loader
Picha

Pinda alia na sekta ya nyuki

WAZIRI Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda amesema pamoja na umuhimu wa nyuki katika kujikomboa kiuchumi, bado sekta hiyo haijatiliwa mkazo ipasavyo.

Pinda aliyasema hayo jijini hapa wakati wa uzinduzi wa warsha iliyowakutanisha wadau wa ufugaji wa nyuki na wataalamu wa sekta hiyo, kutathmini ya utekelezaji sera ya taifa ya ufugaji wa nyuki ya mwaka 1998, na kufanya mapitio ya sera hiyo.

“Sekta ya nyuki sio ndogo kama wengi tunavyoichukulia, sisi ndio tunaoifanya sekta hii kuwa ndogo lakini ukweli ni kwamba sekta hii ni kubwa sana, tukiamua kuichukulia ‘serious’ itatutoa hapa tulipo,”alisema.

Pinda alisema nyuki ni mdudu mdogo sana lakini ana umuhimu mkubwa kwenye uchavushaji wa mazao nchini ambapo takribani asilimia 70 ya uchavushaji wa mazao hufanywa na mdudu huyo.

“Lakini jambo la kusikitisha ni kwamba sekta hii bado haibebwi inavyotakiwa, sijui niseme ni kutokana na muundo ndani ya wizara ambao umemfanya mdudu huyu asionekane kama ana faida nyingi sana,”alisema.

Aliwataka wataalamu kuhakikisha wanawafikia wafugaji wadogo na kujua matatizo ambayo wanakutana nayo katika kazi zao na kuwasaidia katika kujua namna ya kufaidika na ufugaji wao waweze kujikomboa kiuchumi katika sekta hiyo.

Naye, Mkurugenzi wa Utawala wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Lucias Mwenda, aliyekuwa akimuwakilisha Katibu Mkuu wa wizara hiyo, alisema katika kuhakikisha wanainua sekta ya nyuki waliunda kikosi kazi cha kufanya tathimini muhimu kuhusu sera hiyo.

Pia aliwataka wajumbe wa warsha hiyo kutumia muda huo kupitia sera hiyo kwa umakini, kuweka michango yao kwa kuangalia maeneo ambayo bado hayasaidii kasi ya kukua kwa sekta ya nyuki ili sera itakapokamilika iweze kuleta njia na matokeo sahihi.

Naye, Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki, Ezekiel Mwakalukwa alisema katika kuinua sekta hiyo waliona kuna haja ya kupitia sera ya ufugaji wa nyuki ya mwaka 1998, ili kuona namna ya kuiboresha iendane na wakati wa sasa.

RAIS John Magufuli amesema Waziri wa Mambo ya ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi