loader
Picha

Wanasiasa waonywa rushwa kwenye uchaguzi

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoa wa Iringa imeonya wanasiasa ikitaka wajiepushe na vitendo vya rushwa katika mchakato wa kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

Akizungumza na wanahabari wakati akitoa taarifa ya robo ya nne (Aprili -Juni) ya utekelezaji wa majukumu yao, Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Iringa, Mweli Kilimali alisema watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Ili kuwasaidia wananchi kufanya uamuzi sahihi kwa kuchagua viongozi waadilifu na wasiojihusisha na rushwa, Kilimali alisema katika robo ya Julai hadi Septemba, kipaumbele cha Takukuru kitakuwa kinatoa elimu ya kuzuia na kupambana na rushwa katika uchaguzi huo.

“Nitoe mwito kwa wadau wote wa uchaguzi huo kushirikiana na Takukuru kuwadhibiti wanasiasa na wapambe wao watakaojihusisha na vitendo na rushwa kwa kutupa taarifa zitakazosaidia kuwanasa,” alisema.

Pamoja na kipaumbele hicho, Kilimali alisema Takukuru itaendelea kufuatilia utekelezaji wa maendeleo ili iwe na ubora kulingana na gharama zinazotolewa na serikali.

“Lakini pia tutaendelea kufanya uchambuzi wa mifumo kubaini mianya ya rushwa na kushauri namna nzuri ya kuzuia mianya hiyo,” alisema.

Alisema Aprili hadi Juni, mwaka huu, Takukuru ilifanya ukaguzi miradi ya maendeleo 16 yenye thamani ya Sh bilioni 17 iliyokutwa bila tatizo.

Alisema kati ya miradi hiyo, minane ya wilaya ya Iringa, minne ya Kilolo na minne ya Mufindi. Alisema katika kipindi hicho Takukuru ilitoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya vitendo vya rushwa kupitia semina 14, mikutano ya hadhara 76 na mijadala ya wazi kwa wananchi.

Alisema klabu 48 za wapinga rushwa zilifunguliwa na 66 ziliimarishwa na kufanya vipindi mbalimbali vya redio na kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kupitia vyombo vya habari.

Alisema kupitia elimu kwa umma, wananchi 981 wamepata elimu ya rushwa katika kipindi hicho sambamba na wanafunzi zaidi ya 5,953.

“Pia katika kipindi hicho cha Aprili hadi Juni, Takukuru mkoa wa Iringa ilipokea malalamiko 34.

Malalamiko yanayohusu rushwa yako katika hatua mbalimbali za uchunguzi na matano kati yake yamefikishwa mahakamani,” alisema.

Kilimali aliwapongeza wananchi wa Wilaya ya Mufindi akisema katika kipindi hicho walikuwa na mwamko mkubwa wa kuripoti matukio ya rushwa na kutaka wilaya nyingine kuiga mfano.

Rais John Magufuli amemuagiza Naibu Mkurugenzi Mkuu wa ...

foto
Mwandishi: Frank Leonard, Iringa

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi