loader
Picha

Kampuni ya simu ‘yakopesha’ wateja wake

KAMPUNI ya Vodacom imezindua huduma ya kwanza ambayo inaruhusu wateja wa M-PESA kukamilisha miamala wakati hawana fedha za kutosha katika akaunti zao za M-PESA.

Uvumbuzi huu wa kibunifu uitwao M-Pesa Songesha umezinduliwa jana katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Dar es Salaam. Akizungumzia huduma hiyo, Mkurugenzi wa M-Commerce, Epimack Mbeteni alisema, “Dhamira yetu ya kuleta mifumo bunifu ya kifedha kwa kutumia simu za mkononi ilitufanya kutazama kwa makini vikwazo vya mara kwa mara vinavyowazuia wateja wetu kukamilisha miamala yao kwa sababu ya upungufu wa fedha katika akaunti zao.

Uchunguzi huo umefanya kuja na ufumbuzi wa kibunifu wa wateja wetu kuweza kukamilisha miamala ya M-Pesa ambayo ingeshindikana kukamilika kwa sababu ya upungufu wa fedha,” alisema. Mbeteni alisema watumiaji wa M-Pesa wanaweza kufikia huduma ya Songesha kwa kupiga namba za huduma ya M-Pesa, kisha kuchagua huduma za kifedha na kujiunga na huduma hiyo ya M-Pesa Songesha. Baada ya mteja kujiunga na Songesha, atapata ujumbe wa kiwango ambacho anastahili na ataweza kutumia kiwango hicho kukamilisha miamala yake.

Kiasi hicho kitarejeshwa pale ambapo mteja atapokea fedha katika akaunti yake ya M-Pesa. “Kiwango hicho kina riba ya asilimia moja kwa siku 18 na wateja wetu wanaweza kufanya miamala kwa kutumia huduma hii kadri watakavyo ikiwa ni ndani ya kikomo cha kiwango chao.

Tumeungana na Benki ya TPB kuwezesha huduma hii na ili kuamua kiwango mteja anachostahili, benki itatumia taratibu zilizowekwa kulingana na miamala ya mteja husika katika matumizi yake ya M-Pesa,” alisema . Kwa upande wake, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya TPB, Moses Manyatta alisema, “Lengo letu kama benki ni kuhamasisha huduma jumuishi za kifedha huku tukiwahamasisha Watanzania kujenga tabia ya kujiwekea akiba na kujipatia mikopo kwa urahisi.”

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ametoa maagizo ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi