loader
Picha

Tanzania, Uganda zaja na jukwaa la biashara

TANZANIA na Uganda zimeanzisha rasmi Jukwaa la Biashara baina ya nchi hizo, lengo likiwa kufungua milango zaidi ya biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Mbali ya Tanzania na Uganda, nchi nyingine wanachama wa EAC, jumuiya yenye wakazi zaidi ya milioni 170 ni Kenya, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini. Akizungumza wakati wa uzinduzi wa jukwaa hilo hivi karibuni jijini Kampala, Waziri wa Nchi wa Uganda anayeshughulikia masuala ya EAC, Dk Philemon Mateke alisema jukwaa linatarajiwa kuwa `daraja’ muhimu katika sekta ya biashara baina ya Tanzania na Uganda.

“Hatuna sababu za kutofanya biashara kwa uwazi na kisasa zaidi kwani nchi zote hizo zimetengeneza mazingira mazuri ya biashara. Nchi zote zina amani, miundombinu mizuri na kadhalika.

Ni wakati wa kuchangamka kibiashara,” alisema Dk Mateke. Kutokana na kuzinduliwa kwa jukwaa hilo, alisema kwa siku mbili kuanzia Septemba 4 mwaka huu, wadau muhimu watakutana Dar es Salaam kujadili masuala mbalimbali yatakayoboresha ustawi wa biashara. Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Richard Kabonero alisema mkutano huo utafanyika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), ukiwa na kaulimbiu ‘Ukuzaji Biashara na Uwekezaji kwa Ukuaji na Maendeleo Endelevu’.

Miongoni mwa washiriki watakuwa viongozi wa taasisi za kibiashara, watunga sera, wadau wa biashara na wengine, ili pamoja na mambo mengine kuchambua fursa zilizopo baina ya nchi hizo mbili na jinsi zinavyoweza kuleta neema kwa watu wa mataifa hayo.

Alisema wakati wa mkutano, watazungumza pia na Rais Yoweri Museveni wa Uganda na mwenzake wa Tanzania, Dk John Magufuli juu ya masuala mbalimbali na changamoto za kibiashara baina ya nchi zao. Naye Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Aziz Mlima, alisema mikakati ya kukuza biashara baina ya nchi hizo mbili, ikiwa ni pamoja na kuondoa vikwazo mbalimbali inafanyiwa kazi ili kutengeneza mazingira bora ya biashara.

SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika kipindi ...

foto
Mwandishi: KAMPALA, Uganda

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi