loader
Picha

Wenye viwanda 73 kuwekeza katika korosho

WAWEKEZAJI 73 wa viwanda kutoka mataifa zaidi ya ishirini, wameungana na wawekezaji wengine kutoka Tanzania, kujadili namna bora ya uwekezaji wa viwanda vya kuongeza thamani katika zao la korosho nchini, ambapo wengi wao wameonesha nia ya kuanza kuwekeza katika sekta hiyo. Wawekezaji hao walikutanishwa mkoani Mtwara jana katika kongamano la siku mbili la uwekezaji la kimataifa la korosho, lililoandaliwa na Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC).

Akizungumza kwenye kongomano hilo, Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba alisema kuwa Tanzania, inakusudia kuwa na uzalishaji mkubwa wa zao la korosho duniani na imeweka mkakati wa kufikia uzalishaji wa tani milioni moja ifikapo mwaka 2023 hadi 2024 kutoka tani 313,000 sasa. Hata hivyo, imejaribu kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji ili waweze kujitokeza kwa wingi na kuweza kufikia malengo ya serikali ya kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

“Kwani lengo ni kuvilinda viwanda vyetu vya ndani kwa ajili ya kutengeza ajira na thamani lakini pia kutangaz jina la Tanzania nje ya mipaka ya Tanzania na ndani ya soko la kimataifa,” alisema Mgumba. Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Geofrey Mwambe alisema serikali imekuwa na matarajio makubwa ya kuwepo kwa ongezeko la uwekezaji nchini katika zao hilo, ambapo wataanzisha viwanda kutokana na mwamko waliokuwa nao washiriki hao, kwani wameweza kutambua fursa za uwekezaji zilizopo katika korosho.

“Matarajio yetu ni kupata wawekezaji wengi sana ambao wanataka kuwekeza katika sekta hii ya korosho kwani mwitikio umekuwa mzuri na washiriki wengi wameweza kushiriki kongomano hili,” alisema Mwambe. Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), Salum Shamte alisema serikali inafanya juhudi za kutoa fursa ya uwekezaji nchini, lakini bado kuna baadhi ya vikwazo na changamoto ambazo zinawakabili wawekezaji hao, ikiwemo uwekaji wa mazingira rafiki ya uwekezaji katika sekta hiyo.

Mshiriki wa kongamano hilo, Mahmoud Sinani alisema kongamano hilo litawezesha wigo mkubwa katika kuendeleza sekta hiyo. Aliipongeza serikali kwa juhudi hiyo ya kuwakutanisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, kwani itawezesha kujenga mahusiano ya karibu baina yao.

RAIS John Magufuli amesema Waziri wa Mambo ya ...

foto
Mwandishi: Sijawa Omary, Mtwara

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi