loader
Picha

Uhudumiaji meli za mafuta saa 24

Je, ulishajiuliza mafuta haya yanaingia nchini kupitia wapi? Nini kinafanyika katika hatua za awali baada ya mafuta hayo kuingia nchini na hatimaye kufi ka kwenye vituo mbalimbali vya mafuta? Kimsingi, asilimia zaidi ya 90 ya mafuta yote unayoyaona katika vituo vya mafuta nchini pamoja na baadhi ya nchi za jirani, yanapitia katika Bandari ya Dar es Salaam.

Siyo mafuta ya magari na mitambo pekee, bali hata mafuta ya kula yanapitia pia bandarini hapo. Takwimu zilizopo zinaonesha kwamba Tanzania hatujitoshelezi kwa mafuta na hivyo kulazimika kuagiza nje karibu asilimia 60 ya mahitaji yake ya mafuta ya kula.

Kingine kinachopitia katika bandari hiyo ni gesi ya kupikia majumbani ambayo katika kipindi hiki nchi inapojitahidi kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala kwa ajili ya kupikia, kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya gesi ya kupikia majumbani. Katika makala haya, Kaimu Meneja wa Kitengo cha Mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam, maarufu kama Kurasini Oil Jet (KOJ), Kapteni Sixtus Karia, anaeleza mengi yanayofanyika hadi mafuta kumfikia dereva wa bodaboda, basi au gari la mchanga.

Anaanza kwa kueleza kwamba katika bandari ya Dar es Salaam ambayo ndio kubwa kuliko zote nchini wana vituo viwili vya kuhudumia meli zinazoingiza mafuta katika bandari hiyo kwa ajili ya soko la Tanzania au yanayopita kwenda nchi jirani. Anasema kituo cha kwanza ni hicho cha KOJ ambacho kinahudumia meli ndogo za mafuta huku zile kubwa zikihudumiwa na kituo kinachojulikana kama Single Point Mooring (SPM). “KOJ nayo imegawanyika katika maeneo mawili, one na two.

KJO One tunahudumia meli zenye urefu wa mita 183 na KJO Two ni meli zenye urefu wa mita 120,” anasema. Anafafanua kwamba hata vina vya maji vya gati hizo mbili vinapishana, wakati KJO One ina mita 11.5, KJO Two ina kina cha mita saba. Kwa upande wa SPM yenye kina kinachofikia mita 17, Karia anasema wanahudumia meli kubwa zinazofikia mita 265. Karia ambaye pia ni nahodha wa meli kitaaluma, anafafanua kwamba katika kituo cha KOJ wanahudumia zaidi meli zinazokuwa zimebeba gesi ya kupikia majumbani (LPG), dizeli, petroli, mafuta ya kula, mafuta ya ndege, vilainishi (lube oil) na mafut ya taa.

Kwa upande wa SPM anasema wanahudumia mafuta ya aina mbili pekee ambayo ni dizeli na mafuta yasiyosafishwa (crude oil). Akijibu swali kuhusu namna ambavyo mtu anayetaka kuagiza mafuta nje anapaswa kufanya, Karia anasema kwanza anapaswa kuwasiliana na kitengo cha uagizaji wa pamoja kilicho chini ya serikali cha Petroleum Bulk Procurement Agency (PBPA). Akifafanua hatua ya serikali kuja na mpango wa uagizaji wa pamoja (bulk procurement), Karia anasema umesaidia sana kudhibiti bei ya mafuta na ubora kulinganisha na hali ilivyokuwa zamani pale kila mtu alipokuwa akiagiza mafuta kivyake vyake. Anasema hatua hiyo pia imesaidia kupunguza foleni ya meli bandarini kutokana na kuagiza mafuta kwa pamoja.

Akizungumzia taratibu zinazofanyika meli inapofika bandarini anasema zinaanza pale meli inapotoa taarifa ya utayari (notice of readiness) ikimaanisha kwamba imeshatimiza vigezo vyote, ikiwa ni pamoja na malipo ya tozo mbalimbali na hivyo iko tayari kuingia gatini na kushusha shehena.

Anasema kabla ya meli kuanza kushusha mzigo, taasisi mbalimbali za serikali hukagua mzigo husika ikiwa ni pamoja na kuchukua vipimo, kwenda navyo maabara na kujua ubora wake. “Kwa hiyo hata mafuta ya kula yanapimwa na taasisi husika kuhakikisha ubora wake kabla hayajaingia sokoni,” anasema. Anasema ilishawahi kutokea bandarini hapo, meli zikarudishwa na shehena zilizokuwa nayo kutokana na kukosa ubora.

“Meli ya mafuta ikishafika, kwa mfano, kunakuwa na orodha ya wateja ya namna ya kupokea mzigo wao kutokana na mfumo wa uagizaji wa pamoja,” anasema. Kuhusu kiwango cha meli za shehena zinazotia nanga SPM na KOJ kwa mwezi, Karia anasema wanapokea wastani wa meli nne kwa mwezi huku kila moja ikiwa na wastani wa tani laki moja za mafuta.

“Kwa hiyo kwa SPM unaweza kuona tunapokea kati ya tani laki tatu na nusu hadi nne kwa mwezi,” anasema. Kwa upande wa KJO One anasema wanapokea wastani wa meli tano hadi sita kwa mwezi, zote zikiwa na shehena ya wastani wa tani laki mbili. “Kule KJO Two ambako kunafika meli ndogo, mara nyingi tunapokea wastani wa meli tatu hadi nne za gesi ya kupikia kwa mwezi.

Meli zile zinakuwa na wastani wa gesi yenye uzito wa tani 4,000 hadi 5,000 kila moja.” Karia anaona kuna ongezeko la matumizi ya gesi kwa ajili ya kupikia nchini kwani miaka ya nyuma walikuwa wanapata wastani wa meli moja kwa mwezi, lakini sasa zinaingia gatini wastani wa meli tatu hadi nne kwa mwezi zenye wastani wa tani 20,000 za gesi.

Anasema bandari ya Dar es Salaam ina miundombimu yote muhimu ya kupokelea mafuta, lakini haina matangi ya kuhifadhia. “Ipo mipango ya kuwa na matangi yanayomilikiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), lakini kwa sasa mteja anayetaka kuhifadhi mafuta inabidi azungumze na wateja wenye matenki kama vile TIPER ili kumhifadhia,” anasema.

Kuhusu suala la mteja kupata mafuta aliyoagiza mapema anasema linaanzia kwa utayari wa meli baada ya kufika bandarini. Kutegemea ukubwa wa mizigo, anasema wastani wa kushusha mzigo katika meli ni siku nne hadi tano.

TIMU ya Taifa ya Soka ‘Taifa Stars’ inatarajiwa kushuka dimbani ...

foto
Mwandishi: Hamisi Kibari

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi