loader
Picha

‘Shamba la zabibu liwe la kimkakati’

HALMASHAURI ya Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma imeomba kuuchukua mradi wa shamba la zabibu la Chinangali 11 wa ekari zaidi ya 1,250 uwe wa kimkakati ili kuunusuru mradi huo unaosuasua katika uendeshaji wake.

Mradi huo sasa upo chini ya wakulima ambao baadhi wameshindwa kuendesha shamba la ekari 290 kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwemo madeni hivyo halmashauri inakusudia kulipanua shamba na kufikia ekari hizo 1250. Ombi hilo limetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Athuman Masasi wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge katika shamba hilo jana.

Masasi alisema halmashauri italipa deni la wakulima kwa Benki ya CRDB la Sh bilioni 2.7 zilizokuwa zikiongezeka kila mwaka kutokana na malimbikizo ya riba iliyosimamishwa. “Sisi kama halmashauri tulikubaliana tuuchukue mradi huu kama mradi wa kimkakati badala ya kujenga soko au stendi ili tuweze kuuendesha na kupunguza deni.

Lengo sio kuwanyang’anya au kuwaondoa wananchi kwenye umiliki wao bali ni kusaidia kuendeshaji na usimamizi,” alisema. Alisema mradi huo ukisimamiwa vizuri una uwezo wa kuingiza Sh bilioni tatu hadi nne kwa mwaka na kuongeza mapato ya halmashauri. Akizungumzia mradi huo, Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Chamwino, Godfrey Mnyamale alisema shamba lina ukubwa wa ekari 1,250. Alisema shamba lina wamiliki tofauti tofauti na wanataka mfumo ubadilishwe kutoka wa mtu mmoja kwenda wa pamoja kuongeza uzalishaji.

Akijibu maombi hayo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge aliiagiza Halmashauri ya Chamwino Jumatatu impelekee mapendekezo ya kitaalamu ya kufufua mradi wa shamba hilo.

Alisema shamba la zabibu la Chinangali 11 linatakiwa lifanye kazi kwa ufanisi kuongeza mapato na kuwapa fursa wananchi wengi. Aliagiza kupatikana kwa taarifa ya utekelezaji wa maelekezo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyoyatoa alipotembelea mradi huo. “Mkurugenzi kaeni na wataalamu kutoka mkoani pendekezeni nini kifanyike ili mradi huu ufanye kazi kwa ufanisi na kutoa matokeo tarajiwa.

Waziri Mkuu alipita hapa alitoa maelekezo. Nataka nijue alielekeza nini na mmetekeleza lipi katika maelekezo hayo,” alisema Dk Mahenge. Alisema ni lazima deni lililopo lilipwe na kuwataka wakulima wa shamba hilo kujituma na kulima kwa moyo huku wakifuata maelekezo ya wataalam ili wapate wanachotarajiwa. Pia alisema halmashauri iwaandikie barua ya kuwanyang’anya mashamba mara moja wananchi wote waliotelekeza maeneo yaliyopimwa kwenye shamba hilo kwa kushindwa kuhudumia na kusimamia.

Rais John Magufuli amemuagiza Naibu Mkurugenzi Mkuu wa ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Chamwino

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi