loader
Picha

Mkurugenzi, mhasibu watupiana tuhuma nzito

MKURUGENZI wa Mamlaka ya Majasafi na Majitaka wilayani Igunga (Iguwasa) mkoani Tabora, Raphael Merumba amemsimamisha kazi kwa muda usiojulikana aliyekuwa mhasibu wa mamlaka hiyo, Boniface James kwa tuhuma ya kula fedha zaidi ya Sh milioni 20, huku wawili hao wakitupiana tuhuma nzito za ubadhirifu wa fedha.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mwishoni mwa wiki, Merumba alisema alibaini upotevu wa fedha hizo baada ya kugundua baadhi ya cheki ambazo mhasibu huyo alikuwa akighushi sahihi ya yake kisha kuchukua fedha kwa nyakati tofauti katika benki ya NMB Igunga. “Ndugu waandishi siwezi kusema sana juu ya suala hili lakini mimi niligundua upotevu wa fedha hizi baada ya kufuatilia kwa karibu baadhi ya cheki ambazo nilibaini kuna sahihi yangu imeghushiwa na mhasibu huyo,” alisema Merumba.

Naye James alipoulizwa juu ya tuhuma hiyo na kusimamishwa kazi, alikiri kusimamishwa kazi na mkurugenzi huyo tangu Juni 13, mwaka huu lakini akikanusha tuhuma ya kula fedha hizo za Iguwasa.

Alisema tuhuma hiyo siyo ya kweli kwani yeye ni msafi na hajawahi kughushi sahihi yoyote, akidai fedha zote zimekuwa zikitoka kwa idhini ya mkurugenzi huyo na sahihi amekuwa akiweka yeye mwenyewe. Aidha, alidai mkurugenzi huyo amekuwa akilazimisha kusaini hundi na kutoa fedha kwa kulipa malipo hewa kwa baadhi ya wazabuni wa kuuza vifaa vya miundombinu ya maji na baadaye anakwenda kuchukua fedha hizo huku wakigawana na wazabuni.

Alidai Mei 23 hadi 25, mwaka huu, mkurugenzi huyo alisaini hundi ya Sh 540,000 kwa ajili ya watumishi wawili kwenda mkoani Iringa kujifunza suala la maji lakini hakuna mtumishi yoyote aliyekwenda na badala yake fedha hizo alizichukua na kuzitumia kwa kulipa faini kwa mtu mmoja aliyemgongea gari yake.

Mhasibu huyo aliendelea kudai kuwa mkurugenzi huyo alikuwa akichukua fedha kwenye mauzo ya magati ya maji likiwamo la Mnadani kwenye manywesheo ya ng’ombe na fedha hizo anazitumia kwa shughuli zake binafsi na kuziomba mamlaka husika kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini mamilioni ya fedha yaliyoliwa na mkurugenzi huyo tangu ahamishiwe Igunga.

Mwenyekiti wa Bodi ya Maji ya Iguwasa, Elly Matto, alithibitisha kupokea taarifa hiyo ya kusimamishwa kazi kwa mhasibu huyo kutoka kwa mkurugenzi wa mamlaka hiyo, huku akisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwani ni tuhuma ambayo ipo kwenye uchunguzi.

RAIS John Magufuli amesema Waziri wa Mambo ya ...

foto
Mwandishi: Lucas Raphael, Tabora

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi