loader
Picha

Cuba inavyopambana na hujuma za majirani zake

TANZANIA na Cuba zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu. Nakumbuka visiwani Zanzibar tangu wakati wa ukoloni vijana walipata mafunzo yao nchini Cuba na kisha wakarudi visiwani kushiriki katika kuendeleza mapinduzi.

Cuba pia ilisaidia nchi yetu katika sekta ya elimu na afya. Kuna shule ya sekondari ilipewa jina la mwasisi na kiongozi wa mapinduzi ya Cuba, Fidel Castro. Mwanangu, Yenan tulimpeleka hospitali ya Muhimbili akatibiwa na daktari bingwa kutoka Cuba.

Nikashuhudia pia madaktari kutoka Cuba wakifanya kazi hospitali ya Aga Khan. Nikasoma habari za majeshi ya Cuba yakiwasaidia wanaukombozi wa Angola (MPLA) kuikomboa nchi yao kutoka makucha ya makaburu wa Afrika Kusini. Nikasoma vitabu kuhusu mapinduzi ya Cuba chini ya uongozi wa Fidel Castro na mwandani wake, Ernesto Che Guevara.

Nikamshuhudia Castro akipokewa na mwenyeji wake hapa nchini Mwalimu Nyerere. Jina la Cuba lilikuwa likivuma mno, siyo tu hapa nchini kwetu bali katika bara zima la Afrika. Ndipo hivi majuzi nilipopata fursa ya kutembelea Cuba nikakumbuka niliyokuwa nikisikia na kusoma kuhusu nchi hiyo iliyo umbali wa kilometa 90 tu kutoka Marekani. Nikawaza kuhusu vikwazo vya kiuchumi na kijeshi vilivyowekwa na Marekani kwa muda wa takribani miaka 60.

Ni nchi ambayo imeshambuliwa kijeshi na Marekani. Majaribio kadha yalifanywa na shirika la ujasusi la CIA la kumuua Castro lakini ikashindikana. Naungama kuwa nilipigwa na mshangao nilipowasili, kwa vile nilichokiona siyo nilichokitegemea. Cha kwanza kilichonishangaza ni idadi ya wageni wanaotembelea Cuba kutoka nchi mbali mbali duniani.

Kote nilipopita nilikuta mashamba yaliyolimwa pamoja na viwanda. Baadhi ya viwanda niliambiwa ni vya tangu enzi Umoja wa Sovieti (USSR) ukiwa imara. Majengo pia yalijengwa enzi zile, ingawa wenyeji wanaonekana wakiendeleza makazi yao. Ni dhahiri kuwa Cuba inategemea sana utalii na jambo hili linaonekana wazi kote nchini. Hoteli za kitalii zimezagaa kote nchini humo na wananchi wamo mbioni kujitafutia maisha.

Kwa nchi iliyoshambuliwa kijeshi na ikawekewa vikwazo vya kila aina na Marekani, ni jambo la kujiuliza inakuwaje watalii wanazidi kuongezeka na biashara inazidi kunawiri. Wageni wanaoingia wanatoka nchi tofauti na idadi yao inazidi kuongezeka. Mwaka 2003 watalii karibu milioni 2 walitembelea Cuba na kuingiza pato la dola bilioni 2.1. Wengi wao walitoka Canada na Ulaya.

Mwaka 2011 idadi ya watalii ikafikia 2,688,000. Na mwaka 2017 idadi ya watalii ikafikia milioni nne na mwaka 2018 idadi yao imefikia milioni tano. Mnamo Septemba 2017 Cuba ilipatwa na janga kubwa kutokana na kimbunga kiitwacho Irma.

Maeneo kama Camagüey yaliathirika vibaya. Jumla ya nyumba 158,554 ziliezuliwa na 14,657 zikateketea. Takriban watu milioni 1.9 walikosa makazi. Zahanati 980 na shule 2,264 nazo ziliathirika Watu 10 walipoteza maisha yao na jumla ya hasara ilifikia dola bilioni 13.2. Maeneo ya kitalii kama Cayo Coco, Cayo Guillermo, Cayo Santa María na Caibarién nayo yalipigwa na kimbunga.

Kimbunga kama hiki hakijawahi kuonekana Cuba. Pamoja na yote hayo nchi ilijikusanya na maisha yakaendelea. Baada ya muda idadi ya watalii ikaendelea kuongezeka. Idadi kubwa ya watalii wamekuwa wakitoka Canada na Marekani lakini sasa Trump amewafungia mlango Wamarekani. Hata hivyo, Cuba inafanya bidii kuwavutia watalii zaidi kutoka nchi kama Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Hispania, China, Vietnam na Afrika Kusini.

Rais wa Cuba, Miguel Díaz-Canel Bermúdez amesisitiza umuhimu wa utalii katika uchumi wa nchi, akisema serikali inategemea kuwekeza katika upanuzi wa hoteli za kitalii na miundombinu.

Mwaka huu mapato ya utalii katika uchumi wa Cuba yanategemea kufikia dola bilioni tatu. Serikali imefanya kila juhudi ili kurahisisha usafiri wa watalii. Jambo la kwanza nimegundua kuwa viza hutolewa bila usumbufu. Wasafiri hupewa fomu ya kujaza wakiwa katika ndege. Unapofika uwanja wa ndege fomu hiyo (tourist card) inagongwa mhuri na unarudishiwa. Wakati wa kuondoka nchini unairejesha fomu.

Jambo la pili ni kuhusu matumizi ya fedha. Kila mtalii anapofika hotelini anavishwa utepe wa plastiki mkononi. Utepe huo anabaki nao mpaka siku ya kuondoka. Kila aendako anatambulika kuwa ni mgeni, kwa hiyo anatakiwa atumie sarafu maalumu kwa ajili ya wageni. Hii ni njia ya kudhibiti fedha za kigeni zinazoingia. Kuna sarafu za aina mbili. Ya kwanza ni kwa wenyeji nayo huitwa CUP.

Ya pili ni CUC ambayo ni kwa wageni. Kila mgeni anabadili fedha yake ya nje na kupata CUC ambayo thamani yake ni sawa na dola. CUC unaipata benki au hotelini ambako kuna matawi ya benki. Ni CUC hii ndiyo unatumia kila utakapofanya matumizi kama vile kukodi teksi au kula mgahawani. Mfumo huu wa sarafu unazuia mtindo wa nchi kadha ambako fedha za kigeni hubadilishwa barabarani na vichochoroni na serikali hukosa mapato ya kigeni.

Cuba inazihitaji sana fedha hizi za kigeni. Na ndio maana utalii ni sekta kubwa na muhimu. Kwa muda mrefu tangu mapinduzi ya 1959, Cuba ilikuwa na uhusiano wa karibu na USSR. Cuba iliuzia sukari na kununua mafuta. Baada ya mwaka 1990 shirikisho la USSR likasambaratika na Cuba ikaathirika kiuchumi. Halikadhalika, Venezuela nayo ilikuwa ikishirikiana kibiashara na Cuba. Kila siku mapipa 110,000 ya mafuta yakitoka Venezuela. Na Cuba ilituma maelfu ya madaktari kuisaidia Venezuela.

Leo nchi hiyo nayo imewekewa vikwazo. Uchumi wa Cuba unategemea utalii pamoja na kilimo cha miwa na tumbaku. Pia kuna mafuta yaliyogunduliwa karibu na bahari ya Cuba. Pia kuna uchimbaji wa madini kama nikeli na kobalti. Mwaka 2005 iliripotiwa kuwa ghuba ya kaskazini ya Cuba ilikuwa na uwezo wa kuzalisha takribani mapipa bilioni 4.6 hadi 9.3 ya mafuta kwa mwaka.

Nchi hii yenye wakazi takribani milioni 11 inabidi iagize kutoka nje theluthi mbili ya mahitaji yake kwa gharama ya dola zaidi ya bilioni mbili. Ili kuhakikisha kuwa mahitaji haya yanawafikia wananchi kila mmoja hupewa kitambulisho cha kumwezesha kununua bidhaa kwa bei nafuu kutoka maduka maalum (libreta). Leo Cuba ina uhusiano wa kibiashara na nchi kama Canada, China, Uholanzi, Hispania, Ubelgiji, Brazil, Mexico na Urusi.

Bidhaa zinazosafirishwa ni sukari, nikeli, tumbaku, samaki, matunda, madawa na kahawa. Bidhaa zinazoagizwa ni vyakula, mafuta, nguo, pembejeo na mitambo Wananchi na viongozi wa Cuba wanapaswa kupongezwa kwa jinsi walivyoweza kuhimili mashambulizi ya Marekani. Kwa muda wa miaka 60 wameshambuliwa kijeshi na kiuchumi lakini hawakusalimu amri. Rais Trump akatangaza vikwazo zaidi tarehe 4 Juni mwaka huu alipowazuia raia wa Marekani wasitembelee Cuba.

Mwaka 2018 jumla ya Wamarekani 650,000 walitembelea Cuba na Januari hadi Aprili mwaka huu walifikia 250,000. Inakisiwa mpaka mwisho wa 2019 idadi yao ingefikia 800,000 lakini ghafla rais wao akawaambia hamruhusiwi tena kwenda huko. Inawashangaza wengi kuona nchi inayojigamba kuwa na demokrasia kuwazuia raia wake wasitembee watakako.

Hakuna nchi nyingine iliyotangaza marufuku ya aina hii. Trump pia ametangaza utekelezaji wa sheria ya Helms-Burton iliyopitishwa kwaka 1996 nchini Marekani. Sheria hii kandamizi inaruhusu Marekani kuzishitaki kampuni za kigeni zinazofanya biashara na Cuba. Hii inatokana na mali za dikteta Batista na wenzake zilizotaifishwa baada ya mapinduzi ya Cuba miaka 60 iliyopita.

Lengo ni kuzizuia kampuni za Canada na Ulaya zilizowekeza katika sekta za utalii, madini na kilimo nchini Cuba. Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Cuba, Alberto Navarro anasema Marekani kuzishitaki kampuni za kigeni ni uhalaifu wa sheria ya kimataifa. Anaongeza kwamba lengo lake ni kuendelea kuikandamiza Cuba na kuwadhalilisha watu wake. Kisingizio cha Trump ni kuwa eti Cuba imetuma majeshi 20,000 hadi 25,000 huko Venezuela, jambo ambalo Cuba imekuwa ikikanusha.

Waziri wa mambo ya nje wa Cuba, Bruno Rodríguez Parrilla anasema hakuna mwanajeshi wa Cuba nchini Venezuela, isipokuwa tu madaktari. Cuba imekuwa ikiwatuma madaktari na wauguzi huko Venezuela ambayo nayo inatuma mafuta Cuba.

Na si Venezuela tu bali Cuba ina madaktari wake katika nchi zaidi ya 67 duniani. Rais wa Cuba amejibu kwa kusema, “Cuba haitatishika wala kupoteza lengo kutokana na vitisho vipya vya Marekani. Tutaendelea kuchapa kazi na kujilinda kama tulivyokuwa tukifanya siku zote. Wameshindwa siku zote na wataendelea kushindwa.”

KIWANGO cha utabiri wa hali ya hewa nchini kinazidi kukua ...

foto
Mwandishi: Nizar K Visram, Ottawa (Canada)

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi