loader
Picha

Mtanzania aunda gari ya chakula, baiskeli ya kuchaji kwa walemavu

MABADILIKO chanya ya teknolojia yanayoendelea duniani yakitumika vizuri ni sababu ya mapinduzi ya maendeleo kwa jamii na taifa lolote. Fursa za biashara zinaongezeka ndani na nje ya nchi, ubunifu unaosababisha ukuaji wa uchumi unaonekana wazi kuanzia ngazi ya familia, kijiji, mtaa, kitongoji, kata, wilaya, mkoa na taifa.

Mtanzania Jacob Louis, mwaka 2016 alitumia fursa ya maendeleo ya teknolojia na kuunda gari ndogo aliyoipa jina la Kapalata (jina lake la ukoo). Hata hivyo mpaka leo, hakuwahi kuliendesha gari hilo barabarani kama magari mengine baada ya kukosa kibali cha Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa kile walichomueleza kuwa hawana mitambo ya kupima ubora wa magari yanayoundwa au kutengenezwa nchini.

“Waliniambia wataniandikia barua ya kujitambulisha Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ili niweze kutambulika na kupata kibali, lakini mpaka leo sijapata majibu yoyote,” anasema Louis. Pamoja na kukosa kibali hicho, Loius aliyekuja jijini Dar es Salaam mwaka 2006 kuuza bidhaa katika Maonesho ya Sabasaba akitokea Mpanda mkoani Rukwa na kisha kuwezeshwa na Shirika na Viwanda Vidogo (Sido) kutengeneza mashine za kutotolea vifaranga, anasema hajakata tamaa kwani ameendelea kubuni vitu vingine.

Akiwa mpangaji katika eneo la Sido, Vingunguti, jijini Dar es Salaam huku akiendelea kubuni na kutengeneza mashine na vitu mbalimbali, Loius anasema amejipanga kufanya mapinduzi ya kiuchumi lakini serikali inapaswa kuwatambua watu kama yeye. Hivi sasa Louis ambaye hajabahatika kusoma hata darasa la kwanza, lakini amejiongeza kwa maarifa ya kujua kusoma na kuandika, ametengeneza gari ya kuuzia chakula (food truck) maalumu kwa mamalishe na babalishe inayohamishika kutoka eneo moja kwenda lingine.

Gari hilo lenye upana wa futi sita (kama basi dogo la abiria-coaster) limeundwa kwa kuunganisha vipuri na kuwekewa njia ya umeme, likiwa na jiko ndani yake na eneo maalumu la kupakulia chakula na kukihifadhi katika joto bila kupoa.

Kwa mujibu wa Loius, kupitia utafiti alioufanya amefahamu kuwa katika nchi za Ulaya, ukiagiza aina hiyo ya gari mpaka kufika nchini ni zaidi ya Sh milioni 24, lakini yeye analiuza kwa Sh 10,980,000. “Nikiwa kijana mdogo nilikuwa napata hasira sana kuona wazungu wanafanya mambo mengi na sisi tunashindwa, nikaanza kuunda vitu wazazi wakawa wanashangaa, baadae nikaamua kuja kutafuta fursa za maisha Dar es Salaam,” anasema Louis.

Anasema lengo la gari hilo ni kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli za kutafuta suluhu ya baadhi ya changamoto kwa wananchi wa kawaida na yeye amelenga mamalishe na babalishe.

“Mamalishe akipata gari hili anakopesheka hata benki na kukuza mtaji wake. Mimi naangalia jamii ina uhitaji gani natengeneza kitu kutokana na uhitaji huo,” anasema mbunifu huyo aliyeliweka gari hilo katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere. Anasema ana uwezo wa kutengeneza mashine na vitu vingi, lakini tatizo ni mtaji na ugumu wa kupata vibali vya vitu hivyo kama ilivyokuwa kwa gari ambalo sasa anadai ameligeuza chuma chakavu na kuuza kifaa kimoja baada ya kingine baada ya kuona hapati kibali.

Louis anasema amegundua jamii ya watu wenye ulemavu imesahaulika na sasa, anatengeneza baiskeli ya magurudumu matatu itakayokuwa ya kuchaji kwenye umeme kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa miguu na wazee. “Hii baiskeli hatatumia mafuta ya petroli wala dizeli, itakuwa ya kuchaji kwenye umeme au kutumia mikono kama umeme ukikatika au baiskeli ikiwa haijachajiwa,” anasema mbunifu huyo mkazi wa Majohe, Pugu, Dar es Salaam. Anasema anatamani wanyonge na wahitaji katika nchi hii wasiachwe nyuma katika kila kitu, bali wawekwe mbele kwani wanao uwezo wa kipekee wa kufanya mambo makubwa yanayoweza kuleta mapinduzi ya kiuchumi kama watu wengine.

Louis anasema baiskeli hiyo anayoitengeneza itamwezesha mtu mwenye ulemavu kwenda popote katika mji anaoishi, kununua mahitaji, kushiriki semina za kiimani, kwenda msikitini na kanisani. Anasema baiskeli hiyo itawanufaisha pia watu wazima, wastaafu na wazee kuondokana na kero ya usafiri hasa katika miji na majiji kwenye msongamano na vurugu za usafiri kama Dar es Salaam.

Changamoto ya usafiri wa daladala na mwendokasi kwa Jiji la Dar es Salaam imekuwa kero kwa wazee na watu wenye ulemavu hasa asubuhi na jioni na kusababisha wengi wao wanaokuwa wanakwenda hospitali kukwama au kuchelewa na kusababisha madhara ya kiafya zaidi kwao. Louis anasema suluhisho la suala hilo ni baiskeli hiyo, itakayoweza kuendeshwa bila kero, ikiwa na magurudumu matatu na nafasi ya kubeba watu wengine kadhaa wasaidizi wa muhusika.

Mbunifu Louis anasema amefanya utafiti na kugundua kuwa baiskeli kama hiyo inayoendeshwa kwa mikono na watu wenye ulemavu inauzwa kwa Sh milioni 1.5 na kwa kuwa nia yake ni kusaidia jamii, ataiuza kwa bei hiyo hiyo ingawa inaweza kutumika kwa namna mbili; umeme na mikono.

Anasema ameshaanza kuiunda baiskeli hiyo na anatarajia itakamilika Septemba mwaka huu na anapokea oda kuanzia sasa kwa wenye kuhitaji baiskeli hiyo. Changamoto kubwa kwa Louis ni mtaji, lakini anaziomba mamlaka zinazotoa vibali na kuthibitisha vifaa na mashine zinazotengenezwa na Watanzania, kuondoa vikwazo na urasimu uliopitiliza ili kuiweka nchi katika sura ya kimataifa kupitia wabunifu wa ndani.

Anasema kuelekea uchumi wa kati mwaka 2025 kupitia viwanda, wabunifu wa ndani kama yeye wanapaswa kuungwa mkono, kupewa miongozo ya nini cha kufanya na hatua gani za kuchukua ili kuboresha kazi zao kuliko kuwazuia au kuwanyima vibali. Aidha, anatamani pia kodi kwa wabunifu wa ndani ziangaliwe upya, tozo na vizuizi visivyo na tija viondolewe ili kutoa fursa kwa wabunifu wengi zaidi kujitokeza na kuleta mabadiliko chanya kwa Taifa.

Mkazi wa Pugu, Dar es Salaam aliyejitambulisha kwa jina la Rashid Kanole katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam, alipotembelea gari hilo alisema ameguswa sana na ustadi wa Louis kwa kuwa amekuwa mgunduzi wa vitu vingi lakini pia gari hilo la chakula lililo rafiki wa mazingira na msaada mkubwa kwa mama lishe.

“Watu kama hawa wanapaswa kuwezeshwa, Serikali kama ilivyofanya kwa wazalishaji wa umeme wa Iringa na Mbeya, waangalie na hawa, wasisubiri Rais aseme, wachukue hatua, mpaka lini tutategemea wazungu kiteknolojia wakati tuna watu wanaweza?” alihoji Kanole.

Juni 13, mwaka huu, Rais Magufuli alikutana na wabunifu wa umeme wa mkoani Njombe, walioibuliwa na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC- Taifa) kupitia kipindi cha Darubini, John Mwafute na Jairos Ngailo, pamoja na mambo mengine, aliwataka mawaziri na watendaji kutekeleza majukumu yao kwa kufuatilia wabunifu kama hao badala ya kusubiri yeye afanye.

AWAMU ya Kwanza ya Serikali ya Tanzania iliyoongozwa na Mwalimu ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi