loader
Picha

Serikali yaonya wanaosambaza picha za maiti

SERIKALI imetoa onyo la mwisho kuhusu matumizi mabaya ya simu za mkononi yanayofanywa na baadhi ya watu wanaopiga picha miili ya watu wanaokufa kwenye ajali na kuzirusha mitandaoni.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe ametoa onyo hilo jijini Dar es Salaam wakati wa kuaga miili ya wafanyakazi watano wa Azam Media Limited waliokufa juzi mkoani Singida kwenye ajali ya barabarani.

“Acheni kurusha picha za vifo vya ajali mitandaoni, utakuta mtu anarusha picha bila kujali kuwa waliokufa ni binadamu na wana ndugu zao, unadhani ndugu zao wanapoziona picha hizo wanajisikiaje, onyo hili ni la mwisho, hatutasema tena, Sheria ya Makosa ya Mtandao itaanza kufanya kazi yake,”alisisitiza Waziri Mwakyembe.

Wafanyakazi hao waliokufa kwenye ajali hiyo na kuagwa jana Makao Makuu ya Kampuni hiyo ni Salim Mhando, Silvanus Kassongo, Charles Wandwi, Florence Ndibalema na Said Haji.

Marehemu Salim Mhando alizikwa jana kwenye makaburi ya Manzese- Sweetcorner jijini Dar es Salaam, Charles Wandwi atazikwa leo kwenye makaburi ya Sinza, wakati mwili wa Said Haji ulisafirishwa jana kwenda Hale-Tanga, Kassongo alisafirishwa kwenda Iringa na mwili wa Florence Ndibalema utasafirishwa leo kwenda Bukoba kwa maziko.

Katika salamu zake za rambirambi, Dk Mwakyembe alisema kuanzia sasa serikali haitaongea tena kuhusu tabia ya watu kurusha matukio ya vifo vya ajali mitandaoni badala yake Sheria ya Makosa ya Mtandao itaanza kuwashughulikia wenye tabia hiyo.

Pamoja na onyo hilo, Dk Mwakyembe pia aliipongeza Azam Media Limited kwa mchango mkubwa wanaoutoa katika tasnia ya habari na taifa kwa ujumla.

Naibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, alisema kuwa uchunguzi wa ajali hiyo umeshaanza na dereva wa lori lililogongana uso kwa uso na basi aina ya Coaster lililowabeba wafanyakazi hao wa Azam ameshakamatwa.

Alisema Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani linaendelea kukusanya ushahidi kutoka kwa mashuhuda wa ajali hiyo ili taratibu nyingine za kisheria zifuate.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam Media Limited, Tido Mhando, alisema wafanyakazi hao waliokufa waliondoka Jumapili jioni kwenda Chato mkoani Geita kwa ajili ya kurusha moja kwa moja uzinduzi wa Hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato uliofanywa na Rais John Magufuli jana.

Alisema wafanyakazi hao walilala Singida na saa moja asubuhi waliendelea na safari yao, lakini baada ya muda wa saa moja na nusu baadaye wakapata ajali na kupoteza maisha.

Kutokana na msiba huo Tido aliishukuru serikali na Shirika la Hifadhi ya Taifa (TANAPA) kwa ushirikiano mkubwa waliowapatia, lakini pia akatoa wito kwa familia zilizowapoteza wapendwa wao hao kuwasiliana na menejimenti ya Azam Media Limited wakati wowote kama wanahitaji ushauri au msaada wa jambo lolote.

Aidha taasisi na watu mbalimbali walituma salamu za rambirambi kwa msiba huo.Miongoni mwa taasisi hizo ni Chama Cha Mapinduzi.

“Wafanyakazi hawa wa Azam Media Limited wamekufa kishujaa kwa sababu wamekufa wakiwa kazini, Chama Cha Mapinduzi (CCM) tumefanya nao kazi kwa karibu sana,” alieleza Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole wakati akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya chama hicho.

Wengine waliotoa salamu za rambirambi ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, Mbunge wa Ilala (CCM), Musa Azan Zungu, Mkurugenzi wa Masoko wa Benki ya CRDB, Tully Mwambapa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira Tanzania (TFF), Wilfred Kidao.

Wengine ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dk Ayoub Rioba, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk James Kilaba, Mkurugenzi Mtendaji wa ITV na Radio One, Joyce Mhavile, Deodatus Balile aliyetoa salamu kwa niaba ya Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania na Hamisi Mzee alitoa salamu kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Rais John Magufuli amemuagiza Naibu Mkurugenzi Mkuu wa ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi