loader
Picha

JPM: Msichague wala rushwa

RAIS John Magufuli amewataka Watanzania kutowachagua wagombea uongozi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, utakaofanyika baadaye mwaka huu na Uchaguzi Mkuu wa mwakani watakaotoa rushwa.

Aliyasema hayo mjini Geita jana alipokuwa akizindua nyumba 20 za makazi ya askari polisi katika eneo la Magogo mjini Geita. Rais Magufuli alisema wakati uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa unakaribia ni vizuri kwa wananchi kuanza kutafakari juu ya viongozi wazuri watakaowasaidia kuwaletea maendeleo na si kuwachagua kwa rushwa.

“Mkachague viongozi waadilifu, mchague viongozi ambao watakuwa ni watumishi wa wananchi na hasa wanyonge. Msichague wala rushwa, wakiwapa hela zao chukueni, kuleni lakini kura msiwape,” alisema Rais Magufuli. Alisema viongozi wakipatikana kwa njia ya rushwa, watakuwa wanasimamia miradi yenye maslahi yao binafsi badala ya kusimamia maendeleo yenye maslahi mapana kwa wananchi wanyonge wa Tanzania.

Alisema ili kufanikisha uchaguzi wa serikali za mitaa, Jeshi la Polisi lina wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa linaendelea kutunza amani na utulivu, ili uchaguzi huo uweze kufanyika vizuri na kuwezesha kupatikana kwa viongozi wazuri.

Kuhusu makazi ya askari, Rais Magufuli alisema serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha makazi na utendaji kazi wa askari ili jeshi hilo liweze kufanya kazi ya kusimamia amani na utulivu wa nchi lakini pia maisha na mali za wananchi.

Alisema pamoja na kazi kubwa inayofanywa na jeshi hilo lakini wapo wanasiasa ambao wanatoa maneno ambayo yanavidhalilisha vyombo vya ulinzi na usalama kwa maslahi yao na aliwataka kuacha kufanya hivyo na badala yake kuwatia moyo askari ili waendelee kufanya kazi zao kwa bidii na weledi mkubwa.

Hata hivyo, alisema wapo askari ambao wamekuwa wanakiuka maadili ya kazi yao na alimwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro kuendelea kuwafukuza kazi askari wote watakaobainika kukiuka misingi na maadili ya kazi yao na kulipaka matope jeshi hilo.

RAIS John Magufuli amesema Waziri wa Mambo ya ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Geita

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi