loader
Picha

Faida urasimishaji ardhi Moro

MPANGO wa urasimishaji ardhi (Land Tenure Support Program - LTSP) unaotekelezwa kwa pamoja kati ya asasi za kiraia zilizo chini ya mwavuli wa Tanzania Land Alliance (TALA) na serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, umewakuna vilivyo wakazi wa Morogoro baada ya kuona faida zake.

Wakati wizara ikiwa imefanya kazi kubwa ya kusaidia vijiji zaidi 100 kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi na kuandaa zaidi ya hati za kimila 250,000, asasi za kiraia chini ya TALA nazo zimeshiriki kuhakikisha wananchi kupitia makundi mbalimbali wanapata elimu ya kunufaika na ardhi bila migogoro.

Wananchi walionufaika ni kutoka katika Wilaya za Ulanga, Malinyi na Kilombero ambao wamepata elimu kuhusu ushiriki wao katika mchakato wa uandaaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi, hatua ambayo imesaidia sana kutatua migogoro ya ardhi. Joseph Kudinga aliyepata mafunzo katika Kijiji cha Miwangani, Wilaya ya Kilombero anasema katika kipindi cha utekelezaji wa mpango huo, yeye na wakazi wenzake wamenufaika na elimu na ujuzi juu ya haki ya ardhi, huduma ya msaada wa kisheria na namna ya kutatua migogoro ya ardhi katika maeneo yao.

Anasema katika mpango huo, wamenufaika pia na elimu ya utunzaji wa mazingira, haki za binadamu na haki za makundi maalumu kama vile wafugaji, wanawake na vjana. Mpango huo unaotekelezwa mkoani Morogoro katika wilaya za Ulanga, Malinyi na Kilombero unasaidiwa na wadau kadhaa ikiwemo serikali za Sweden na Denmark kupitia balozi zao zilizopo Dar es Salaam.

Samora Michael, mkazi wa Wilaya ya Malinyi, anasema elimu juu ya mpango wa matumizi bora ya ardhi na haki za wafugaji itasaidia sana kupunguza migogoro ya ardhi kati yao na wakulima katika wilaya ya Malinyi. Mratibu wa asasi za kiraia ambaye pia Ofisa Maendeleo wa Wilaya ya Kilombero, Ashura Kalufya, anasema kuwa zaidi ya vijana 250 wamepatiwa mafunzo kuhusu haki ya kupata, kutumia na kumiliki ardhi.

Anasema idadi kama hiyo ya wanawake wamepata pia mafunzo hayo yanayolenga kuhakikisha haki zao ikiwemo za mirathi zinatambuliwa na kulindwa. Mwanasheria kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Irene Nambuo, anasema waligundua kuwa maeneo mengi yamegubikwa na migogoro mingi ya ardhi, migogoro ya mipaka, uvamizi wa ardhi na migogoro ya mirathi.

“Kwa jumla tumefikia wananchi zaidi ya 400. Kwanza baada ya kugundua matatizo yaliyopo ilibidi tuanze na suala la kukuza uelewa na pia kutoa huduma ya kisheria katika kata tano kila wilaya,” anasema. Kalufya anaongeza kuwa ili kufanikisha hilo ilibidi watumie mbinu mbalimbali ikiwemo huduma ya kisheria ya kutembelea wananchi moja kwa moja (mobile legal service), hatua iliyowawezesha kumfikia mtu mmoja mmoja mwenye matatizo husika.

Ofisa Miradi wa shirika linaloshughulika na mazingira (LEAT), Stanslaus Nyembea, anasema kuwa mpango huo unatekelezwa kuanzia ngazi ya chini vijijini ili kuleta mabadiliko chanya katika sera kwa ngazi zote kupitia asasi za kiraia zilizo chini ya mwamvuli wa TALA.

“Malengo mengine ya mpango huu ni kuyajengea uwezo mashirika yanayojishughulisha na maliasili ili yawe na sauti ya kuweza kufanya uraghibishi wa dhati kwa wananchi wa vijijini kuhusu haki zao, haki za ardhi na maliasili zinazowazunguka,” anasema. Katika ngazi ya chini, anasema mpango huo unawawezesha wananchi, hususani wanawake, vijana na makundi ya wakulima wadogo na wafugaji kutambua haki zao na namna ya kutatua migogoro miongoni mwao.

Akizungumzia mabadiliko ya sera, Ofisa Miradi Mwandamizi wa Shirika la Hakiardhi, Joseph Chiombola, anasema ushirikishwaji wananchi kwenye sera na uchambuzi wa sheria ni muhimu sana. Anasema sekretarieti ya TALA na Hakiardhi waliandaa semina kuhusu mchakato wa kubadili sera ya ardhi na matokeo yake kwa wakulima wadogo na kwamba semina hiyo ilihusu asasi za kiraia kujua mchakato wa mapitio ya sera ya ardhi, kutambua majukumu yao katika mapitio ya sera hiyo na kuwajengea uwezo.

Naye Ngorisa Valentine kutoka Mtandao wa Wakulima Wadogo (MVIWATA) anasema wakulima wadogo wamenufaika na mpango huu kwa kupata mafunzo juu ya kilimo endelevu, haki za wakulima wadogo, hati za kimila na simamizi wa masuala ya ardhi. Anasema jumla ya watu 443 kutoka katika kamati za vijiji, mabaraza ya vijiji na mipango ya matumizi bora ya ardhi wamenufaika na mafunzo hayo. “Mafunzo haya yanalenga kuwapa uelewa na ujuzi katika usimamizi wa masuala ya ardhi ili waweze kutekeleza shughuli na majukumu yao vilivyo.

MVIWATA na washirika wao waliendesha mafunzo haya katika vijiji tisa katika wilaya tatu,” anasema. Anavitaja vijiji hivyo kuwa ni pamoja na kijiji cha Idete B, Idete, Kalenga, Sofi Majiji, Misegese, Madibira, Chilombola, Igumbilo na Mzelezi. Naye Emmanuel Saringe kutoka Shirika la Pingos Forum anasema TALA ilibaini kuwa wanavijiji wengi hawakuwa na elimu juu ya masuala ya ardhi ikiwemo mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji vyao, hali iliyosababisha kuwepo kwa migogoro mingi ya ardhi.

Anasema mara nyingi jamii ya wafugaji haikushirikishwa kikamilifu katika mipango ya matumizi ya ardhi, hali iliyosababisha vijjiji vingi kutenga maeneo ya kilimo, makazi ya watu na shughuli nyingine huku eneo la malisho kwa ajili ya wafugaji likisahaulika. “Kwa hiyo elimu na ujuzi tulioupata kupitia mpango huu wa TLSP utatusaidia wanavijiji na viongozi mbalimbali kuhakikisha kila mtu na kila jamii inapata fursa ya kutumia ardhi kwa usawa na hivyo kujiletea maendeleo katika maeneo yao,” anasema Rehema Libenanga, mkazi wa Ulanga.

KIWANGO cha utabiri wa hali ya hewa nchini kinazidi kukua ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi