loader
Picha

Tari inavyopania kupunguza uagizaji mafuta ya kula nchini

UKIENDA Bandari ya Dar es Salaam katika kitengo cha mafuta cha Kurasini (KOJ), utagundua kwamba mafuta mengi ya kula yanayopitia katika kituo hicho yanatoka nje ya nchi. Hii maana yake ni kwamba, Tanzania haijitoshelezi kwa mafuta ya kula hivyo kulazimika kutumia pesa nyingi za kigeni kuagiza mafuta hayo nje ya nchi.

Msimamizi wa KOJ, Kapteni Sixtus Karia, anasema hajawahi kuona bidhaa ya mafuta ya kula kutoka nchini kwenda nje isipokuwa tunapokea tu mafuta kila uchwapo. Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Ilonga (Tari Ilonga), wilayani Kilosa, mkoani Morogoro, inasema mahitaji ya mafuta ya kula nchini yanaongezeka mwaka hadi mwaka.

Mratibu wa Utafiti wa zao la alizeti nchini kutoka TARI Ilonga, Frank Reuben, anasema Tanzania huzalisha asilimia 40 tu ya mafuta ya kula huku asilimia 60 iliyobaki ikitazamiwa kuagizwa kutoka nje ya nchi.

Anasema mafuta yanayoagizwa nje ya nchi hugharimu kati ya Sh bilioni 400 (takribani Dola za Marekani 174,109,860) mpaka Sh bilioni 675 (Dola za Marekani 293,810,388) kila mwaka. “Uagizwaji huu mkubwa wa mafuta kutoka nje unafanyika wakati nchi ikiwa na uwezo wa kuzalisha mazao mengi kwa ajili ya mafuta ya kula yakiwamo ya alizeti, chikichi, pamba na soya,” anasema.

Anasema serikali imeweka mkakati wa kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula nchini kupitia kilimo cha alizeti na chikichi. Tari kupitia kituo chake cha Ilonga, Kilosa inaratibu utafiti wa alizeti huku kituo cha Kihinga kilichoko Kigoma kikiratibu utafiti wa zao la chikichi. “Kwa sasa, kiasi cha mafuta kinachozalishwa nchini, alizeti huchangia asilimia 70 na mazao mengine huchangia asilimia 30.

Mazao hayo ni pamoja na chikichi, pamba, ufuta na karanga. Hivyo ni muhimu sana kuwekeza kwenye alizeti inayoweza kulimwa na kuzalishwa kila mwaka kwa muda mfupi,” anasema. Anasema katika maeneo mengine nchini, alizeti huzalishwa mara mbili kwa mwaka na mbegu zilizosajiliwa na kusambazwa kwa ajili ya uzalishaji wa mafuta ya alizeti ni aina ya Record.

Anasema mbegu hii huchukua asilimia 85 ya soko kutokana na mfumo wake wa uzalishaji. Anasema kwa muda mrefu upatikanaji wa mbegu za alizeti kwa wakulima umekuwa hafifu hivyo Wizara ya Kilimo kupitia Tari, imeweka mkakati kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora kwa mkulima kwa kuandaa malengo mkakati sita.

Anataja malengo hayo kuwa ni kuwezesha upatikanaji wa mbegu bora za alizeti, kujenga uwezo wa maofisa ugani na wakulima ili kuwa na uzalishaji endelevu na kuhamasisha matumizi ya mbegu bora za alizeti kwa wakulima. Malengo mengine anasema ni kutafiti na kueneza matumizi ya kanuni bora za kilimo cha alizeti, kufanya utafiti unaolenga ugunduzi wa mbegu bora za alizeti, kutafiti masoko, matumizi ya uhifadhi wa alizeti baada ya mavuno pamoja na usindikaji.

Anasema ili kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora za alizeti nchini, Reuben anasema Kituo cha Ilonga kimepanda ekari 83 za uzalishaji wa mbegu za alizeti. Anasema kati ya hizo, ekari 20 ni kwa ajili ya mbegu za awali na ekari 63 ni kwa ajili ya mbegu zilizothibitishwa ubora. “Tari inategemea kuzalisha maradufu mbegu za alizeti kwa msimu ujao. Hii ni hatua kubwa maana kabla ya kuanzishwa kwa Tari mwaka mmoja uliopita, jumla ya ekari mbili zilikuwa zinalimwa kwa mwaka.

“Sasa mbegu ya awali itasambazwa kwa Wakala wa Mbegu (ASA), kampuni za wazawa wazalendo zinazosambaza mbegu hii na zilizothibitishwa ubora zitapelekwa moja kwa moja kwa wakulima,” anasema. Anasema mbegu aina ya Record hustawi maeneo mengi ya Tanzania yakiwamo yaliyo kwenye mwinuko wa mita 2,000 kutoka usawa wa bahari. Mbegu hiyo anasema, hustahimili ukame na ina ukinzani dhidi ya magonjwa na wadudu.

Kwa ekari moja, mbegu ya Record hutoa mafuta kati ya lita 220 hadi 250. Mkurugenzi wa Kituo cha Tari-Ilonga, Dk Joel Meliyo, anasema uzalishaji wa mbegu bora za mazao ya mafuta hasa alizeti ni mojawapo ya majukumu ya kitaifa ya kituo hicho. Anasema ekari hizo 63 zilizopandwa mbegu zilizothibitishwa, kila ekari inatoa wastani wa kilo 600 za mbegu, hivyo wanatarajia kuzalisha tani 37.8 za mbegu.

“Kwa kila ekari moja, mbegu zinazotosha ni kilo mbili hivyo kwa tani 37.8 zitaweza kupandwa katika ekari 19,000. Ukivuna vizuri kwa mwaka unapata kilo milioni 11.4. “Mafuta katika kila mbegu ya mafuta ni asilimia 40, na asilimia 60 iliyobakia ni mashudu. Hivyo ukiwa na kilo milioni 11.4 unatarajia kupata mafuta kilo milioni nne au tani 4,560 za mafuta. Huo ni mchango mkubwa wa mafuta nchini,” anasema. Anasema Tari Ilonga imejipanga kuona katika kipindi cha miaka mitano, nchi inapunguza uagizwaji wa mafuta kutoka nje ya nchi angalau kwa nusu.

Anasema wanapanga kuzalisha mbegu kwa wingi ili kuhakikisha tani zote zinazotakiwa nchini kwa ajili ya wakulima alizeti zinapatikana. Ni kwa mantiki hiyo anasema wanatakiwa kupanda ekari laki nane ili nchi ijitosheleze kwa mafuta. Mkurugenzi Mkuu wa Tari Taifa, Dk Geoffrey Mkamilo, anasema kila kituo cha utafiti wamekubaliana kuwe na mazao ya mkakati na hivyo kupitia Tari Ilonga watahakikisha.

Akifungua Maonesho ya Kilimo Biashara yaliyoandaliwa na Tari pamoja na Baraza la Nafaka la Ukanda wa Afrika Mashariki (EAGC), Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba anasema kilimo ni sekta muhimu katika maendeleo ya uchumi wa wananchi na taifa.

Anasema kilimo kina mchango mkubwa katika kuisukuma nchi kuelekea uchumi wa kati unaotegemea viwanda akifafanua kwamba zaidi ya asilimia 65 ya mali ghafi viwandani inatazamiwa kutoka kwenye kilimo. Anasema kwa takwimu zilizopo kilimo kinachangia asilimia 28.7 kwenye pato la taifa huku kikiajiri takribani asilimia 65.5 ya Watanzania. Hata hivyo anasema, Tari inapambana kuona kilimo kinachangia pakubwa zaidi katika pato la taifa kuliko ilivyo sasa.

WAKAZI 1,639 wa vijiji vya Matongo na Nyabichune katika eneo ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

1 Comments

  • avatar
    Beatus wenga
    16/01/2020

    Nashukuru sana kupata Elimu hii ya uzalishaji wa alizeti hapa nchini, mimi ni mkulima wa mpunga kutoka Mbarali kwa mwaka huu nimeguswa sana na kilimo cha alizeti pamoja na mahindi hasa kwa mbegu hizi za kitalaam na kwa mwaka huu ninalima Dodoma.Nimepitia makala mbalimbali za kitaalam kutoka kwa waandishi tofauti nashukuru nimepata mwanga wa kutosha na naweza kuwashauri baadhi ya wakulima. Nilichogundua ni kwamba watanzania wenzangu wengi wetu hatuwatumii watalaam wetu,na kubaki kulima kwa matumizi ya nyumbani tu.Ningependa kupata mtalaam mmoja wa kilimo ili aweze kunikwamua hasa kwa ushauri, (0715709673)

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi