loader
Picha

TEC, Bakwata, CCT kuanziasha uchumi jamii

BARAZA la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), zimedhamiria kuunga mkono serikali kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati unaochochewa na viwanda kwa kuanzisha mkakati mpya wa mfumo wa uchumi wa jamii.

Katibu Mkuu wa TEC, Padri Dk Charles Kitima aliwaambia wanahabari ofisini kwake Kurasini Dar es Salaam kufanikisha hilo, keshokutwa TEC, Bakwata na CCT zitazindua kitabu maalumu Social Market Economy Model for Tanzania (Smet) katika hafla itakayofanyika katika Hoteli ya Courtyard, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Dk Kitima, mkakati huu wa mfumo wa uchumi wa jamii ni matunda ya ushirikiano wa pamoja wa viongozi wa dini nchini na wataalamu wa uchumi wa soko huria.

Alisema wataalamu hao ni pamoja na watafiti wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Mzumbe na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino cha Tanzania (SAUT).

“Julai 11 na 12 mwaka huu, tutakuwa na warsha kwa viongozi wa dini zote wapatao 100 na washiriki wengine kutoka taasisi mbalimbali zikiwamo za serikali ili kuwawezesha wadau kutangaza na kushiriki kikamilifu katika mfumo wa uchumi wa soko wa jamii kwa Tanzania (Smet) kama njia mbadala ya kukuza uchumi nchini katika kipindi hiki cha mpito na maendeleo kupitia viwanda,” alisema Dk Kitima.

“Huu ni mfumo unaolenga utu wa mtu bila kunyanyasa wengine; unaolenga kumfaa binadamu na siyo kumwangamiza; ni mfumo unaolenga kutunza mazingira siyo kuyaharibu na yote haya yanakuwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo,” alisema Dk Kitima.

Alisema licha ya jukumu lao kubwa kuwaweka binadamu karibu na Mungu, viongozi wa dini pia wanatambua wajibu wao kufanya binadamu hao kushiriki uchumi shirikishi wa uzalishaji mali ili wawe na maisha bora na maendeleo.

Kwa msingi huo, kwa niaba ya taasisi za dini washirika wa mkakati huu, Dk Kitima alisema Watanzania wanapaswa kushirikishwa na kuelewa umuhimu wa uzalishaji na uendeshaji biashara adilifu katikati ya uchumi wampende zaidi Mungu na wapate maendeleo ya kweli.

Alisema katika warsha hiyo, viongozi wa dini na washiriki wengine wataelimishwa mfumo wa uchumi wa jamii ili nao wasambaze elimu hiyo.

“Huu ni uchumi unaolenga kuwafanya watu waone fursa kutengeneza uchumi wa mtu binafsi, familia na uchumi wa taifa ili serikali ipate pato lake na kwenye kilimo, mtu azalishe vizuri, alipwe vizuri na kupata mapato mazuri,” alisema kasisi huyo wa Kanisa Katoliki nchini.

“Tunataka tuwajenge watu wawe na ushindani na uzalishaji shirikishi katika uchumi hata kupitia Watanzania kumiliki kampuni mbalimbali na kubwa hata kupitia hisa ndiyo maana tunahimiza pia watu wafundishwe kuzalisha kiaudilifu na kulipa kodi,” alisema.

“Watu watambue biashara siyo tu kununua simu China na kuja kuziuza Tanzania, bali kila mmoja afikirie na kuongeza juhudi za kuzalisha simu hizo nchini. Hii itaepusha kasumba ya vijana wanapohitimu masomo, kutaka kuajiriwa badala ya kujiajiri na kuajiri wengine,” alisema.

Alisema umefika wakati Watanzania waepuke kuwa na mfumo wa uchumi usiowafanya kuwa soko la bidhaa na huduma za wengine wa nje.

SHIRIKA la Taifa la Biashara (ZSTC) limesema ni makosa kwa ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi