhudumia meli zenye uzito wa tani 65,000 ikilinganishwa na gati la sasa lenye uwezo wa kuhudumia meli zenye uwezo wa tani 45,000, pia litakuwa na eneo la kuhifadhia mizigo lenye ukubwa wa mita za mraba 79,000 na uwezo wa kuhudumia tani zaidi ya milioni moja kwa mwaka,” anaeleza Kijavara.

Uwezo wa Bandari ya Mtwara kwa sasa katika kuwahudumia wateja unakidhi viwango vinavyotakiwa kutokana na kuwa na vifaa vya kisasa na vya kutosha. Kaimu Ofisa Utekelezaji Mwandamizi wa Bandari ya Mtwara, Ibrahim Ruzuguma, anasema shughuli za msingi za kila siku za Idara ya Utekelezaji bandarini hapo ni kupakua na kupakia meli katika gati, kuhifadhi mizigo kwa muda pamoja na kukabidhi mizigo inayohifadhiwa kwa wateja.

Ruzuguma anasema: “Tuna vifaa vingi vya kutosha kuweza kuwahudumia wateja wetu saa 24. Tuna winchi kubwa inayotembea yenye uwezo wa kunyanyua tani 100 za mzigo na nyingine mbili zenye uwezo wa kunyanyua tani 50 na tani 25 kila moja.”

Anaongeza: “Pia, tuna trekta (TT) nane za kubeba mizigo na makontena, forklift zenye uwezo wa kubeba tani tatu hadi tano zipo nane na zenye uwezo wa kubeba tani 12 hadi 42 zipo tatu pamoja na mzani wa kupimia mizigo.” Kutokana na uwezo huu, Ruzuguma anasema Bandari ya Mtwara imeweza kusafirisha tani 229,397 za korosho kwenda kwenye masoko ya nje ya nchi ikiwemo India na Vietnam katika msimu wa 2017/2018 pamoja na saruji kwenda Zanzibar, Visiwa vya Comoro na nchini Msumbiji.

“Hayo yote ni mafanikio ya uwezo wa Bandari ya Mtwara ambayo ni muhimu kwa uchumi na maendeleo ya watu wa mikoa ya Kusini ya Lindi, Mtwara na Ruvuma; pamoja na nchi jirani za Kusini zinazotumia bandari hii kusafirishia mizigo yao,” anasema. Ruzuguma anasema kwa utaratibu waliojiwekea, Bandari ya Mtwara inatakiwa kuhudumia makontena 250 kwa saa 24, lakini kutokana na umuhimu wa kuhudumia mizigo kwa haraka, bandari inahudumia makontena 315 kwa saa 24.

Ofisa Utekelezaji huyo anaongeza kuwa, kwa kuwa bandari yao siyo kisiwa, wanafanya kazi kwa kushirikiana na wadau wengine wa bandari wakiwemo mawakala wa meli, mawakala wa ushuru na forodha. Anazitaja baadhi ya taasisi nyingine ambazo ni wadau wa bandari kuwa ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC), Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) na vyombo vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha wateja wanahudumiwa kwa wakati, katika usalama na bila usumbufu.

Katika utekelezaji wa kazi hizo zote, suala la teknolojia ya habari na mawasiliano (tehama) haiwezi kuwekwa kando. Ofisa Tehama wa Bandari ya Mtwara, Khalphan Yakub, anasema mifumo ya Tehama bandarini hapo imeimarishwa ili kusaidia shughuli za kila siku za uendeshaji wa bandari. Shughuli hizi ni pamoja na kuingiza meli bandarini, upakuaji na upakiaji wa mizigo, pamoja na malipo mbalimbali yanayofanywa na wateja au mawakala wa meli. Imebainika pia kuwa, ukubwa na wingi wa shughuli katika Bandari ya Mtwara pia unahitaji ulinzi madhubuti ili kudhibiti vitendo vya wizi, na hata kuhakikisha usalama wa mizigo ya wateja na usalama wa bandari kwa jumla.

Umuhimu wa haya yote ndio unayomfanya Ofisa Ulinzi na Usalama katika Bandari ya Mtwara, Kharid Kitentya kusema kuwa, wanao wajibu wa kuhakikisha bandari iko salama kwa kuwa bandari ni sehemu nyeti ya uchumi wa nchi. Anatanabaisha kuwa, dhana ya kudhibiti ulinzi inabeba mambo mengi lakini makubwa ni matatu ambayo ni pamoja na kuhakikisha wafanyakazi wako salama, mali za wateja ziko salama, na hata miundombinu ya bandari ikiwemo njia ya kuingilia meli, majengo na vifaa viko salama.

Ili haya yote yaweze kutekelezeka, anasema wamewekeza vya kutosha katika rasilimali watu kwa maana kwamba Idara ya Ulinzi ina askari wa kutosha na vifaa zikiwemo kamera 38 za CCTV. Kamera hizi zina uwezo wa kuangalia usalama wa bandari yote saa 24 kwa kumulika kila kinachofanyika bandarini hapo, kumwona kila anayeingia na kutoka bandarini na zaidi sana bandari nzima imezungushiwa uzio.

“Suala la ulinzi ni uchumi, huwezi kutofautisha kati ya uchumi na ulinzi kwa sababu kama hakuna usalama uchumi hauwezi kuwepo, hivyo tumetoka kwenye ule ulinzi wa kawaida wa kudhibiti uhalifu pekee na tumeingia kwenye ulinzi wa uchumi, kwa hiyo lazima tuwekeze akili zetu, taaluma zetu na fedha ili tuwe na ulinzi wa kutosha,” anasisitiza Kitentya.

Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Bandari ya Mtwara (Dowuta), Jerome Gabriel, anasema chama hicho kina wajibu wa kuhakikisha haitokei migogoro ndani ya bandari pamoja na kuishauri menejimenti namna bora ya kushughulikia kero za wafanyakazi. Gabriel anasema wafanyakazi wanakitumia chama kwa kupeleka matatizo yao yanayowasilishwa katika menejimenti kama vile masuala ya maslahi ya wafanyakazi na vitendea kazi na kupatiwa ufumbuzi.

HIFADHI ya mazingira ni juhudi zinazofanywa na binadamu ili kuhakikisha ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi