loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wasichana wang'ara kidato cha 6

BARAZA la Mitihani la Taifa (NECTA) limetangaza matokeo ya mitihani kwa wanafunzi wa kidato cha sita, waliofanya mitihani hiyo Mei mwaka huu ambayo yanaonesha asilimia 96 wanafunzi waliofanya mitihani hiyo, wamefaulu na kiwango cha ufaulu kikiongezeka kwa asilimia 0.74.

Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk Charles Msonde alitangaza matokeo hayo mbele ya waandishi wa habari katika ukumbi wa Wizara ya Elimu ya Zanzibar.

Amesema watahiniwa wa shule waliofaulu ni 78,666 sawa na asilimia 99.14 ya waliofanya mitihani.

Amesema ukiangalia ubora wa madaraja waliyopata watahiniwa wa shule, utabaini kuwa watahiniwa 76,655 sawa na asilimia 96.61 walifaulu katika daraja la kwanza hadi la tatu, wakiwemo wasichana 32,887 sawa na asilimia 97.22 na wavulana 43,768 sawa na asilimia 96.15.

Shule 10 bora kitaifa Dk Msonde alitaja shule 10 bora kitaifa, majina ya shule na mikoa kwenye mabano kuwa ni Kisimiri (Arusha), Feza Boys (Dar es Salaam) , Ahmes (Pwani), Mwandet (Arusha), Tabora Boys (Tabora), Kibaha (Pwani), Feza Girls (Dar), St.Mary’s Mazinde Juu (Tanga), Canossa (Dar) na Kemebos (Kagera).

Shule 10 za mwisho

Alitaja shule 10 za mwisho katika matokeo hayo, majina ya shule na mikoa kwenye mabanokuwa ni: Nyamunga(Mara), Haile Sellasie (Mjini Magharibi), Tumekuja (Mjini Magharibi), Bumangi(Mara), Buturi(Mara), Mpendae (Mjini Magharibi), Eckernforde(Tanga), Nsimbo(Katavi), Mondo(Dodoma) na Kiembesamaki Islamic (Mjini Magharibi).

Hata hivyo, Dk Msonde alifafanua kwamba shule 10 za mwisho, hakuna mwanafunzi aliyefeli katika matokeo hayo kwani wanafunzi wamepata daraja la kwanza hadi la tatu.

Alitoa mfano wa shule ya Kiembesamaki Islamic ya Zanzibar, ambayo jumla ya wanafunzi 85 walifanya mitihani yao, ambapo wote wamefaulu kwa kupata daraja la kwanza hadi ya tatu na hakuna aliyepata daraja la sifuri.

Matokeo hayo yanaonesha kwamba wasichana wanaongoza kwa kufanya vizuri katika masomo ya Sayansi kitaifa, huku Faith Matee kutoka Shule ya St.Mary’s Mazinde Juu kutoka Tanga akishika nafasi ya kwanza na kufuatiwa na Levina Chami kutoka Shule ya St.Mary’s Goreti ya Kilimanjaro.

Wanafunzi 10 bora sayansi

Alitaja wanafunzi 10 bora wa masomo ya sayansi, majina na shule zao katika mabano kuwa ni: Faith Matee (St Mary’s Mazinde Juu), Herman Kamugisha (Kisimiri), Levina Chami(St Mary Goleti), Benus Eustace (Mzumbe), Augustino Omari(Ilboru), Satrumin Shirima (Temeke), Khalid Abdallah (Feza Boys), Assad Msangi (Feza Boys), Peter Riima(Kibaha) na Augustine Kamba (Feza Boys).

Mapema, Dk Msonde alipongeza kamati za shule kwa usimamizi mzuri wa maandalizi ya mitihani ya kidato cha sita pamoja na walimu, kwa kuwawezesha wanafunzi kufaulu kiwango kizuri.

Alisema tathmini ya awali ya matokeo hayo, inaonesha kwamba mtihani wa kidato cha sita, ufaulu umepanda kidogo kwa asilimia 0.74, ambapo mwaka 2018 ufaulu ulikuwa asilimia 97.58 na mwaka huu ni 98.32.

Alisema ubora wa ufaulu kwa wanawake, umezidi kuimarika na kuwazidi wanaume kwa asilimia 1.07 ikiwemo katika masomo ya sayansi kitaifa.

Alisema Baraza la Mitihani la Taifa limezuia kutoa matokeo ya wanafunzi wa shule 20, ambao walipata matatizo mbalimbali ya kiafya na kushindwa kufanya mitihani hiyo. 14 wafutiwa matokeo Pia, alisema Baraza hilo limefuta matokeo ya watahiniwa 14, waliobainika kufanya udanganyifu, wakiwemo wanafunzi tisa wa shule.

‘’Hawa wanafunzi waliofanya udanganyifu ni wao wenyewe ambao wapo waliokutwa na ‘’mabomu’’ ya karatasi za majibu na wengine kuingia katika vyumba vya mitihani na simu kwa ajili ya kutafuta taarifa zaidi,’’ alisema.

Jumla ya watahiniwa 91,298 walisajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha sita Mei 20, mwaka huu, wakiwemo watahiniwa wa kujitegemea 11,082.

Kati ya watahiniwa 91,298 waliosajiliwa kufanya mitihani hiyo kidato cha sita, watahiniwa 90,001 sawa na asilimia 98.58 waliofanya mitihani na watahiniwa 1,297 sawa na asilimia 1.42 hawakufanya kwa sababu mbali mbali, ikiwemo ugonjwa na wengine utoro.

Baraza la Mitihani la Taifa pia limetoa matokeo ya mtihani wa Ualimu daraja la A GATCE, ambapo waliosajiliwa kufanya mtihani huo walikuwa ni 4,846,wakiwemo wasichana 2,102,pamoja na Wavulana 2,744 sawa na asilimia 56.62.

Mwanafunzi hodari alonga Wakati huo huo, John Mhala kutoka Arusha anaripoti kuwa mwanafunzi Herman Kamugisha (20) wa Shule ya Sekondari ya Kisimiri iliyopowilayani Arumeru mkoani Arusha, ambaye amepata Daraja la Kwanza, ameshika nafasi ya pili kitaifa kwa wanafunzi bora wa masomo ya Sayansi, ambapo amesema malengo yake ni kuwa mhandisi wa ndege.

Akizungumza na gazeti hili, Kamugisha alisema kuwa kufanya kwake vizuri na hatimaye kuongoza, haikuwa malengo yake, bali hali hiyo imetokana na mazingira aliyoyakuta ya walimu wa Kisimiri ya kuhimiza wanafunzi kusoma, ndiko yalikomfikisha hapo na yeye kufanya vyema katika somo hilo.

Kamugisha ambaye alisema kuwa hajawahi kumwona baba yake mzazi tangu akiwa na umri wa miaka 12, kwa sasa anaishi Kihonda mkoani Morogoro kwa rafiki ya baba yake.

Alieleza kuwa matarajio ya kuwa mhandisi wa ndege, yanatokana na kuvutiwa na jitihada za Rais John Magufuli za kufufua Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL).

‘’Tunapaswa kujivunia kuwa na ndege zetu na pia tunapaswa kujivunia kwa kuwa na wahandisi wa ndege wa hapa nchini. Mimi ni lazima niwe mhandisi ikiwa ni njia mojawapo ya kumuunga mkono Rais wangu,’’ alisema Kamugisha.

Kamugisha alisema kuwa hakutarajia kufanya vyema katika somo hilo, bali mazingira aliyoyakuta ya kuhimizwa kusoma mara kwa mara kutoka kwa walimu wa shule hiyo, ndiko kulikomfanya yeye kufaulu.

Aliwashukuru pia walimu wake kwa kumfuatilia na kumfundisha ipasavyo ambapo pamoja na kwamba yeye aliona ni adhabu kwake, lakini amepata matokeo mazuri.

Kamugisha alisema kuwa mama yake mzazi, Alphonsia Pius ambaye yuko mkoani Shinyanga kwa sasa, hana taarifa za yeye kufanya vyema katika masomo kwani yuko katika mazingira magumu na hataweza kupata taarifa.

Lakini, alisema atafanya kila jitihada za kuhakikisha anapata taarifa hizo. Alisema kuwa anamshukuru sana Mungu na baba yake mlezi, rafiki wa baba yake, kwa kumlea na hatimaye kufanya vyema katika masomo.

Mkuu wa Shule ya Kisimiri, Valentine Tarimo alishukuru shule yake kuongoza kitaifa.

Alisema kuwa hiyo imetokana na ushirikiano uliopo kati ya walimu na wanafunzi wa shule hiyo.

Tarimo alisema wamerudi katika nafasi yao ya kuongoza kitaifa katika masomo ya jumla, baada ya kupotea katika nafasi hiyo mwaka 2017/18, lakini miaka mingine yote ya nyuma walikuwa wakiongoza kitaifa.

KAMPUNI ya uzalishaji wa vifaa mbalimbali vya umeme cha Kilimanjaro ...

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman, Zanzibar

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi