loader
Picha

Tujipange kutomeza mimba za utotoni

HABARI kwamba uongozi wa Mji wa Kasulu umejipanga kuhakikisha unatokomeza tatizo la mimba za utotoni katika wilaya yao, ni ya kuigwa kwa nchi nzima kwa kuwa ni njema kwa wote wenye mapenzi mema na watoto.

Tunasema ni jema kwa kuwa tatizo la mimba za utotoni si tu kwamba linakera, bali ni tishio kwa maisha ya watoto ambao ndio wanaandaliwa kuwa taifa la kesho.

Hivi sasa mimba za utotoni ni tatizo ambalo limekuwa sugu. Kwanza, watoto wanashindwa kuendelea na masomo kwa kuwa sera ya elimu haikubali mtoto mwenye mtoto kuendelea na masomo lakini mbaya zaidi watoto hawa wanakosa mwelekeo wa maisha.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba wanaowapa mimba watoto, hawana malengo nao.

Wakishawapa mimba, hakuna makubaliano yoyote yanayokuwa yamefikiwa wakati huo, hivyo kuwaacha na ‘mizigo’ inayowalemea watoto ambao kwa hakika, hawana uwezo wa kulea mimba na watoto wanaozaliwa kwa uhakika.

Mkakati ambao sasa Wilaya ya Kasulu imejiwekea katika kupambana na tatizo hili wa kujenga mabweni ya wasichana na kutoa elimu kwa wazazi, haunabudi kuenea katika mikoa na wilaya zote ili kunusuru kizazi hiki cha kesho.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Jumuiya za Serikali za Mitaa wa Mkoa wa Kigoma, Twalib Salehe, wilaya yao ili iweze kupambana na tatizo la mimba za utotoni, imeanza na mikakati ya ujenzi wa mabweni ya wasichana katika shule za sekondari mbili, za Muba na Kasange.

Twalib anasema mpaka sasa katika wilaya yao, kuna kesi 19 za wanafunzi kupewa mimba na kati ya hao, wanafunzi saba ni wa shule za msingi na wanafunzi 12 ni wa shule za sekondari.

Tunaamini, kujenga shule za bweni kunaondoa mashaka kwa wanafunzi wanaotoka nyumbani kila siku kwenda shuleni kwa kuwa hapa katikati kabla ya kufika shuleni kuna vikwazo vingi na ndipo mimba zinapoanzia.

Wapo wale wa bodaboda wanaowapa lifti lakini pia wapo wanaume wanao’jitolea’ kuwasindikiza huku wakiwapa maneno ya ulaghai ikiwa ni pamoja na kuwahonga fedha ili wafanye nao mapenzi, tena yasiyokuwa salama.

Ni ukweli ulio wazi kwamba kama mtoto anapewa mimba, maana yake alifanya ngono zembe, hivyo mbali na mimba anaweza kuambikizwa pia magonjwa yakiwemo ya kisonono, kaswende na hata Ukimwi.

Jingine ambalo limekuwa ni tatizo ni wazazi kutumia watoto wao hasa wa kike kujiongezea kipato. Hili ni tatizo la umasikini.

Pia wazazi wamekuwa hawatoi ushirikiano kwa Polisi kutoa ushihidi mahakamani badala yake wakitaka masuala haya yamalizwe kimila.

Mkurugenzi wa shirika lisilokuwa la serikali la Kivulini, Yasin Ally anasema wazazi wamekuwa sababu kubwa ya watoto kupata mimba kutokana na watoto kutumiwa kama vitega uchumi vya familia hivyo wanastahili wapewe elimu ya kutosha.

Naye Ofisa wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Kasulu, Maimuna Abdul anasema tatizo la mimba kwa watoto limekuwa kero kubwa katika wilaya yao na kuongeza kwamba kwa mwaka huu mpaka sasa, wamepokea kesi 19 wakati mwaka jana walipokea kesi 22 na mwaka 2017 walipokea kesi 22.

Tunaamini, kama wazazi wakipewa elimu wakashiriki kikamilifu kutoa ushirikiano Polisi na mabweni yakajengwa kwa kila shule ya wasichana, tatizo la mimba za utotoni laweza kupungua.

WAUMINI wa dini ya Kiislamu nchini jana na leo wameungana ...

foto
Mwandishi: Tahariri

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi