loader
Picha

Umuhimu, changamoto wajawazito Songwe kuhudhuria kliniki

LICHA ya elimu inayotolewa na wataalamu wa afya kuhusu umuhimu wa wajawazito na watoto kuhudhuria kliniki mapema, baadhi ya wananchi mkoani Songwe hawafanyi hivyo kwa sababu mbalimbali, ikiwamo ya baadhi kuamini wanaweza kuhatarisha mimba zao.

Hata hivyo, wapo wengine wanaohudhuria kliniki, lakini hao hawafiki mapema na wakati wa kujifungua jambo linalowafanya wajawazito wengine au watoto wao na wakati mwingine, mama na mtoto kupoteza maisha. Baadhi ya akinamama waishio vijijini ili wanazitaja baadhi ya sababu zinazowasukuma kuchelewa kuanza mahudhurio ya kliniki wanapopata ujauzito kuwa ni pamoja na ukosefu wa elimu au hamasa ya kutosha kuhusu umuhimu wa kuwahi kliniki, mfumo dume na upungufu wa vituo vya afya hasa katika maeneo ya vijijini.

Mmoja wa wanawake hao ambaye ni mama wa watoto watatu, Suzan Kapenda anasema haoni umuhimu wa kuhudhuria kliniki katika miezi ya mwanzoni ya ujauzito kwa kuwa watoto wake wote alijifungua salama licha ya kuchelewa kuanza kupata huduma za kliniki. “Mimba za wanangu wote nilikuwa nakwenda kliniki zikiwa tayari ni kubwa, lakini zote najifungua salama tu, wa kwanza nilijifungua nikiwa na miaka (19) na nilianza kwenda kliniki nikiwa na ujauzito wa miezi saba na siku nilipopata uchungu ndipo nilienda kwa ajili ya kujifungua baada ya miezi tisa kuisha,” anasema Suzana.

Anaongeza: “Wawili waliofuata, nao ilikuwa hivyo hivyo na wote wapo vizuri tu kiafya ingawa nilipojifungua mtoto wa kwanza nilifokewa sana na madaktari eti kwa kuwa nimechelewa kufika hospitalini na pia, kutokwenda kliniki mara kwa mara.”

Kuhusu sababu hasa za kuchelewa na kutohudhuria ipasavyo kliniki, Suzana anasema hospitali iko mbali, hivyo anaogopa kutumia gharama nyingi za usafiri kwenda mara kwa mara hospitalini. “Sasa hali hiyo unaona itafanya kazi zangu nyingi kusimama mara kwa mara hasa shughuli zangu za kilimo…” Salah Antony mkazi wa Kijiji cha Iyendwe, Kata ya Kapele wilayani Momba anasema wanashindwa kuhudhuria kliniki kutokana na kata yao kutokuwa na kituoa cha afya, hivyo wengi kwenda hospitali wakati wa kujifungua pekee na wengine kujifungulia nyumbani.

“Wifi yangu alifia njiani kutokana kukosa elimu ya uzazi pamoja na umbali wa kwenda kwenye Kituo cha Afya cha Ndalambo na Hospitali ya Vwawa ambako huduma za upasuaji zinafanyika. Kwa kweli tunaishukuru serikali kwa kusikia kilio chetu cha muda mrefu hasa sisi akina mama kwa kuanza kutujengea kituo cha afya katika kata yetu ya Kapele,” anasema Salah.

Anasema kimsingi, wanapenda na wanatamani kuhudhuria kliniki kama walivyo akina mama wanaoishi karibu na vituo vya afya, lakini kutokana na umbali mrefu uliopo ili kufikia kituo cha afya, takriban kilomita 50 hujikuta wanatumia gharama kubwa huku barabara ikiwa siyo rafiki kwao hasa katika kipindi cha masika ambapo barabara nyingi huharibika zaidi.

Naye Merry Daud Kamanga anasema mwaka jana wanawake wawili na watoto wao kutoka Kijiji cha Namsinde, Kata ya Kapele walifariki dunia kutokana na umbali wa kituo cha afya na ubovu wa barabara unaosababisha watu wengi kuzidiwa wakiwa njiani na wengine kuamua kwenda kutibiwa nchi jirani ya Zambia. Diwani wa kata hiyo, Vedastan Simpasa, anasema Kata ya Kapele pia hukumbwa na changamoto za barabara zinazosababisha baadhi ya wagonjwa kuomba kwenda kutibiwa nchi jirani ya Zambia ili kuepusha vifo vinavyochochewa pia na umbali mrefu uliopo ili kuvifikia vituo vya afya.

Daktari Bingwa Magonjwa ya Wanawake na Afya ya Uzazi Hospitali ya Mkoa wa Songwe, Dk Lukombodzo Lulandala, anasema mwaka 2018 Mkoa wa Songwe ulikuwa na vifo vya wajawazito vilitokea wakati wa kujifungua. Anasema: “Waliopoteza maisha kutokana na kupoteza damu nyingi baada ya kujifungua ni asilimia 11, kifafa cha mimba asilimia 8, upungufu wa dawa asilimia 5, waliopata shida ya kupumua ghafla na kufariki ni asilimia 4, wanaoshindwa kujifungua na kulazimisha kujifungua hadi kufa ni asilimia 2 na wanamwaga sana damu na kufariki ni asilimia 1.”

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo wa afya, mama anapaswa kuanza kuhudhuria kliniki pale tu, anapodhani ana ujauzito, ili kuwahi kupata vipimo vitakavyothibitisha na kupata ushauri wa daktari kuhusu hali yake. Anasema hilo linapofanyika mapema humpa mjamzito fursa ya kupata elimu ya afya wakati wa ujauzito, elimu ya maandalizi ya wakati wa kujifungua na wapi anapaswa kujifungulia. “Pia mama atapata fursa ya kufanyiwa vipimo vya awali kama vile kupimwa kisukari, shinikizo la damu, magonjwa ya zinaa, kundi la damu, malaria, hali ya mkojo na pia kupata dawa za kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali ukiwemo malaria, magonjwa ambayo ni hatari kwa afya mtoto aliyepo tumboni,” anasema.

Anazitaja faida nyingine za mjamzito kuhudhuria mapema kliniki kuwa ni pamoja na kupata chanjo na dawa kinga muhimu kwa mtoto aliye tumboni. Anasema: “Hii inamfanya mjamzito kujifungua salama, kuzaa mtoto mwenye afya njema na utimamu mzuri wa akili.” Anaongeza: “Katika mahudhurio ya kliniki, mjamzito atajua kama atajifungua kwa upasuaji au kwa njia ya kawaida kutokana na hali ya mtoto.”

Madhara ya kuchelewa kliniki, kutojifungulia hospitali Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, madhara ya kuchelewa kuhudhuria kliniki na kutojifungulia hospitali ni pamoja na kuchelewa kubaini magonjwa yenye athari kubwa kwa mama na mtoto yakiwamo magonjwa ya kisukari na presha na kuchelewa kupata chanjo na dawa za kinga muhimu kwa mtoto awapo tumboni na hata baada ya kuzaliwa.

Madhara mengine kwa wanaochelewa au kutokwenda kujifungulia hospitali ni pamoja na kukosa msaada na kupata shida wakati wa uzazi, mtoto kupoteza uhai, hatari ya uwezekano wa mama kupata fistula endapo atapata uchungu pingamizi kwa muda mrefu na kukosa huduma za wataalamu sambamba. “Pia kuna uwezekano wa mama kupoteza baadhi ya viungo vya uzazi kutokana na mfuko wa uzazi kupasuka na kushindwa kufanyiwa marekebisho,” anasema Dk Lulandala.

Kwa mujibu wa Dk Lulandala, takwimu za mwaka 2018 zinaonesha kuwa, mwaka 2018 akina mama waliojifungua katika vituo vya kutolea huduma walikuwa 36,660 sawa na asilimia 79. “Waliojifungulia njiani kuelekea vituo vya afya ni 1,505 (asilimia 3) na waliojifungulia kwa wakunga wa jadi ni 222, waliojifungulia nyumbani ni 1,193 hivyo, utaona bado tuna kazi kubwa kuhakikisha wajawazito wanajifungulia katika vituo vya kutolea huduma,” anasema. Dhana potofu Miongoni mwa changamoto kubwa zilizopo ni pamoja na kuwapo imani potofu kwa akina mama kuwa, wakiwahi hospitali kujifungua, watafanyiwa upasuaji wakati wa kujifungua, jambo ambalo mtaalamu huyo anasisitiza kuwa, siyo sahihi.

Anasema: “Wataalamu humfanyia upasuaji yule ambaye kweli ana sifa za kupasuliwa na siyo vinginevyo. Mfano, endapo mtoto ni mkubwa sana ukilinganisha na uwezo wa nyonga za mama, au mtoto akikaa vibaya. Anaongeza: “Hata hivyo zipo sababu nyingine nyingi za kitalaamu lengo kuu likiwa ni hasa kunusuru maisha ya mama na mtoto.” Mtaalamu huyo anawataka wanaume kushiriki kikamilifu katika kipindi chote cha ujauzito, ikiwa ni pamoja na kwenda na wenza wao kliniki, pamoja na kuwaruhusu wake zao kuwahi kliniki kujifungua ili kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza.

Mkuu wa mkoa Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Brigedia Nicodemas Mwangela anasema ujenzi wa hospitali za halmashauri za Tunduma, Ileje na Songwe ukikamilika hivi karibuni, utapunguza changamoto ya upungufu wa huduma za afya hasa kwa mama na mtoto. “Serikali yetu ina dhamira ya dhati kwa wananchi wake katika sekta ya afya. Tunaona dhahiri jitihada kubwa katika kuboresha vituo vya afya hivyo wananchi watumie fursa hii na kumuunga mkono Rais John Magufuli kwa kutumia vyema vituo vya afya alivyovijenga nchi nzima,” alisema Mwangela.

MAFUNZO ya uongozi na usimamizi wa elimu ni ...

foto
Mwandishi: Baraka Messa

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi