loader
Picha

Hongera wizara kutambua madaktari bingwa

NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile ametangaza mpango wa kuwatambua madaktari wenye uzoefu wa muda mrefu kama mabingwa.

Amesema wamebuni mpango huo kuongeza idadi ya madaktari bingwa walio katika hospitali mbalimbali nchini, hususani za mikoa na wilaya.

Katika mpango huo, wizara imeamua kuandaa utaratibu wa madaktari wenye uwezo mkubwa na uzoefu wa muda mrefu, kufanya mitihani maalumu ya kuthibitisha viwango vyao vya ujuzi.

Alisema, mpango huo utafanana na upimaji ujuzi wa wataalamu wa fani ya uhasibu ambao hufanya mitihani ya shahada za umahiri (CPA).

Tumeguswa na hatua hii ya wizara kuongeza wigo wa madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali nchini kupitia mfumo mbadala.

Kwa muda mrefu, madaktari bingwa wamekuwa wakitokana na wanaoenda kusomea shahada za juu za uzamili (Msc) na uzamivu (PhD) katika umahiri wa fani ambayo wamekuwa wakitibia.

Kutokana na mfumo huo, imekuwa vigumu kupata wataalamu wengi waliobobea wa kuweza kuwa madaktari bingwa kwa kuwa ni wachache wanaopata ufadhili kusomea umahiri wa fani.

Ndio maana tunasema, hatua hii ya wizara kuja na mfumo mbadala wa kuwatambua madaktari wenye uwezo, ujuzi na uzoefu wa muda mrefu lakini hawajaweza kuongeza vyeti darasani ni nzuri na itachochea ufanisi wa madaktari wengi.

Tanzania imejaliwa madaktari wengi wenye uwezo mkubwa kutokana na kupata mafunzo mazuri kwenye vyuo vikuu vya tiba na afya vya Muhimbili (Muhas), Bugando, KCMC na taasisi nyingine za afya zinazotoa mafunzo ya uganga.

Ni katika muktadha huo, tunasema tunaunga mkono hatua hii ya wizara kuwatambua na pia kuwapandisha madaraja na kuboresha maslahi yao, madaktari itakaowatambua kimfumo huu.

Hii itakuwa motisha kubwa kwa madaktari wengi ambao hawajabahatika kuwa mabingwa lakini wamekuwa wakifanya kama za kibingwa.

Ni vyema basi madaktari wenye uwezo, ujuzi na uzoefu huo mkubwa lakini hawajatambuliwa wakajiandaa kufanya mitihani ya umahiri ili nao sasa watambuliwe rasmi pale watakapofaulu.

Hatua hii itasaidia kuongeza idadi ya madaktari wanaotambuliwa kama madaktari bingwa na pia motisha kwa ambao wamekuwa wakitumika bila kutambuliwa hivyo na kuboresha huduma.

Tunaungana na wananchi kuipongeza wizara na serikali kwa jumla kwa kubuni mfumo huu na kutumaini kwamba utapokewa vyema na wote.

Tunaomba madaktari wenye nia, uwezo, ujuzi na uzoefu mkubwa wa kuweza kuwa madaktari bingwa, wajiandae kwa mtihani itakayotolewa.

WAUMINI wa dini ya Kiislamu nchini jana na leo wameungana ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi