loader
Picha

Shahidi: Mhasibu Takukuru aliandaa mkataba feki

MKAZI wa Boko, Abubakar Hamisi (46) ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa mkataba wa mauziano ya kiwanja kati yake na aliyekuwa Mhasibu Mkuu wa Takukuru, Godfrey Gugai, uliandikwa Sh milioni 60 lakini walipewa Sh milioni 80 ili kupata ahuweni ya kodi.

Hamisi ni shahidi wa 20 katika kesi ya utakatishaji fedha na kumiliki mali zilizozidi kipato, inayomkabili Gugai na wenzake. Akiongozwa na Wakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Awamu Mbagwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba shahidi huyo akizungumza jana alidai kuwa Gugai ni jirani yake na amewahi kufanya naye biashara.

Alidai walifanya makubaliano baina ya familia na Gugai ya kuuziana kiwanja namba 64 kilichopo kitalu C cha Boko Ununio Dar es Salaam, kwa Sh milioni 80 na malipo yalifanyika kwa fedha taslimu. Alidai baada ya familia kufanya makubaliano na Gugai, Mwanasheria wake alienda kuandaa mkataba na walipofika nyumbani kwake jioni aliwapa na kuusoma kisha akawakabidhi fedha. Shahidi huyo aliendelea kudai kuwa katika mkataba huo uliandikwa Sh milioni 60 tofauti na makubaliano lakini walikabidhiwa fedha taslimu Sh milioni 80.

Aliendelea kudai katika mkataba huo uliofanyika nyumbani kwake akiwa na mwanasheria uliandikwa hivyo ili kuweza kupata ahuweni ya kodi. Baada ya maelezo hayo, shahidi huyo aliiomba mahakama kupokea mkataba wa mauziano ya kiwanja kama kielelezo baada ya kuutambua kwa majina na saini. Hata hivyo, upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Semi Malimi ulipinga kupokewa kwa mkataba huo wakidai kuwa ni nakala na sio nyaraka halisi ya mkataba.

Alidai nyaraka yoyote inayotolewa mahakamani lazima iwe halisi kwa mujibu wa sheria kifungu 67 (1) na kama ni nakala yapo mazingira yanayoruhusu ipokewe. Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 11, mwaka huu atakapotoa uamuzi kama kielelezo hicho kipokewe au la. Gugai na mwenzake watatu wanakabiliwa na makosa 43, kati ya hayo, makosa 19 ni ya kughushi, 23 ni utakatishaji fedha na moja ni kumiliki mali zilizozidi kipato halali, ambalo hilo linamkabili Gugai.

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ametoa maagizo ...

foto
Mwandishi: Francisca Emmanuel

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi