loader
Picha

Vanila; ‘Dhahabu ya kijani’ inayopata hekaheka Kagera

VANILA ni zao linalojulikana zaidi mkoani Kagera kama ‘dhahabu ya kijani’ kutokana na kuwa mkombozi wa wakulima wengi. Hii ni kwa kuwa, ukiwa na miche japo mitano, ni kama vile tayari una dhahabu shambani kwako.

Tangu mwaka 2015 dhahabu ya kijani (vanilla) imekuwa mkombozi hali iliyochochea kasi ya kilimo cha zao hili kiasi kwamba, kijana wa miaka 20 au mzee wa miaka 70 kumiliki Sh milioni 20 hadi 30 ni jambo la kawaida hasa katika msimu wa mavuno. Kimsingi, vanila ni zao linaloweza kufanya mabadiliko makubwa na kuinua uchumi katika familia, jamii na taifa kwa jumla.

Kadri muda unavyopita ndivyo idadi ya wakulima inavyoongezeka kwani mpaka mwaka 2013 Mkoa wa Kagera ulikadiriwa kuwa na wakulima 600 wa vanilla 600, lakini idadi hiyo imeongezeka na sasa wakulima wa zao hilo ni zaidi ya 6,000. Zao hili linalimwa katika sehemu yenye kivuli hasa kwenye migomba au kwenye miti na linahitaji kiasi cha mwanga kuwa sawa na kiasi cha kivuli; yaani kwa asilimia 50 kwa 50.

Vanila inapopandwa, huwekewa mti aina ya jatrofa ili kukua kwa kupanda mti huo na mazao yake ni kama maharage. Hadi sasa bei ya vanila kwa walanguzi wa vanila changa ni kati ya Sh 20,000 hadi 30,000 kwa kilo moja. Mwaka 2017/18 bei ya vanilla mkoani Kagera ilifikia kati ya Shi 100,000 hadi 150,000. Katika siku za nyuma, vanilla iliwahi kuzalishwa mkoani Kagera hadi kufikia tani 103.

Katika kipindi hicho, bei ya vanila ilikuwa chini hadi kufikia Sh 4,500 kwa kilo moja. Kwa sasa zinazalishwa tani 10 hadi 12 za zao hili. KILIMO CHA VANILA KAGERA Kilimo cha vanila mkoani Kagera huwafanya wakulima wengi kulala katika mashamba yao au kuajiri vibarua kwa muda na kungoja mazao hayo yakomae shambani ili kulinda shamba usiku na mchana.

Katika miaka ya nyuma, wakazi wa Kata ya Kanyigo iliyopo wilayani Missenyi hawakuona umuhimu wa kulima vanila na badala yake, wakajikita katika mazao mengine kama kahawa na ndizi, lakini sasa kuna wakulima 1,500 wa vanilla wanaolenga kujiinua kiuchumi na kuongeza pato la taifa. Mpaka sasa kata hii kupitia Shirika la Maendeo Kanyigo (Kadea), imeunda umoja wa wakulima unaolima mazao matatu ili kujikwamua kiuchumi ambayo ni kakao, chai na vanila.

Shirika hili linahimiza walau kila mwananchi kuwa na zao mojawapo kati ya hayo na kuachana kabisa na kasumba ya kulalamikia uchumi huku wengine wakikalia kusema hakuna fedha wakati hawana cha kuuza.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wakulima wa Kata ya Kanyigo, Yese Mshobozi, anasema mwitikio ni mkubwa japo changamoto ni baadhi ya watu wasiopenda kufanya kazi ambao wengine, hushiriki vitendo vya wizi vinavyowatesa wakulima na kurudisha nyuma kasi ya maendeleo ya wakulima hao. Anasema uwepo wa wizi katika mashamba ya vanilla umesababisha kuitishwa kikao cha dharura chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Marco Gaguti na Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, Denice Mwila ili kuweka mikakati itakayoimarisha ulinzi wa zao hilo na kuongeza uzalishaji wake.

Kikao hicho kiliwashirikisha wakulima takriban 2,000 kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Missenyi waliokutana na Mkuu wa Mkoa katika Kata ya Kanyigo. Miongoni mwa mambo makubwa yaliyodaiwa katika kikao hicho, ni pamoja na mikakati imara ya kuwanufaisha wakulima na kuinua uchumi wa mkoa, badala ya wananchi kutegemea mazao kama ndizi na kahawa pekee. Hii ni kwa kuwa mazao hayo yamekuwa yakilimwa kwa mazoea, hivyo kutomnufaisha mkulima kutokana na uwezekezaji mdogo na teknolojia duni katika mnyororo wa thamani hadi sokoni.

Mkuu wa mkoa alipofika Kanyigo, pia alitembelea na kukagua shamba la vanila la Mwalimu Jovin Mbanga na baada ya hapo, alikutana na wakulima na kusikiliza kilio chao hususan kuhusu kero ya wizi wa vanila changa na marando katika mashamba. Ilidaiwa kuwa, vanilla inapoibwa shambani, huuzwa nchi jirani ya Uganda.

Wakulima hao walimweleza Mkuu wa Mkoa (Gaguti) kuwa, changamoto kubwa inayowakabili ni wizi wa vanila, hali inayowalazimisha kulala katika mashamba usiku mzima ili kulinda mazao yao yasiibwe. Ilielezwa kuwa, wizi huo hufanywa na baadhi ya Watanzania wasiokuwa wazalendo wanaoshirikiana na wafanyabiashara kutoka nje nchi kwa kupewa mitaji ya kununulia vanila za wizi, hali inayowafanya kuwahujumu Watanzania wenzao.

Changamoto nyingine walizomwambia Mkuu wa Mkoa, wakulima walisema ni kutokuwa na masoko rasmi ya kuuza vanila inapokomaa na kuvunwa sambamba na wanunuzi wa vanilla kutosajiliwa na kutambulika kiserikali ili mwananchi mwenye vanila, auwauzie kupitia soko maalumu yaani, kwa mnunuzi maalumu. Baada ya kusikiliza kero hizo za wakulima, mkuu wa mkoa huyo aliagiza kila mmoja kuhakikisha vanila inakuwa na muda maalumu wa kuvunwa katika mashamba na kwamba, kutakuwa na vituo maalumu kama masoko ya kununulia vanila.

Alisema ni marufuku na kosa kubwa kwa mfanyabaishara yeyote kwenda kwa wakulima moja kwa moja kununua zao hilo. “Sisi kama serikali hatujafikia uamuzi wa kumfunga kamba kila mwananchi kulima, isipokuwa kwa kuwa kuna soko la kutosha, kila mwananchi aone umuhimu na atumie fursa zilizopo kulima na kujiinua hivyo maamuzi ninayoyatoa kuanzi sasa ni kwamba, mwananchi yeyote atakayekamatwa na vanilla kabla ya tarehe ya kuvunwa kutangazwa atachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani na kufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi,” anasema Gaguti.

Anasema bila wakulima wa vanila kujiunga kwa njia ya ushirika na kutambuliwa, hata kubaini wezi itakuwa vigumu hivyo ni vyema wakulima wa vanilla wajiunge katika ushirika wa vyama vya msingi hali itakayowasaidia katika mambo mengi likiwamo hili la kubaini wezi wa mazao yao shambani. Aidha, Gaguti alisema hali hiyo itawapa soko la uhakika la kuuza mazao (vanila) ambayo tayari imeongezwa thamani na hivyo, kupata bei nzuri zaidi. Alisema hali hiyo pia itaweka urahisi zaidi kwa Serikali kuwasimamia kama ushirika kuliko mwananchi mmoja mmoja.

Mkuu wa mkoa anawataka wafanyabiashara wote zikiwamo kampuni zinazojihusisha na ununuaji wa vanila kujisajili na kupewa leseni ya kununua zao hilo kuliko ilivyo sasa. Akazitaka pia kampuni zinazotoa ruzuku kwa wakulima, kununua vanila kwa wakulima kwa kadiri ya bei ya soko, badala ya kuwapunja na kuwanyonya wakulima.

Akawataka watendaji wa vijiji na kata kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kikamilifu kama wanataka kuendelea kubaki kazini hasa jukumu la ulinzi na usalama kwa mfumo wa Nyumba Kumi Bora za Usalama ambapo wezi wa vanila watabainika kirahisi kila eneo. Wakulima Erick Godison na Deogratias Tibakilana wanasema mbele ya mkuu wa mkoa kuwa, wezi wa vanila wanajulikana kwani vijiji vilishafanya upigaji kura na kuwabaini wezi ambao majina yao yalipelekwa kwa mkuu wa wilaya ya Missenyi.

Walishauri watu waliotajwa katika kura hizo kuhusika na wizi wa vanila wahojiwe ili wabainishe hizo vanilla wanazitoa na kuziuza wapi wakati hawalimi. Mkuu wa Mkoa anamwagiza Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, kuwachukulia hatua wote waliotajwa wakituhumiwa kuhusika na wizi wa vanila. Katika mkutano huo, Mwila (Mkuu wa Wilaya) anawataka wananchi wilayani kwake wakiwamo wakulima wa vanila katika Kata ya Kanyigo, kubadilika kwa kuwa wizi mwingine wa vanila hutokea ndani ya familia.

Mwila anatoa mfano kuwa, unakuta shamba ni la baba na akitoka kwenda pengine Bukoba Mjini kufanya shughuli zake mama au mtoto anavuna vanilla haraka haraka na kuziuza na baba akirudi, anaambiwa vanila zimeibwa.

TIMU ya Taifa ya Soka ‘Taifa Stars’ inatarajiwa kushuka dimbani ...

foto
Mwandishi: Diana Deus

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi