loader
Picha

Udongo wapimwa afya kuongeza tija

TEKNOLOJIA ya maabara ya kupima afya ya udongo kwa gari maalumu lenye uwezo kupima sampuli 100 za udongo kwa siku imezinduliwa kupima udongo kumhakikishia mkulima uzalishaji mazao kwa wingi na yenye tija sokoni.

Uzinduzi wa teknolojia hiyo kutoka Uholanzi ulifanywa Arusha na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega na Naibu Waziri wa Kilimo na Ubora wa Chakula wa Uholanzi, Marjolijn Sonnema kwa niaba ya nchi yake ili kufanikisha mageuzi katika sekta ya kilimo.

Akizungumza baada ya kufanya uzinduzi wa teknolojia hiyo, Ulega aliishukuru Serikali ya Uholanzi kwa kutoa teknolojia yake nchini kwani italeta mapinduzi katika uzalishaji mazao.

“Kupima afya ya udongo kunatoa majibu juu ya ubora wa ardhi, mazao yanayofaa kulimwa eneo hilo, kiwango cha mbolea kinachotakiwa na pia makadirio ya mavuno,” amesema Waziri Ulega.

Amesema gharama ya kupima shamba ni Sh 25,000 hadi Sh 30,000 ambazo wakulima wanaweza kumudu na kuwataka wapime mashamba yao kabla ya kilimo kuanza ili kujua matatizo yaliyopo kwenye ardhi yake na nini kifanyike ili tija ya uzalishaji iongezeke zaidi.

“Teknolojia hii imeletwa kwetu hivyo tuna kila sababu ya kuhamasisha wakulima kupima mashamba yao ili wajipatie uhakika wa zao linalofaa katika ardhi yake na nini afanye katika kuboresha kuongeza tija ya uzalishaji,” alisema.

Naibu Waziri Ulega alisema mageuzi katika sekta ya kilimo yatapatikana kupitia teknolojia ya kupima afya ya udongo na kusababisha kuongezeka uzalishaji wa mazao ya kilimo hali itakayochochea ujenzi wa viwanda vya kuchakata na kuongeza thamani ya mazao.

“Ushirikiano wa serikali na sekta binafsi unachochea kasi ya maendeleo kwa kuibua teknolojia na ujuzi kuiletea nchi maendeleo, naipongeza kampuni ya Life Support System Tanzania (LSSL) kwa kuwekeza kwenye teknolojia hii,” amesema Naibu Waziri Ulega.

Mkurugenzi Mkuu wa LSSL, Dk Edmond Matafu amesema magari manne yapo tayari na mashine 100 za mkono za kupimia ambazo zitatumiwa na maofisa ugani kuchukua sampuli za udongo katika maeneo ya vijiji kote nchini.

Amesema juhudi za serikali za kujenga uchumi wa kati na viwanda zitatekelezeka nchini kwa ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali ili kuhakikisha vitu vinavyokwamisha maendeleo vinatatuliwa maendeleo yaweze kufikiwa.

“Upimaji afya ya udongo utafanyika kote nchini kwani tumejipanga vizuri kutoa huduma hii kwa wakulima hivyo ushirikiano ndio kitu muhimu kufanikisha suala hili ambalo litaenda kuinua uzalishaji wa zao nchini,” ame  sema Dk Matafu.

Uzinduzi wa maabara hiyo ulishuhudiwa na Naibu Waziri wa Kilimo na Ubora wa Chakula kutoka nchini Uholanzi, Marjolijn Sonnema na pia Balozi wa Uholanzi nchini, Joroen Verheul.

Wengine ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Elisante ole Gabriel na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Methew Mtigumwe na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini, Geoffrey Kirenga.

Rais John Magufuli amemuagiza Naibu Mkurugenzi Mkuu wa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Arusha

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi