loader
Picha

Dk Bashiru amshukia mbunge CCM, awaonya wengine uchaguzi 2020

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally, amemlipua Mbunge wa Same Magharibi, Dk David Mathayo, kuwa amekuwa haonekani katika jimbo hilo na kushindwa kuwahudumia wananchi na kuwaonya wabunge wa chama hicho wenye tabia kama hiyo kuwa majina yao hayatapitishwa kwenye uteuzi wa kuwania tena majimbo hayo uchaguzi mkuu mwakani.

Dk Bashiru ametaja majukumu ambayo mbunge huyo ameshindwa kuyatekeleza ni pamoja na kutofanya ziara, mikutano na kutatua kero za wananchi katika jimbo lake. Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo wa CCM, wakati ukifika wa kuchukua fomu za kugombea ubunge kupitia chama hicho hatasita kumtosa kutokana na kushindwa kuwahudumia ipasavyo wananchi waliomchagua. Dk Bashiru alitoa kauli hiyo jana wakati wa majumuisho ya ziara yake wilayani Same mkoani Kilimanjaro, ambapo alikutana na viongozi wa CCM wa ngazi zote katika mkutano wake wa ndani uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya wilaya ya Same.

Aidha, aliwaonya wabunge wa CCM wasioenda majimboni mwao na kuitisha mikutano ya wananchi na kutatua kero zao kuwa hawatapitishwa tena na chama hicho kuwania nafasi hiyo. “Wakati ukifika tutatandika mkeka ili kuangalia ulifanya mikutano mingapi, ulifanya ziara ngapi, umetatua kero ngapi na umetekeleza kwa kiasi gani ahadi zako ulizoahidi kwa wananchi kwenye jimbo lako katika kipindi cha miaka hiyo mitano, hapa tusije tukalaumiana.”

“Wako Watanzania wengi wanaoweza kufanya kazi hizo za uongozi hivyo ifike wakati mtu asiyekuwa na uwezo, utashi wala kuwa tayari kutumikia umma asipewe tena nafasi yoyote ya kuongoza,” alisema. Dk Bashiru alisema wananchi walitipatia CCM ridhaa ya kuongoza nchi, hivyo haiwezi kukubali kuadhibiwa na umma kutokana na watu wachache wanaolalamikiwa kwa kushindwa kutimiza majukumu yao.

“Serikali inatekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwamo wa maji Same Mwanga Korogwe, lakini wewe hata siku moja kuja kuwaeleza wananchi hawa hujawahi kufanya hivyo, unasubiri hadi tuje sisi ndio tuzungumzie maendeleo katika jimbo lako.” “Hapa natoa maelekezo kwa wabunge wote wanaotokana na CCM, wale waliokabidhiwa dhamana kupitia chama chetu wakizembea hatuwezi tukakubali,” alisema.

Alisema muda umefika wa chama hicho kutowavumilia viongozi mizigo na kuwataka wanaoona wanaweza kuongoza kujipanga na kuhakikisha wana sifa stahili kabla ya kuomba ridhaa ya kuwania kugombea uongozi kupitia chama hicho.

Alisema CCM haiwezi kupima maendeleo ya wananchi kwa kuwapelekea maji, vituo vya afya na lami peke yake kama hawasikilizwi kero zao na malalamiko yao yanapuuzwa. “Tumeshakubaliana kwenye Kamati Kuu na hata kwenye Halmashauri Kuu kuwa viongozi wote wa kuchaguliwa wenye tiketi ya CCM ni lazima wafanye mikutano na ziara kwenye majimbo yao ili kutatua kero za wananchi, hili ni jambo la lazima na sio la hiari tutawafuatilia, tutawakagua,” alisisitiza Dk Bashiru.

Rais John Magufuli amemuagiza Naibu Mkurugenzi Mkuu wa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Same

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi