loader
Picha

Utafiti unavyoongeza rasilimali samaki nchini Tanzania

UTAFITI wa mradi wa ufugaji wa viumbe baharini ulianza miaka 22 iliyopita yaani mwaka 1996. Kipindi hicho watafiti kutoka Taasisi ya Sayansi za Bahari ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), walifuatwa na Chuo cha Mafunzo Zanzibar kuona kama maeneo ya Bumbwini Makoba walikokuwa wakikausha chumvi yanaweza kutumika kufuga kamba.

Baada ya kushauriana, wakaamua waanze kwa kufuga samaki ambao ni rahisi zaidi. Mhadhiri Mwandamizi na Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Bahari na Uvumbuzi katika Taasisi ya Sayansi za Bahari, Dk Aviti John Mmochi, anasema walianza kufuga samaki aina ya perege na mwatiko ambaye maeneo mengine anajulikana kama mkuyi au mkuyu.

Anasema wamemfanyia utafiti samaki aina ya mwatiko kwa miaka saba katika mashamba ya Chuo cha Mafunzo, Makoba na baadaye, kusambaza ufugaji huo sehemu mbalimbali za Tanzania. Taarifa ya Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) ya mwaka 2013 inaonesha kuwa, Tanzania iliyoanza na tani mbili mwaka 2004 ilifikisha tani 231 mwaka 2012.

“Japo siyo kiasi kikubwa sana, utafiti huo umechangia kuanzisha ufugaji huo unaoweza kuendelezwa la kupunguza umaskini kwa watu wa Pwani na pia kupunguza msongamano wa wavuvi usio endelevu.”

“Kiasi cha samaki duniani wa kuvua ni tani milioni 80 lakini wamebaki katika takwimu hiyo kwa takribani miaka 30 bila kuongezeka japo taaluma na nguvu za kuvua zimeongezeka mpaka tuna uwezo wa kutumia vyombo kuita samaki kwa kutumia fish finder watufuate,” anasema.

Anasema njia mbadala ilibidi iwe kufuga sa-maki ambapo ufugaji ulikuwa mdogo sana ukapanda na hivi sasa kiasi cha samaki wanaofugwa kinakaribia kufikia samaki wa kuvua. “Tanzania tuna samaki wa kuvua tani 400,000 kiasi kinachotuweka kwenye 10 bora katika kuvua, japo wengi wao wanatokea Ziwa Victoria, huku bahari kuu ikiwa haijaguswa,” anasema.

Anaelezea changamoto za uvuvi kuwa ni pamoja na ukosefu wa vyombo na zana za kuvulia hasa kwa bahari kuu au vina virefu kama vya maziwa ya Tanganyika na Nyasa unaowalazimisha wavuvi kuvua kwenye kina kifupi. Uvuvi huo wa kina kifupi unaharibu mazalia ya samaki na kuvua samaki wachanga ambayo ina maana wanawazuia wasizaliane.

Anasema katika utafiti huo walianza na samaki aina ya mwatiko hivi sasa wanafanya majaribio katika utafiti wa samaki aina ya kolekole pia wapo kwenye mpango wa kuzalisha vifaranga. Aidha, anasema wamepata eneo Pangani wanalofanyia majaribio ya kuzalisha na kufuga samaki aina za perege kwenye maji ya chumvi. “Tumeweza kuzalisha perege ambao ni madume matupu bila kutumia homoni. Kwa kutumia madume ya perege wa Rufiji na Wami ambao ni super male samaki akikutana na wa kike kama sato wa Ziwa Victoria wanaokubaliana kwa asili zao wanazalisha madume matupu,” anasema.

Anaongeza kuwa wanafanya utafiti wa viasili wa perege wote Tanzania ili kujua yupi anafaa kufugwa kwenye maeneo mbalimbali ya nchi ili kukuza uzalishaji na kuepuka kuchanganya mbegu za samaki.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, utafiti huo unadhaniwa kuwa kichocheo cha Serikali ya Zanzibar kuanzisha mradi wa utotoaji wa vifaranga vya mwatiko, majongoo bahari na kaa ambao wote hao walishafanyiwa utafiti kwenye Taasisi ya Sayansi za Bahari na kisha, kupelekwa kwa wananchi waliokuwa wanaokota vifaranga toka baharini.

Anasema anaamini kuwa maendeleo hayo kikiwemo na Kituo cha utotoleshaji wa vifaranga, Kituo cha Ufugaji wa Samaki cha Pangani (UDSM) na mabadiliko ya kisera na kitendaji yanayoendelea kwenye idara zinazohusika na ufugaji wa viumbe kwenye maji vitasababisha maendeleo makubwa na ya kasi katika ufugaji wa baharini.

KIWANGO cha utabiri wa hali ya hewa nchini kinazidi kukua ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi