loader
Picha

Aina za viwanda vinavyohitajika nchini

KWA miaka mingi sekta ya viwanda imekuwa haifanyi vizuri, na Tanzania imeendelea kutegemea kilimo chenye tija ndogo na sekta ya kuzalisha malighafi na bidhaa zenye thamani ndogo.

Matokeo yake, mchango wa viwanda katika pato la taifa umebaki vilevile kwa muda mrefu. Pia, uchumi umekuwa ukikua kwa asilimia 7 kwa miaka 15 iliyopita. Ukuaji huo ni chini ya kiwango kilichokadiriwa cha kati ya asilimia 8 na 10, kinachohitajika kupunguza na hatimaye kuondoa umaskini.

Ujenzi wa viwanda unatajwa kuwa moja ya mikakati madhubuti itakayowezesha ukuaji wa uchumi kuhamia kwenye uzalishaji wa juu utakaoongeza thamani kubwa tofauti na ule wa sasa ambao umetawaliwa na uzalishaji wa malighafi. Kwa kutambua umuhimu wa viwanda, serikali ya awamu ya tano imekuja na dhamira mpya ya kufufua viwanda na kuanzisha vipya.

Lengo la mpango huo limetajwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 - kuwaletea wananchi maisha bora na kujenga uchumi imara wenye uwezo wa kukabiliana na ushindani. Kwa maana hiyo, lazima tuhakikishe kwamba viwanda vinavyoanzishwa vinatimiza matakwa hayo. Hata hivyo, katika kutimiza azma ya ujenzi wa viwanda, lipo swali ambalo halijajibiwa: tunahitaji kujenga viwanda vya aina gani na wapi? Tuzingatie kuwa, ujenzi wa viwanda ni suala moja, na aina ya viwanda na vijengwe wapi ni suala lingine.

Hili ni swali la msingi linalohitaji majibu kama tunataka kunufaika na ujio wa viwanda.

SIFA ZA VIWANDA VITAKAVYOTIMIZA MATAKWA YA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2025

Viwanda vitakavyotimiza matakwa ya Dira ya Maendeleo ni vile vyenye sifa zifuatazo;

(i) Viwanda vya kuongeza thamani rasilimali tulizo nazo Tanzania imejaliwa kuwa na rasilimali nyingi, na watu wengi wanategemea rasilimali hizo kwa ajili ya kujipatia mkate wao wa kila siku. Kwa hiyo, kuanzisha viwanda vitakavyoongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, misitu, madini na utalii vitakuwa na mchango mkubwa kwenye maisha ya wananchi na ukuaji wa uchumi kwa jumla.

Hapa tunazungumzia viwanda ambavyo vina uhusiano ya kuondoa umaskini wa mamilioni ya wananchi wanaoishi vijijini. Huu ndio ulikuwa mtazamo wa Mwasisi wa Taifa hili, Mwalimu Julius K. Nyerere katika kuanzisha viwanda vya kusindika/kuchakata na kutengeneza bidhaa na huduma zinazotokana na mazao yanayozalishwa nchini na kuuzwa ndani na nje ya nchi. Maana yake ni kwamba, viwanda hivyo vitatumia malighafi kutoka kwa wakulima na hivyo kuwa soko la uhakika la bidhaa hizo. Lakini pia, kwa kuongezea thamani, bidhaa na huduma zinazozalishwa, wakulima na wafanyabiashara wa kimataifa watapata bei nzuri na kipato chao kitaongezeka.

(ii) Viwanda vitakavyoajiri watu wengi Kuna aina mbili za teknolojia zinazotumika viwandani: Teknolojia ya kutumia nguvukazi nyingi au misuli na teknolojia ya kutumia mashine au mitambo.

Wakati teknolojia inayotumia misuli inaajiri watu wengi lakini ina ufanisi mdogo, teknolojia ya mashine au mitambo inatumia teknolojia bora, inaajiri watu wachache wenye ujuzi wa hali ya juu na ina ufanisi na ushindani wa hali ya juu. Kwa kuwa teknolojia zote mbili ni muhimu katika kutimiza matakwa ya Dira ya Taifa ya Maendeleo, ni vema serikali ikahakikisha viwanda vya aina hizo mbili za teknolojia vinaanzishwa. Serikali inaweza kuiga kutoka China kwa kuweka vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi kuvutia viwanda vinavyotumia teknolojia ya nguvukazi.

(iii) Viwanda vya kuzalisha bidhaa na huduma zenye faida linganifu Tanzania ina faida linganifu au fursa nyingi zinazotokana na kuwa na rasilimali nyingi, mahali nchi ilipo, ongezeko la idadi kubwa ya watu wenye umri mdogo, ongezeko la miji na fursa zinazoambatana nayo na matumizi ya teknohama yaliyosambaa nchi nzima. Ili ujenzi wa viwanda uwe na manufaa makubwa kwa wananchi na taifa kwa jumla, lazima viwanda hivyo vianzishwe katika kusindika/ kuchakata au kuzalisha bidhaa ambazo Tanzania ina faida linganifu dhidi ya mataifa mengine.

Kwa maana hiyo, viwanda vianzishwe kuzalisha bidhaa na huduma ambazo faida linganishi ya Tanzania inaongezeka na mahitaji ya bidhaa na huduma hizo duniani pia yanaongezeka. Hii inajumuisha bidhaa kama korosho, nafaka zisizokobolewa, maharage ya kokoa, nazi, mafuta ya mbegu na mimea, mashudu, madini ya dhahabu; na huduma za utalii. Pia, viwanda vizalishe bidhaa na huduma ambazo faida linganifu ya Tanzania inapungua, lakini mahitaji ya dunia kwa bidhaa na huduma hizo yanaongezeka.

(iv) Viwanda vinavyotumia teknolojia ya kisasa na ubunifu Ili kujenga uchumi unaokua kwa kasi itakayo-tufikisha kwenye uchumi wa kati na wenye ushindani, tunahitaji kuanzisha viwanda vinavyotumia teknolojia ya kisasa na ubunifu. Matumizi ya teknolojia ya kisasa yana mchango mkubwa wa kuongeza ufanisi na tija kwenye uzalishaji. Matokeo yake, bidhaa na huduma zinazozalishwa zinakuwa na uwingi, ubora na ushindani kwenye soko. Hata hivyo, tunapohamasisha mpango huu tuwe makini maana kuna hatari ya kuwapendelea wenye uwezo wa kutumia teknolojia ya kisasa na kuwasahau maskini ambao ndio walengwa wa mpango wa kujenga viwanda.

(v) Viwanda visambae nchini kote Kwa kawaida uanzishwaji wa viwanda unaambatana na shughuli nyingine za kiuchumi kama ujenzi wa barabara, umeme, mawasiliano na nyinginezo zinazochangia kuleta maendeleo kwenye eneo husika. Ili maeneo mengi yaweze kunufaika na mchango huo, ni vema serikali ikaweka mkakati wa kuhakikisha viwanda vinatawanyika nchi nzima badala ya kujikusanya maeneo machache. Tujifunze kutoka kwa Mwalimu Nyerere aliyehakikisha viwanda vinatawanyika maeneo mengi nchini.

Ni vema pia juhudi za makusudi zikafanyika kuhakikisha viwanda vinaanzishwa katika miji midogo na hasa maeneo ya vijijini. Kwa kufanya hivyo, viwanda vitakuwa na mchango mkubwa kukuza uchumi na kupunguza umaskini nchini.

HITIMISHO

Ili ujenzi wa viwanda uwe na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wenye ushindani na kuboresha maisha ya watu na kuondoa umaskini, ujenzi wa viwanda ni muhimu lakini suala la aina ya viwanda na vijengwe wapi ni muhimu zaidi.

Kwa mfano, iwapo viwanda vingi vinavyojengwa vitakuwa vile ambavyo haviajiri watu wengi, havina mwingiliano na sekta ya kilimo, vinatumia teknolojia ya hali ya juu na vimeanzishwa maeneo ya mijini tu; vinaweza vikakuza uchumi kwa kasi lakini havitakuwa na mchango mkubwa kuwaletea wananchi maisha bora na mazuri, na kupunguza umaskini.

HIFADHI ya mazingira ni juhudi zinazofanywa na binadamu ili kuhakikisha ...

foto
Mwandishi: Prof. Kitojo Wetengere

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi