loader
Picha

‘Changamkieni fursa za usafiri, uboreshaji bandari Ziwa Nyasa’

WAFANYABIASHARA wa ndani na nje wamehimizwa kuchangamkia huduma za bandari za Ziwa Nyasa zinazoboreshwa ili kuokoa muda na fedha pale wanaposafi risha bidhaa zao kwenda katika maeneo mbalimbali yanayopakana na ziwa hilo la tatu kwa ukubwa nchini.

Halikadhalika, katika kuelekea kukamilika kwa ujenzi wa meli ya kisasa ya abiria na mizigo ya Mv Mbeya II, wananchi pia wametakiwa kukaa mkao wa kuanza kutumia usafiri huo maridadi, unaotarajiwa kuanza Septemba mwaka huu.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Claudia Kitta, Meneja wa Bandari za Ziwa Nyasa, Abed Gallus na Msimamizi wa Kituo cha Mamlaka ya Mapato (TRA) katika bandari za Kyela, Gerson Charles, walipofanya mazungumzo na gazeti hili kwa nyakati tofauti wilayani Kyela hivi karibuni.

Mkuu wa wilaya, Kitta, anasema uwepo wa meli mbili za kisasa za kubeba mizigo za Mv Njombe na Mv Ruvuma pamoja na meli ya abiria Mv Mbeya II ni ukombozi mkubwa kwa wananchi, hususani wa mikoa ya Mbeya, Njombe na Ruvuma zinazopakana na ziwa hilo pamoja na nchi jirani za Malawi na Msumbiji.

“Ninapenda kuchukua fursa hii kutoa wito kwa wananchi kuanza kutumia hizi meli. Wananchi wetu hawana sababu tena kutumia njia ndefu na ghali ya barabara badala ya kutumia njia ya maji,” anasema. Anaishukuru serikali ya awamu ya tano kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuboresha pia bandari za Ziwa Nyasa ili kutoa huduma bora zaidi na za kisasa kwa wananchi.

Meneja wa Bandari za Ziwa Nyasa, Abed Gallus, naye anatoa wito kwa wananchi na wafanyabiashara wanaoendesha shughuli zao kati ya Ruvuma na Mbeya kutumia usafiri wa maji anaosema ni nafuu sana. Anatoa mfano kwamba kusafirisha tani moja ya makaa ya mawe ambayo yanachimbwa kwa wingi mkoani Ruvuma katika wilaya za Mbinga na Nyasa hadi Mbeya ni Sh 110,000.

“Lakini kusafirisha tani hiyo hiyo ya makaa ya mawe kwa umbali huo huo kwa kutumia njia ya maji ni Sh 85,000. Kwa hiyo utaona hapo kwamba kwa kila tani moja ya makaa ya mawe mtu anaokoa Sh 25,000 endapo atatumia njia ya maji,” anasema. Mchimbaji mdogo katika mgodi wa Liweta, Richard Mahundi, anaamini kwamba soko la makaa ya mawe ni kubwa na litazidi kuongezeka kutokana na Tanzania kuanzisha sera ya viwanda.

“Viwanda vingi vitazidi kujengwa kutokana na sera ya viwanda na jambo la kuzingatia ni kwamba viwanda karibu vyote vinategemea sana makaa ya mawe katika uzalishaji,” anasema. Anafafanua kwamba makaa ya mawe hutumika kwa ajili ya kutoa moto wa kuchomea bidhaa mbalimbali wakati wa uzalishaji na gharama nafuu kulinganisha na nishati zingine.

Kwa sasa kiwanda cha saruji kilichoko Mbeya cha Tembo Cement ni miongoni mwa viwanda vikubwa vinavyotumia makaa ya mawe kwa wingi katika uzalishaji wa bidhaa hiyo. Kuhusu usafiri wa abiria, Meneja wa Bandari za Ziwanya Nyasa, Gallus, anawahimiza abiria kutumia fursa ya ujio wa meli ya Mv Mbeya II kusafiri wao na mizigo yao kwa gharama nafuu katika mwambao wa Ziwa hilo. “Usafiri wa meli ni nafuu na wa starehe. Isitoshe mtu anaweza kusafiri na mzigo wa tani moja kwenye meli, jambo ambalo haliwezekani kwa usafiri wa basi,” anasema.

Msimamizi wa Kituo cha Mamlaka ya Mapato (TRA) kinachoshughulikia mizigo na abiria katika bandari za Kyela, Gerson Charles, anasema atamshangaa sana mtu atakayeendelea kutumia usafiri ghali na mrefu wa barabara kati ya Songea na Mbeya badala ya kutumia njia fupi ya maji na nafuu ya maji. “Wito wangu kwa wafanyabiashara ni kuwataka wajue kwamba mambo mengi yanafanyika kuboresha bandari za Ziwa Nyasa na usafiri katika ziwa hili, kwa hiyo ni wakati mwafaka wa kutumia vilivyo neema hii.

Ni vizuri watu watumie hizi meli mpya zilizokwishajengwa na zinazoendelea kujengwa kwani zitawarahisishia kufikisha bidhaa zao katika vijiji na miji ilio katika mwambao wa Ziwa Nyasa,” anasema. Meneja Gallus anasisitiza kwamba TPA imedhamiria kuboresha bandari, usafiri na usafirishaji ndani ya Ziwa Nyasa. “Miradi tulio nayo ni ya kuboresha usafiri na kuongeza uwezo wa bandari za Ziwa Nyasa katika kuhudumia mizigo na hata abiria anasema,” anasema.

Anafafanua kwamba kwa kuwa mizigo mingi, hususani makaa ya mawe inatokea mkoani Ruvuma, wanaboresha sasa bandari ya Ndumbi iliyoko mkoani humo na ya Kiwara iliyoko Kyela ambako makaa hayo hufikia. Anasema katika bandari ya Kiwira wanajenga sakafu ngumu kwa ajili ya kuhifadhi mzigo huo na kwamba hatua hiyo itawezesha malori kuchukulia hapo mzigo badala ya kusubiria kwenye meli.

“Tunapohifadhi mzigo katika eneo hilo tutarahisisha ushushaji wa mzigo katika meli. Yaani meli ikija itachukua muda mfupi kushusha mzigo wote na kuuweka hapa na kisha usombaji unafanyika taratibu kutokea hapa huku meli ikiondoka kwenda kuchukua mzigo mwingine. “Kwa kufanya hivyo tuna hakika kwamba bandari za Ziwa Nyasa zitaongeza uwezo wake wa kuhudumia mzigo kwa uharaka,” anasema Gallus. Anasema katika bandari hiyo ya mizigo ya Kiwira pia wanajenga gati mbili ambazo zitawezesha kuhudumia meli tatu kwa wakati mmoja.

“Tulikuwa na gati moja ambalo lilikuwa linatuwezesha kuhudumia meli moja tu kwa wakati mmoja. Gati hizi mbili zitakapokamilika tutakuwa na uwezo wa kuhudumia meli tatu kwa wakati mmoja na hivyo kupunguza muda wa meli kusubiria nje. Mteja hatopoteza muda,” anasema. Mchimbaji makaa ya mawe katika mgodi wa Liweta, Mahundi, anasema wao wameshachangamkia tayari hatua hizo zinazochukuliwa na TPA.

Anasema wamehamasika kuanza kuchimba makaa ya mawe mara tu baada ya meli mbili za mizigo kujengwa sambamba na ujenzi wa bandari ya Ndumbi. “Kwa kweli isingekuwa ni uamuzi wa serikali kutuboreshea bandari ya Ndumbi na ujenzi wa hizi meli mbili za mizigo, wala tusingefikiria kuanza mradi huu sasa,” anasema. Anawahimiza wafanyabiashara wengine nao kuchangamkia fursa hiyo.

KIWANGO cha utabiri wa hali ya hewa nchini kinazidi kukua ...

foto
Mwandishi: Hamisi Kibari

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi