loader
Picha

Tushikamane dhidi ya dengue

HAKUNA ubishi kwamba ugonjwa wa dengue na ebola ni tishio kwa maisha na uhai wa Watanzania kama ilivyo katika nchi nyingine barani Afrika na dunia kwa ujumla wake.

Kutokana na ukweli huo, tunapenda kuungana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kwa kauli yake ya kuwataka waganga wakuu wa mikoa kuchukua hatua za makusudi kuzuia mbu waambukizao homa ya dengue na kusisitiza mikoa iliyo mpakani kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa ebola.

Waziri Mwalimu aliagiza hayo jana Dodoma wakati akifungua mkutano wa kikao kazi cha viongozi mbalimbali wa hospitali za rufaa za mikoa.

Katika maagizo yake aliwataka waganga wakuu ambao maeneo yao yamekumbwa na ugonjwa wa homa ya dengue na hata mikoa ambayo haijakumbwa na tatizo hilo kuhakikisha wanaangamiza mazalia kwa kutumia dawa ya viuadudu.

Kama alivyosisitiza Waziri Mwalimu, katika hili waganga wakuu wa mkoa kwa kushirikiana na wakurugenzi wa wilaya na halmashauri wahakikishe kushirikiana kiuhalisia katika kukabiliana na mbu hao hatari kwa kuhakikisha kwamba madimbwi yote katika maeneo yao yananyunyiziwa viuadudu kudhibiti hali ya kusambaa kwa ugonjwa huo.

Katika shughuli hiyo pia viongozi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji pamoja na wananchi kwa ujumla wao washikamane katika hili hata kwa kutoa taarifa za maeneo yanayoonekana wazi yana madimbwi mengi ya maji yanayotakiwa kunyunyiziwa dawa hizo.

Hapa tunapenda kukumbushana tu kwamba hiyo siyo mara ya kwanza kwa Watanzania kushughulikia masuala mbalimbali yanatishia afya zetu, kwani hapo nyuma zilikuwepo kampeni mbalimbali za kukabiliana na magonjwa yakiwemo ya mlipuko kwa kushikamana kiasi ya kuyashinda magonjwa hayo yakiwemo ya kipindupindu na hata Ukimwi.

Sisi tunaamini kwamba iwapo vita dhidi ya ugonjwa wa dengue unaotukabili sasa katika mikoa yetu mbalimbali, ikiwamo ya Dar es Salaam, Tanga, Singida na mingine ambayo uwezekano wa kukabiliwa na ugonjwa huo pia upo kwa kiaisi kikubwa, sote tuwe katika njia moja ya kuongeza mshikamano na ushirikiano kukabiliana nao vilivyo.

Katika hili hatuna budi kushirikiana kwa karibu zaidi na askari wetu kwa maana ya wataalamu wetu wa afya kwa kuzingatia kwa vitendo ushauri wao wa kitaalamu katika kupambana na adui dengue.

Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu na kwamba katika vita hivi ni watu wote tuwe pamoja kwa hali na mali kuukabili ugonjwa huo wa dengue.

Kujihakikishia kwamba vita hivi siyo vya mchezo kwa usalama na maisha yetu, tuhakikishe pia kwamba wenzetu watakaojifanya kampeni hiyo haiwahusu tusiache kuwafikisha kwa viongozi wetu wa kijamii na serikali ili nao wakumbushwe kushiriki vita hiyo bila kufanya ajizi.

Hili linawezekana kwa kuimarisha mshikamano dhidi ya vita hivi.

WAUMINI wa dini ya Kiislamu nchini jana na leo wameungana ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi