loader
Picha

Amunike, TFF wamalizana

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeachana na kocha Emmanuel Amunike baada ya kufanya vibaya kwenye michuano ya Kombe la Mataifa Afrika, Afcon 2019. Michuano hiyo bado inaendelea Misri ambapo ipo katika hatua ya mtoano.

Tanzania ilishiriki kwa mara ya kwanza baada ya miaka 39 na kupoteza mechi zote za kundi C, dhidi ya Senegal, Algeria na Kenya. Taarifa ya TFF kwa vyombo vya habari jana, ilisema wamefikia makubaliano ya pamoja na kocha huyo ambaye mkataba wake ulibakiza miezi mitatu kumalizika.

Taarifa ya TFF ilisema Shirikisho hilo litatangaza kocha wa muda atakayekiongoza kikosi kitakachoshiriki mechi za kufuzu fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan) zinazotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu. “Makocha wa muda watatangazwa baada ya kikao cha dharura cha kamati ya utendaji kitakachokutana Julai 11 (keshokutwa),” ilisomeka taarifa hiyo.

Akiiongoza Stars, Amunike ameshinda mechi mbili kati ya 10, sare mbili na sita kapoteza. Katika hatua nyingine, kocha Sebastien Desabre amebwaga manyanga kama kocha wa Uganda baada ya kufanya vibaya kwenye michuano ya kombe la mataifa Afrika, Afcon inayoendelea Misri.

Shirikisho la soka la Uganda, FUFA, lilitangaza juzi kwamba wamefikia makubaliano ya kocha huyo kuachia ngazi. Uganda ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Senegal mjini Cairo, Ijumaa iliyopita katika mechi ya hatua ya 16, ikiwa ni kwa mara ya kwanza kuingia hatua hiyo tangu mwaka 1978.

Fufa ilisema itamthibitisha kocha mpya siku chache zijazo baada ya Desabre kuondoka huku akiwa amebakiza miezi mitano kwenye mkataba wake. “FUFA inashukuru kwa mchango wa Desabre kwenye maendeleo ya Uganda Cranes, ikiwemo pamoja na kufuzu fainali za Afcon na kucheza hatua ya mtoano za Afcon 2019,” ilisomeka taarifa ya Fufa. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 42, Desabre amekuwa kocha wa Uganda tangu aliposaini mkataba wa miaka miwili Desemba mwaka 2017.

Kabla Cranes haijafungwa na Senegal Ijumaa, wachezaji waligomea mazoezi wakishinikiza Fufa kuwalipa madeni yao ya posho. Fufa ilitangaza kuwa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni jana alitarajiwa kuwakaribisha wachezaji wa Cranes Ikulu kuwafanyia hafla maalumu.

RAIS wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Anthony ...

foto
Mwandishi: Tuzo Mapunda

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi