loader
Picha

Majeruhi Azam Media wasubiri upasuaji

MMOJA kati ya majeruhi ambaye ni mfanyakazi wa Azam Media ya Dar es Salaam, Mohamed Mainde amesema ajali waliyoipata mkoani Singida wakati wakienda Chato, ni moja kati ya mitihani ambayo Mwenyezi Mungu, humpa kila mwanadamu kwa wakati wake.

Mainde ameyasema hayo jana akiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) wakati Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Manyanya alipokwenda kuwapa pole wafanyakazi hao wawili, kati ya watatu waliolazwa Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) jijini Arusha.

Mainde alimshukuru Manyanya kwenda kuwajulia hali na kusisitiza ajali ile ni mtihani ambao Mwenyezi Mungu humpa mwanadamu kwa wakati wake na muda husika.

“Nashukuru kwa kuja kutuona, huu ndio moyo wa upendo uliotuonesha, tumepata mtihani na leo tupo hapa na tunawashukuru madaktari kwa kutuhudumia na leo hii najisikia nafuu,” alisema.

Mfanyakazi mwingine wa Azam Tv, Artus Masawe alishukuru kujuliwa hali na Naibu Waziri huyo. Alisema anajisikia nafuu baada ya kufanyiwa upasuaji wa mdomo na miguu.

Manyanya alisema tukio hilo la ajali lilipotokea, alishtuka sababu waliokufa na hao majeruhi ni watu waliojituma katika kufanya kazi bila hata kujali hadhi ya mtu.

Alisisitiza kujitoa kwao katika kazi, kuliwafanya watambulike maeneo mbalimbali. Alisema anashukuru Mungu kuwaona leo hii, wakiwa wanajitambua na wanajua wanaongea na nani.

“Nawapa pole sana na nimewapa mkono wa pole ambao utawasaidia kugharamia vitu vidogo vidogo wakiwa hapa hospitalini, nawashukuru sana madaktari kwa kutoa huduma kwa wagonjwa hawa na wagonjwa wengine, hakika Mungu ni mwema,” alisema.

Mmoja kati ya madaktari aliyewafanyia upasuaji wafanyakazi hao, Dk Peter Makanza alisema Mainde amefanyiwa upasuaji mara tatu, bado operesheni mbili katika maeneo ya miguu. Jana walianza kuwafanyia mazoezi madogo wakati wiki mbili zijazo watafanyiwa upasuaji mwingine mara mbili tena.

Massawe akiendelea vyema baada ya kufanyiwa upasuaji miguuni pamoja na mdomo wake, mtaalamu wa kinywa na meno ataanza naye mazoezi ya kinywa.

Massawe anaendelea vizuri na anaongea. Juzi hospitali hiyo ilipokea majeruhi hao wawili, waliokuwa na hali mbaya. Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura, Dk Richard Mabula alisema kuwa hospitali hiyo imepokea majeruhi wawili, kati ya watatu, ambao ni wafanyazi wa Azam Media Limited.

Alisema juzi walipigiwa simu na kampuni ya ndege ya Arusha Medivac Ltd, kwa lengo la kwenda mkoani Singida katika hospitali ya wilaya, kusaidia uokoaji wa majeruhi hao watatu.

Alisema walipofika majira ya mchana Singida, waliambiwa majeruhi hao wamehamishiwa Hospitali ya Nkinga, ambapo baada ya kufika hapo, waliwachukua wakiwa katika hali mbaya, huku mmoja akiendelea kutibiwa hospitali hapo.

Alisema baada ya kuwachukua majeruhi hao, Artus Masawe (Injinia)na Mohamed Mainde (Injinia) walishauriana wawapeleke Hospitali ya Bugando Mwanza, Dar es Salaam au Arusha.

Alisema lakini rubani wa ndege hiyo(hakumtaja jina) aliona wakienda Bugando watachukua saa tatu angani na wakienda Dar es Salaam watachukua saa mbili angani ila wakija Jijini Arusha watachukua saa moja angani.

“Baada ya rubani kushauri haya tuliondoka Singida na wagonjwa hawa wawili ambao hali zao hazikuwa nzuri kisha tulitua uwanja mdogo wa Arusha saa 18:45 jioni na kuwaleta hospitalini hapa kwa ajili ya matibabu zaidi,” alieleza.

Wakati huohuo, madereva wawili waliopoteza maisha kwenye ajali iliyosababisha vifo vya wafanyakazi watano wa Azam Media, wamezikwa jana mkoani Morogoro na Tanga.

Akizungumza na gazeti hili jana katika kituo cha kuegesha mabasi ya kusafirishia abiria kuelekea mikoani, Mabibo NIT mahala ambapo madereva hao wawili walikuwa wakifanyia shughuli zao, Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva wa Ubungo NIT, Shomary Yatima alibainisha kuwa umoja huo umefanikisha maziko ya madereva hao salama katika vijiji walivyotokea kwenye mikoa yao. Alisema Ubungo NIT imekuwa ikifanya kazi na Azam Media tangu kuanzishwa kwa kampuni hiyo.

Alibainisha kuwa madereva waliokufa kwenye ajali hiyo, ndio walikuwa wakiwaendesha wafanyakazi wa Azam kwa miaka yote, kila wanapohitaji usafiri kuelekea mikoani.

Alisema, kila wafanyakazi wa kampuni hiyo, wakitaka kuelekea maeneo mbalimbali kuonesha mipira au katika shughuli nyingine za kijamii, kisiasa hukodisha Coaster iliyokuwa zikiendeshwa na madereva wawili.

Alibainisha kuwa miili mitatu, kati ya hao saba waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo ya juzi, imesafirishwa kuelekea mkoani Kagera, Iringa na Tanga kwa kutumia usafiri kutokea hapo Ubungo NIT.

Alisema kabla ya safari ya wafanyakazi wa Azam Tv, madereva hao walikuwa kijiweni hapo kwa takribani wiki moja bila ya kusafiri kwenda kokote hadi safari ya Azam ilipowafikia kama kawaida.

Jumatatu iliyopita katika eneo la Shelui mkoani Singida gari aina ya Coaster likitokea Dar es Salaam, likiendeshwa na madereva hao wawili kwa kupokezana, liligongana uso kwa uso na lori lililokuwa likitokea mkoani Mwanza.

Wafanyakazi hao watano wa Azam TV waliokufa papo hapo kwenye ajali hiyo na tayari wameshazikwa ni Salim Mhando (Muongozaji wa Matangazo), Florence Ndibalema (Mhandisi wa Sauti), Sylvanus Kasongo (Mhandisi Mitambo) na wapiga picha wawili Said Haji na Charles Wandwi. Majeruhi watatu waliopona kwenye ajali hiyo, Artus Masawe, Mohammed Mwinshehe na Mohammed Mainde. Madereva waliokufa ni Omary Mhina na Juma Khatibu.

Mhina alizikwa jana mkoani Morogoro na Khatibu alizikwa Handeni Tanga jana hiyo hiyo pia. Habari hii imeandikwa na Veronica Mheta, Arusha na Evance Ng’ingo, Dar.

Rais John Magufuli amemuagiza Naibu Mkurugenzi Mkuu wa ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi