loader
Picha

Hongera Mbarawa kutatua kero ya maji

JUZI kulikuwa na tukio la utiaji saini wa miradi sita ya maji jijini Dar es Salaam, kati ya Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa) na wakandarasi, itakayogharimu Sh bilioni 114.

Mgeni rasmi katika tukio hilo alikuwa Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa akiwa na Naibu Waziri, Jumaa Aweso.

Wengine walioshuhudia tukio hilo ni Mwenyekiti wa Bodi wa Dawasa, Jenerali Davis Mwamunyange na wajumbe wa bodi hiyo.

Katika tukio hilo, Waziri Mbarawa alizungumza mambo mengi kuhusu miradi ya maji nchini na matatizo makubwa yaliyopo, yanayosababisha kero ya maji iendelee kuwepo katika maeneo mengi.

Kwa mujibu wa Mbarawa, tatizo kubwa ni mtandao wa ufisadi wenye mizizi mirefu kuanzia ngazi za wilaya, halmashauri, mkoa hadi wizarani, jambo linalofanya miradi ya maji nchini kutekelezwa kwa gharama kubwa.

Kwamba mtandao huo wa kifisadi unahusisha wahandisi wa maji wa wilaya, ofisi za wakurugenzi watendaji (ma-DED), mkoa, wizarani na hadi ofisi ya waziri mwenyewe.

Mbarawa anafafanua kwamba ufisadi huo unafanyika, kwa kuweka makadirio ya juu ya miradi ya maji, ikilinganishwa na gharama halisi inayotakiwa, hivyo kumfanya kila mtendaji katika ofisi husika kuchukua ‘kamisheni’ (hongo) yake na matokeo yake miradi hiyo kutekelezwa kwa bei kubwa.

Kwa mfano, katika mradi wa maji wa Kirando wilayani Nkasi mkoani Rukwa, zabui ilipotangazwa mwaka 2014 mkandarasi aliyeshinda, alitakiwa kuutekeleza mradi huo kwa gharama ya Sh bilioni 7.6. Serikali ilipotangaza tena zabuni ya mradi huo, mkandarasi alisema angeutekeleza kwa gharama ya Sh bilioni 4.56, lakini serikali haikusaini mkataba huo.

Hivi sasa serikali inatekeleza mradi huo kwa gharama ya Sh bilioni 3.9 tu. Mradi mwingine ni ule wa kusambaza maji Sumbawanga Vijijini pia mkoani Rukwa kwenye vijiji 10. Zabuni ya mradi huo ilipotangazwa, mkandarasi alitakiwa kuutekeleza kwa gharama ya Sh bilioni 3.9 hadi Sh bilioni 6.2 kwa kujenga matangi manane.

Lakini, serikali ilipoupitia upya, mradi huo ilibaini kuwa matangi ya maji yanayohitajika ni matano tu na sasa mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya Sh bilioni 2.5.

Mradi mwingine ni wa Makete mkoani Njombe, ambao ulitakiwa kutekelezwa kwa gharama ya Sh bilioni 5.69, lakini kwa sasa unatekelezwa kwa Sh bilioni 2.5.

Mwingine ni mradi wa maji wa Tandahimba mkoani Mtwara, ambao ulitakiwa kutekelezwa kwa gharama ya Sh bilioni 3, lakini baada ya kupitiwa upya unatekelezwa kwa Sh bilioni 1.6 tu!.

Kutokana na maelezo hayo, ni wazi kuwa Mbarawa ametufumbua macho, kwa kuanika kila kitu kinachokwamisha jitihada za serikali, kutatua kero ya maji, ikiwemo mtandao mkubwa wa ufisadi ulivyo kutoka wilayani hadi makao makuu ya wizara.

Kinachotakiwa sasa ni viongozi wa serikali katika ngazi za wilaya, mikoa na wizara pamoja na vyombo vya dola, kuwasaidia Profesa Mbarawa, Aweso na wazalendo wengine katika wizara hiyo, kutatua kero ya maji nchini.

Mbarawa anastahili pongezi; na wote kwa pamoja tumuunge mkono na kumsaidia kwa hali na mali.

WAUMINI wa dini ya Kiislamu nchini jana na leo wameungana ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi