loader
Picha

Barabara Dodoma kuongeza watalii Ruaha

MKOA wa Dodoma unaweka mkakati wa kuvutia watalii kutembelea mbuga ya Ruaha kupitia njia ya mkato ya kuingia kwa kupandisha hadhi barabara ya Mpunguzi hadi Ilangali kilometa 95, badala ya kuzunguka njia ndefu ya Mtera, Iringa hadi Ruaha.

Akizungumza katika mikutano miwili ya hadhara miwili katika kijiji cha Ilangali na Manda vilivyopo katika kata ya Manda wilayani Chamwino, Mkuu wa Mkoa, Dk Binilith Mahenge alimtaka Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) wilayani Chamwino, Makandi Mange kuipa kipaumbele barabara hiyo wakati akitenga fedha za kuboresha barabara.

Dk Mahenge alimuagiza Mange kupanga bajeti ya kutengeneza barabara kwa kiwango cha changarawe kwa lengo la kuwapa unafuu watalii kutoka Dodoma kutembelea hifadhi hiyo lakini pia kupata mapato ya halmashauri hiyo.

Alitoa maelekezo hayo na kumtaka Mange kuleta mapendekezo yake katika kikao cha bodi ya barabara kinachofanyika mwisho wa mwaka kikiwa na mpango wa namna ya kuboresha barabara hiyo.

Maagizo hayo yalitolewa baada ya wananchi wa vijiji viwili kumlalamikia mkuu huyo wa mkioa kwamba barabara hiyo ni mbaya, lakini mkoa ungeweza kuiboresha na kutumiwa na watalii kwa ajili ya kufika kwenye hifadhi na kuiongezea halmashauri mapato.

Mkazi wa Kijiji cha Manda, Michael Semamba aliuliza serikali ina mkakati gani kutengeneza barabara hiyo hadi katika lango la mbuga ya Ruaha ili kupata mapato kutokana na watalii kutembelea hifadhi hiyo.

Cosmas Ulaya wa kijiji cha Manda, alihoji kwamba serikali inaonaje kutengeneza barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe ili kupitika wakati wote kutokana na hali yake mbaya kwa sasa.

Mwananchi Kaneni Mgimwa aliomba kutengeneza barabara hiyo umbali wa kilometa 95 kutoka Mpunguzi hadi Itengule ili kuongezeka magari ya abiria badala ya sasa ambapo ni gari la kampuni moja ndilo linapita huko na kujaza watu kupita kiasi.

Alisema kutokana na ubaya wa barabara hiyo, kumechangia kuwa na basi moja ambalo linajaza abiria kupita kiwango na hivyo kusababisha kufika mjini wakiwa wamechafuka kutokana na kuminyana ndani ya gari.

John Petro alimuomba mkuu wa mkoa kuiboresha barabara hiyo na kuipandisha hadhi ili kutumiwa na watalii kutoka Dodoma kwenda Ruaha badala ya kutumia njia ndefu ya kuzunguka Mtera, Iringa hadi kwenye hifadhi hiyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mkutano wa kijiji cha Ilangali kilichopo umbali wa kilometa 137 kutoka makao makuu ya wilaya, waliomba barabara hiyo muhimu katika usafiri ijengwe kwa kiwango cha changarawe kwa ajili ya kuwasaidia kusafiri na kusafirisha mazao yao.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chamwino, Samwel Kawea alimuomba Dk Mahenge kuwasaidia kuipandisha hadhi barabara hiyo ili itengenezwe kwa kiwango cha changarawe kutokana na umuhimu katika utalii na usafirishaji abiria na mazao.

Akizungumza na Meneja wa Tarura aliahidi kwenda kuandaa bajeti kwa ajili ya barabara, lakini kipaumbele kinatakiwa kuwa barabara hiyo ambayo ina umbali wa kilometa 95 kutoka Mpunguzi hadi Mlangali.

Mkuu wa mkoa aliwataka watendaji wa halmashauri, akiwemo mbunge na viongozi wote kupigania kutengenezwa kwa barabara hiyo na katika mkutano wa bodi ya barabara utakaofanyika mwezi Desemba wanatakiwa kuwa na ajenda hiyo.

WADAU wa utalii wametabiri kuwa Wilaya ya Kisarawe itakua kimapato ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Chamwino

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi