loader
Picha

Mifuko ya plastiki imepita zimebaki changamoto mifuko mbadala

KUANZIA Juni Mosi mwaka huu, ni kosa la jinai kutengeneza, kuagiza, kusambaza na kutumia mifuko ya plastiki nchini Tanzania, na wote watakaokaidi marufuku hiyo watakutana na mkono wa sheria.

Uamuzi huu unatokana na kelele za muda mrefu za wadau wa afya na mazingira wakilalamika mifuko hiyo kuchangia uharibifu wa sura ya nchi yetu na kusababisha majanga mbalimbali.

Marufuku hiyo inahusu sehemu yote ya Tanzania Bara, lakini ni hatua nyingine ya kuungana na upande wa pili wa Muungano, kwa maana ya Zanzibar ambako kwa miaka kadhaa sheria ya kupiga marufuku mifuko hiyo ilishafanya kazi. Kwa zaidi ya miaka kumi, Tanzania Bara ilikuwa katika harakati za kupiga marufuku mifuko ya plastiki, lakini kukawa na vikwazo mbalimbali kabla ya kufikiwa kwa uamuzi huo mwaka huu.

Uamuzi huu umepongezwa na wadau wengi wakiwemo wananchi wa kawaida, lakini pia ni uamuzi unaoleta sura ya pamoja ya Afrika Mashariki kwa sababu baadhi ya nchi zikiwemo Kenya na Rwanda tayari zilishapitisha sheria hiyo, huku Uganda na Burundi nazo zikiwa kweye mchakato huo. Mifuko ya plastiki imelalamikiwa kutokana na uchafuzi na uharibifu wa mazingira duniani, na harakati za kukomesha matumizi yake zinalenga kulinda mazingira.

Kwa kupitia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (Environmental Management Act), Serikali ya Tanzania imetunga Kanuni za Mwaka 2019 za kupiga marufuku matumizi ya mifuko hiyo. Kifungu cha Nane cha Kanuni hizo kinaorodhesha makosa matano ambayo ni; kuzalisha na kuagiza mifuko ya plastiki, kusafirisha nje ya nchi mifuko ya plastiki, kuhifadhi na kusambaza mifuko ya plastiki, kuuza mifuko ya plastiki na mwisho kumiliki na kutumia mifuko ya plastiki.

Kwa kosa la kwanza la uzalishaji na uagizaji adhabu yake ni mosi, faini isiyopungua Sh milioni 5 na isiyozidi Sh milioni 20, pili kifungo kisichozidi miaka miwili jela, adhabu ya tatu ni mjumuiko wa adhabu zote mbili za awali faini na kifungo. Adhabu za kosa la pili ambalo ni kusafirisha mifuko nje ya Tanzania ni sawa na za kosa la kwanza. Kwa kosa la tatu la kuhifadhi na kusambaza mifuko, adhabu zake ni mosi, faini isiyopungua Sh milioni 5 na isiyozidi Sh milioni 52, pili kifungo kisichozidi miaka miwili na tatu, ni faini na kifungo kwa pamoja.

Ukipatikana na hatia ya kuuza mifuko ya plastiki adhabu ambazo utakumbana nazo ni mosi, faini isiyopungua 100,000 na isiyozidi Sh 500,000. Adhabu nyingine kwa kosa hili ni kifungo kisichozidi miezi mitatu jela na tatu, yawezekana ukahukumiwa adhabu zote mbili za awali yaani kifungo na faini. Lakini pia ukiendelea kutumia na kumiliki mifuko ya plastiki, basi jiandae kulipa faini isiyopungua Sh 30,000 na isiyozidi Sh 200,000 , kifungo kisichozidi siku saba ama faini na kifungo vyote kwa pamoja.

Katika kuhakikisha hakuna anayeonewa ama kuathirika kibiashara na katazo hilo, marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki ilitangazwa tangu Aprili 10 ili kuwapa watu wakiwamo wafanyabiashara muda wa kujiandaa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Januari Makamba akatoa mwongozo kuhusu kinachotakiwa kufanyika kwa wafanyabiashara ambao watakuwa wangali na shehena kubwa ya mifuko hiyo tarehe ya marufuku itakapowadia. “Baadaye utafanyika utaratibu wa kurejerezwa (recycle) na kutengenezwa bidhaa nyingine kama sahani, viti na kadhalika,” akasema.

Akaongeza: “Kwa mfano, Sudan hawajakataza mifuko, tutawasaidia wale waliopata soko wasipate hasara, lakini kwa kibali maalumu na itasindikizwa hadi mpakani kwa gharama za msafirishaji.” Lakini serikali pia ikatoa tangazo la katazo ya mifuko kwa wageni wanaotarajia kuingia nchini baada ya Juni Mosi. “Wageni wanaoingia (Tanzania) wanashauriwa kutobeba vifungashio vya plastiki vya aina yoyote. Katika maeneo ya mipaka ya kuingilia nchini kutakuwa na dawati maalumu kwa ajili ya kutupa mifuko hiyo,” ilisema taarifa ya serikali.

Serikali ikasema lengo lao siyo kuwafanya wasafiri kutofurahia safari zao, bali kushiriki katika kutunza mazingira. Wakati anatoa agizo hilo, Waziri Makamba anasema kuna viwanda zaidi ya 70 vilivyojitokeza kutengeneza mifuko mbadala. Kati ya hivyo, sita ni vikubwa na 30 vya kati. Na tumeona mara tu baada ya Juni Mosi, mifuko mingi mbadala imeingia mitaani kubeba nafasi ya mifuko ya plastiki ambayo imeondoka kwa mujibu wa sheria. Hata hivyo ikiwa ni mwezi mmoja tu tangu kuanza kutumika kwa mifuko mbadala, tayari kuna changamoto kubwa zimeanza kujitokeza.

Baadhi ya wafanyabiashara wazalishaji wa mifuko huyo wanalalamika kwamba kumekuwa na usumbufu mpya kutoka kwa maofisa wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wanaodai mifuko inayozalishwa haina viwango. Baadhi yao wameshaandika barua za malalamiko kwa Mkurugenzi Mkuu wa TBS wakilalamikia hatua ya maofisa wa Shirika hilo kuwazua kuzalisha mifuko ya chini ya gramu 50 zinazodaiwa kukosa viwango, na badala yake, TBS wanataka wafanyabiashara hao kuzalisha mifuko yenye uzito wa kuanzia gramu 70.

Hata hivyo, wafanyabiashara hao wanasema kwamba sheria ya kimataifa (ISO) ndiyo inayoongoza uzalishaji wa mifuko na kwamba hata nchi jirani Kenya na Rwanda ambako wataalam wetu walikwenda kujifunza, zinazalisha mifuko ya uzani wa chini ya gramu 50. Mmoja wa wafanyabiashara Omar Ameir anasema ukinzani huo wa sheria za Tanzania na zile za kimataifa ungewekwa wazi kwenye vikao vya awali vya maandalizi. “Katika vikao vyote vya maandalizi ya uzalishaji wa mifuko TBS walikuwepo, NEMC walikuwepo na taasisi nyingine.

Na hakukuwa na mwongozo wowote kwamba lazima mifuko tutakayozalisha iwe na uzani wa kuanzia gramu 70. Kwanini TBS wasubiri watu wameanza uzalishaji kisha ndiyo waanze kuwapiga marufuku?” amelalamika. Mfanyabiashara huyo amesema maagizo mapya ya TBS kwa wafanyabiashara yanarudisha nyuma sera ya nchi ya ongezeko la viwanda, lakini yanaifanya Tanzania kuwa kisiwa katika uzalishaji wa mifuko.

“Wenzetu Kenya na Rwanda wanazalisha mifuko kama hii, lakini pia kuna watu wanaingiza mifuko kutoka China, ambayo iko chini ya viwango zaidi na inauzwa hapa nchini, TBS wapo. Hii inaleta picha gani?” “Kwanini tusiamini kwamba kuna ukinzani mkubwa katika suala hilo ambalo tayari lilishapata mwafaka kupitia vikao baina ya wizara husika na wazalishaji wa mifuko mbadala?”amelalamika mfanyabiashara huyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Habari dhidi ya Umasikini (MeCAP), Mdoe Kiligo anasema mkanganyiko huo unaweza kurudisha nyuma mwelekeo wa taifa kuelekea kwenye uchumi wa viwanda. “Kama mifuko inayolalamikiwa na TBS inatumika kimataifa, ikiwa ni pamoja na nchi jirani zikiwemo Kenya na Rwanda, maana yake sisi Watanzania tunataka kuingia kwenye soko la ushindani tukiwa peke yetu? Lakini pia kama Wachina wanaingiza mifuko kama ile inayozalishwa na viwanda vya ndani na wanaruhusiwa kuuza, tafsiri yake sio nzuri kwa nchi,” anasema.

Anaongeza kuwa, kituo chake kilikuwa na mchango mkubwa kwenye kufuatilia na kuandaa ripoti katika suala la uharibifu wa mazingira unaotokana na mifuko ya plastiki, na walitegemea kuona viwanda vinavyozalisha mifuko mbadala vikilindwa badala ya kuvikatishwa tamaa. Hivyo, kinachotaka kutokea sasa kwa baadhi ya mamlaka ni kuanza kuweka ukinzani katika mifuko mbadala iliyoanza kutumika baada ya kupigwa marufuku mifuko ya plastiki ni kama kurudisha nyuma jitihada zilizozaa matunda za kupambana na uharibifu wa mazingira.

Siyo tu kurudisha nyuma jitihada hizo kwa upande wa mazingira, bali pia kunaweza kukakinzana na kasi ya ukuaji wa ajira kupitia viwanda hivyo vya kutengeneza mifuko mbadala, vilivyoanza kuajiri watu wengi na kuunga mkono kaulimbiu serikali yetu iliyojizatiti kuhakikisha nchi inakuwa na uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda.

Hivyo, ni vyema sasa kwa mamlaka zilizofanikiwa kuondoa mifuko ya plastiki; ziketi na wafanyabiashara na wazalishaji wa mifuko mbadala kisha kuja na majibu ya haraka katika changamoto hii ya aina gani ya mifuko inayohitajika ambayo mingi tayari imeshaingia sokoni kama hatua ya kutekeleza katazo la serikali iliyolenga kunusuru mazingira. Mwandishi wa makala haya ni msomaji na mchangiaji katika gazeti hili akitokea Kituo cha Habari dhidi ya Umasikini (MeCAP).

KIWANGO cha utabiri wa hali ya hewa nchini kinazidi kukua ...

foto
Mwandishi: Mawazo Lusonzo

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi