loader
Picha

Meneja atuhumiwa kuiba dhahabu ya mil 500/-

MENEJA wa Maabara wa Tume ya Madini, Dornald Joseph Njonjo (30) anashikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa tuhuma za kuiba madini ya dhahabu kilogramu 6.244 yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 507, yaliyokuwa yamehifadhiwa kwenye Kasiki ya Ofisi za Wakala wa Madini, Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Kamanda wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kunatokana na taarifa ambazo jeshi hilo lilizipata Juni 29, Mwaka huu kutoka kwa Ally Sadick (40) ambaye ni Ofisa Madini Mkoa wa Dar es Salaam baada ya kugundua kuibiwa madini hayo.

Amesema baada ya Polisi kupata taarifa hizo ilianza uchunguzi mara moja na kubaini kuwa madini hayo yaliibiwa na mtuhumiwa huyo kuanzia Desemba, mwaka jana hadi ilipokuja kubainika hivi karibuni.

“Baada ya mtuhumiwa kuhojiwa alikiri kuiba madini hayo kidogo ambayo yalikuwa yamehifadhiwa kwenye chumba katika jengo la ofisi za tume ya madini zilizopo Masaki na kueleza kuwa alikuwa akiyauza katika duka la kuuzia vito vya dhahabu,” alisema Mambosasa.

Aidha, alisema mtuhumiwa huyo pamoja na kufanya wizi huo, pia alibuni mbinu nyingine ya kuhifadhi madini bandia yenye uzito wa kilo 6.001 nyuma ya jengo la tume ya madini ili kuyapeleka katika chumba walichoiba madini hayo halisi ili kuyabadilisha na yaliyoibiwa kwa lengo la kupoteza ushahidi.

Alisema madini hayo halisi ya dhahabu yalikamatwa mwaka 2017 huko maeneo ya bandarini Zanzibar yakiwa yanasafirishwa kinyume cha sheria kisha kuitafishwa na serikali na kuhifadhiwa katika ofisi hizo za tume ya madini.

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linakamilisha utaratibu wa kupeleka jalada kwa Mwendesha Mashtaka wa Serikali ili mtuhumiwa aweze kufikishwa mahakamani.

Aidha, katika hatua nyingine jeshi hilo linawashikilia watu saba kwa tuhuma za wizi wa bajaji mbili, fedha pamoja na bidhaa mbalimbali walioufanya katika maeneo ya Ukonga.

Watuhumiwa wanaoshikiliwa ni pamoja na Said Salum (27), Amo Kefas (30), Said Ahmad (38), Mohamed Musa (31), Mboke Samwel (26), Abdallah Kipaneli (25) na Mfaume Mussa (25).

Alisema watuhumiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo saa nne usiku wa Julai 9 mwaka huu katika maeneo ya Kibeberu na Magole, Ukonga baada ya kuvunja maduka matatu na kufanikiwa kuiba mali hizo.

Amezitaja bajaji hizo na namba zake za usajili kuwa ni MC 312 CFB na MC 540 CED zote zikiwa aina ya TVS zenye na rangi ya bluu na kwamba taarifa za wizi huo zilipokelewa katika kituo cha Polisi Stakishari na upelelezi ulianza mara moja ambapo siku hiyo hiyo saa 5 asubuhi watuhumiwa waliweza kukamatwa huko maeneo ya Hondogo Gogoni Kiluvya wilaya ya Ubungo.

Aidha watuhumiwa hawa wamekuwa wakifanya matukio ya uhalifu kwa kutumia gari aina ya Toyota Harrier nyeusi yenye namba T.666 DJG ambayo inashikiliwa na Jeshi la Polisi ili kubaini mmiliki wake na kudai kuwa wote watafikishwa mahakamani hivi karibuni.

Rais John Magufuli amemuagiza Naibu Mkurugenzi Mkuu wa ...

foto
Mwandishi: Oscar Job

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi