loader
Picha

Magufuli ataka minada ya nyamapori

RAIS John Magufuli ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuanzisha minada ya nyama za porini au kutoa vibali vya kuuzwa kwa nyama hizo, kwa lengo la kujenga mazingira rafi ki baina ya wananchi na hifadhi.

Amesema wizara hiyo inatakiwa kuanzisha shughuli zitakazowavutia wananchi, kulinda na kuendeleza hifadhi za taifa.

Rais Magufuli alisema hayo jana wakati akizindua Hifadhi ya Taifa ya Burigi iliyopo Chato mkoani Mwanza, ambapo alimtaka Waziri Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla ikibidi kurekebisha sheria, ili wananchi wanufaike na hifadhi hizo.

Hifadhi ya Burigi ni ya tatu kwa ukubwa nchini yenye kilometa za mraba 4,702, ambapo ya kwanza ni Ruaha yenye ukubwa wa kilometa za mraba 20,300 na Serengeti ni ya pili yenye ukubwa wa kilometa za mraba 14,763. Hifadhi hiyo inaundwa na mapori matatu ambayo ni Kimisi, Biharamulo na Burigi.

Rais Magufuli alisema kukosekana kwa mipango, itakayowawezesha wananchi kunufaika moja kwa moja na hifadhi za taifa ni kati ya sababu za wananchi kutoshiriki kikamilifu katika kuimarisha ulinzi wa wanyama wa kwenye hifadhi hizo.

Alisema,”Kenya kuna mahala ambapo wananchi wanaenda kula nyama mbalimbali za wanyama wa porini na hivyo wanajiona kuwa ni sehemu ya hifadhi hizo, hivyo basi waziri anzisha minada ya nyama za porini au toa vibali vya kuuzwa kwa nyama hizo, lakini sio tu kuishia mtalii kuja kuwinda na kuua wanyama kisha kuwaacha tu wakati kwa wale wanaoliwa wanaweza kuuzwa kwa wananchi”.

Katika kile kinachoweza kutafsiriwa kuwa ni baraka ya uzinduzi wa hifadhi hiyo, mvua kubwa ilinyesha kwa muda mfupi katika tukio hilo, ambalo pia lilihudhuriwa na mabalozi, wawekezaji na maelfu ya wakazi kutokea maeneo jirani.

Kabla ya uzinduzi wake, wakazi wa maeneo jirani na hifadhi walipikiwa na kula aina tofauti za wanyama pori watano, ambapo licha ya Rais kupongeza hatua hiyo, alimpongeza mara tatu aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali mstaafu, Salim Kijuu kwa kutumia siku mbili kati ya tatu alizopewa, kuondoa wafugaji kwenye pori hilo wakati akiwa Mkuu wa Mkoa.

Alisema, amevutiwa na namna alivyotekeleza kazi hiyo kwa umakini, akiiongoza kamati iliyoundwa kushughulikia usafishwaji wa pori hilo na kuzitaka mamlaka nchini, kujenga utamaduni wa kuwapongeza na kuwatunza watu wanaofanya mambo makubwa kwenye kazi zao.

Mkuu huyo wa Mkoa mstaafu alikabidhiwa hundi ya Sh milioni 10 na cheti cha utambuzi.

Pia, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Saada Malunde alipatiwa Sh milioni tano huku Faustine Masalu aliyekuwa Mkuu wa Operesheni kwenye kamati hiyo na Mkuu wa Pori la Kimisi, Bilamungu Kagoma wakipatiwa Sh milioni mbili kila mmoja.

Rais Magufuli alisema kamati hiyo, iliifanya kazi yake kikamilifu, hatua iliyowahisha uanzishwaji wa hifadhi hiyo.

Alikemea watendaji wengine wanaopewa majukumu ya kulinda rasilimali za nchi, kuzembea katika kutelekeza majukumu yao.

Alisema,“Ninashangaa kusikia kuwa kuna askari wenye silaha na mafunzo lakini kwenye maeneo wanayolinda kunakuwa na majangili wanaendelea kuua tembo, nataka hali hiyo kukoma mara moja na badala yake muwe mnawawahi wao mapema au ikishindikana mfukuzwe kazi”.

Aliwapongeza askari wa Jeshi Usu la Mamlaka ya Uhifadhi Tanzania (Tanapa) kwa kushiriki kikamilifu kuwadhibiti majangili, hali iliyosaidia kudhibiti mauaji ya tembo, ambapo mwaka 2014 kulikuwa na tembo 43,030 na kwa sasa kuna tembo zaidi ya 60,000 nchi nzima.

Alisema,“tulikuwa na faru zaidi ya 750 kwenye miaka ya 1970 na 1980 ila wakapungua hadi kufikia faru 15. Kutokana na jitihada za kudhibiti ujangili huu faru wameongezeka kufikia zaidi ya 40 ambapo Faru Rajabu amefanya kazi nzuri ya kusaidia ongezeko hilo”.

Katika kuhakikisha kuwa Jeshi Usu la Tanapa linafanya kazi kikamilifu, wakuu wa taasisi zinazojihusisha na maliasili na utalii kutokea Tanapa, Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Bonde la Ngorongoro na uhifadhi wa wanyamapori walipatiwa vyeo ngazi ya kamishna.

Akiizungumzia zaidi hifadhi hiyo ya Burigi, Rais Magufuli aliwataka wawekezaji zaidi, kujitokeza kuwekeza miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye maeneo jirani na hifadhi hiyo.

Alibainisha kuwa hifadhi hiyo inafungua milango ya uwekezaji na utalii kwa wakazi wa mikoa ya Mwanza na Kagera na itaongeza fursa za biashara na ajira kwa wananchi wanaoizunguka.

Alisema ni dhahiri kuwa hifadhi hiyo, itaiwezesha sekta ya utalii kuendelea kuwa sekta inayoongoza kuiingizia nchi fedha za kigeni, hivyo na kuongeza mchango wake katika pato la taifa kutoka asilimia 17 ya sasa.

Alisema:“Ujangili na uchungaji usiozingatia uhitaji ndio chanzo cha kupungua kwa wanyama nchini, hivyo kupandishwa hadhi kwa mapori hata matatu na kuwa hifadhi kuchagize maendeleo ya uchumi wa wananchi na serikali kwa ujumla. Vipo vijiji hapa vinaitwa majina kutokana na zamani wingi wa wanyama waliokuwa wakivizungumza.

Kwa mfano Kijiji cha Kanyama kinamaanisha wanyama, Kashimba kinamaanisha simba, Nyambifi kinamaanisha fisi huku Nyambogo kikimaanisha Mbogo, yaani kulikuwa na wanyama wenye majina hayo wengi na ndio maana vikaitwa hivyo sasa wanyama hao warejee”.

Alisema serikali itafikia watalii milioni mbili ifikapo mwaka 2020 kutoka milioni 1.5 wanaokuja sasa, baada ya kuongeza mbuga za wanyama kutoka mbuga 16 mpaka mbuga 19. Mbuga zilizoongezeka ni Burigi Chato, Ibanda Kyerwa na Rumanyika Karagwe.

Alisema utalii unachangia pato la taifa kwa asilimia 25, hivyo uwepo wa hifadhi za taifa utachangia kuwaondoa wananchi katika umasikini endapo watatumia fursa za uwepo wa mbuga hizo.

Habari hii imeandikwa na Diana Deus, Chato na Evance Ng’ingo, Dar.

Rais John Magufuli amemuagiza Naibu Mkurugenzi Mkuu wa ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi