loader
Picha

Ziara ya JPM Namibia yaanza kulipa

ZIARA ya siku mbili nchini Namibia ya Rais, Dk John Magufuli imeelezwa kuanza kuonesha mafanikio baada ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupokea ugeni kutoka Kampuni ya Burmeister and Partners (PTY) Ltd inayomiliki kiwanda cha kuchakata nyama nchini humo iliyoonesha nia ya kuwekeza hapa nchini.

Hayo yalithibitishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo, Profesa Elisante Ole Gabriel ambaye amemshukuru Rais Magufuli kutokana na ziara yake ya kikazi ya siku mbili aliyofanya nchini Namibia kuanzia Mei 27 hadi 28 mwaka huu.

Akizungumza ofisini kwake jijini Dodoma na mmoja wa wakurugenzi katika kampuni ya Burmeister and Partners (PTY) Ltd Hendrick Boshoff, Profesa Gabriel alisema lengo la ziara yake ni kupata taarifa za awali, kutoka kwa wataalamu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili waweze kuwa na njia sahihi ya uwekezaji ambao utakuwa na tija kwa watanzania kupitia sekta ya Mifugo.

“Mheshimiwa rais alifanya ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Namibia akiambatana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina na viongozi wengine, nichukue fursa hii kwa niaba ya wizara kumshukuru mheshimiwa rais kutuanzishia suala la soko la mazao ya mifugo hususan nyama, tumetembelewa na mmoja wa wakurugenzi wa Kampuni ya Burmeister and Partners (PTY) Ltd inayomiliki kiwanda cha kuchakata nyama nchini Namibia ili kukutana na wataalam baada ya rais kuonesha muelekeo na wao wakaitikia,” alisema Profesa Gabriel.

Katika mazungumzo hayo Katibu Mkuu huyo aliuhakikishia ugeni huo kutoka Namibia kuwa wizara iko tayari kuhakikisha nia ya kampuni hiyo kuanzisha kiwanda kingine cha kuchakata nyama hapa nchini inafikia katika utekelezaji baada ya ziara ya mheshimiwa rais nchini Namibia. Profesa Gabriel alieleza kuwa ujio wa ugeni huo unaratibiwa na wizara nne zikiwemo za Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Viwanda na Biashara, Ofisi ya Waziri Mkuu eneo la Uwekezaji na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika Sekta ya Mifugo.

Aidha, ametoa wito kwa watanzania kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali hususani zinazolenga kuongeza masoko ya kutengeneza na kuuza bidhaa zinazozalishwa hapa nchini. “Viwanda kama hivi vikija ajira nyingi zitaongezeka na pia pato la taifa litaongezeka, bado tuko chini katika ulaji wa nyama takwimu zilizotolewa na Shirika la Chakula Duniani (FAO) zinaonesha walau mtu wa kawaida anatakiwa kula kilogramu 50 kwa mwaka, bado kwa watanzania tunakula kilogramu 15 kwa mwaka mzima, tunaleta wenzetu waongeze bidii katika hilo ili wazalishe na soko la ndani liwepo tuuze na nje ya nchi,” alifafanua Profesa Gabriel.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Burmeister and Partners (PTY) Ltd inayomikili kiwanda cha kuchakata nyama nchini Namibia Hendrick Boshoff alimwambia Profesa Gabriel kuwa, kampuni hiyo ilianza kuendesha shughuli zake miaka 40 iliyopita na wamekuja nchini Tanzania wakilenga zaidi uwekezaji wa kuyaongezea thamani mazao ya mifugo hususan nyama.

Akimuakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Viwanda Vidogo na Kati (DSME), Dk Consolata Ishebabi alisema ugeni huo utafahamishwa pia fursa mbalimbali zilizopo hapa nchini kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) ili kufahamu mazingira mbalimbali ya uwekezaji yakiwemo ya sekta binafsi.

Aidha, Dk Ishebabi alifafanua kuwa ugeni huo utafikishwa pia katika Kampuni ya Ranchi ya Taifa (NARCO) ambapo watafikishwa katika Ranchi ya Kongwa ambayo ipo chini ya NARCO kuweza kuona aina ya mifugo iliyopo nchini na waweze kupata taarifa za jumla ambazo zitawapatia mwanzo mzuri wa kuwekeza hapa nchini katika Sekta ya Mifugo.

SERIKALI imetoa ripoti ya uchunguzi wa Maabara ya Taifa ya ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi