loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

MWENGE WA UHURU Tunu isiyopaswa kubezwa

BAADHI ya watu nchini wamekuwa mahiri kubeza baadhi ya mambo wanayoyaona hayana umuhimu katika nchi kwa mtazamo wao wa kiitikadi. Kubeza kwao hakuna tafsiri pana inayothibitisha wanachokisimamia, badala yake wamekuwa wakibeza bila ya kufanya utafiti wa kina juu ya hoja zao hizo.

Kwa mfano, nimewashuhudia baadhi wakibeza juu ya uwepo wa ukimbizaji wa Mwenge wa Uhuru ambao kimsingi ni alama ya taifa letu. Kwa wasiofahamu, mwenge huu uliwashwa kwa mara ya kwanza na kuwekwa juu ya kilele cha Mlima Kilimanjaro Desemba 1961.

Wanaoubeza hawamuenzi Hayati Baba wa Taifa, bali wanamkejeli na hawana uzalendo wa dhati kwa nchi yetu. Lengo la kuwashwa kwa mwenge kama ambavyo iliwahi kuelezwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ni kuleta matumaini kwa jamii ya watu waliokata tamaa, upendo palipokuwa na chuki na heshima pale palipooneshwa dharau.

Katika moja ya zawadi ambayo taifa hili liliachiwa na Baba wa Taifa, ni pamoja na huu Mwenge wa Uhuru, ambao kimsingi, umekuwa unakimbizwa hapa nchini na kufungua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo inayokwenda sanjari na uwajibikaji wa viongozi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Mwenge wa Uhuru ni alama muhimu katika taifa letu inayoashiria uwepo wa nuru na mwanga na siyo laana kama ambavyo imekuwa ikielezwa na baadhi ya watu hasa baadhi ya wanasiasa wanaopinga kila kitu. Mwalimu Nyerere aliamini mwenge kama alama ya umoja, mshikamano na kama kichocheo cha uwajibikaji.

Baada ya Tanzania kupata uhuru, hakukuwa na njia nyingine ya kuwahamasisha wananchi kujenga fikra zao na kuipenda nchi yao kwa kujenga mshikamano wa pamoja na kupinga udhalimu na unyonyaji ili kuwa na jamii yenye usawa. Nyerere aliutumia Mwenge kupandikiza mbegu ya uzalendo kwa Watanzania iliyowawezesha kushiriki katika ujenzi wa uchumi wao kuanzia ngazi ya kaya, kijiji, wilaya hadi taifa kwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa na kugawana keki ya taifa kwa usawa.

Aliutumia Mwenge kutoa elimu kwa Watanzania kutoka kwenye mifumo ya kutawaliwa na wakoloni na kuwafanya wajikite kuzalisha mali kama jamii ya watu wanaojitegemea.

Umeendelea kuwa ni tanuru la kuwapika na kuwaibua viongozi na watumishi wa serikali tangu ulipoanzishwa hadi wakati huu. Inasemekana kuwa mmoja wa viongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa kwa miaka ya 1970, aliteuliwa na Mwalimu Nyerere kuwa mkuu wa wilaya wa kwanza. Uteuzi huo umeendelea hadi sasa. Baadhi ya viongozi waliowahi kushika nyadhifa za kuteuliwa, waliostaafu na walioko kazini ni wakuu wa wilaya na mikoa.

Yumo Jordani Rugimbana aliyeteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni na baadaye kuwa Mkuu wa mikoa ya Lindi na Dodoma ambaye sasa amestaafu.

Mwingine ni aliyekuwa kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa mwaka jana, Charles Kabeho aliyeteuliwa mwaka jana na Rais John Magufuli kuwa Mkuu wa Wilaya ya Tarime. Wapo akina ‘Rugimbana’ na ‘Kabeho’ wengi ambao ni viongozi wanaotokana na matunda ya uwepo wa Mwenge wa uhuru unaobezwa kwa sasa. Mwalimu aliutumia Mwenge wa Uhuru kama yamini ya kupambana na watu wazembe, wazururaji na wahujumu wa uchumi wa nchi yetu.

Nakumbuka kwa mara ya kwanza nikiwa nasoma katika shule ya msingi, mwenge ulifika kijijini kwetu mwaka 1983 huku ukiwa na kiitikio cha “Walanguzi- Mwenge choma, wezi- Mwenge choma, wanaoiba fedha za umma- Mwenge choma.” Mwenge umeimarisha Lugha ya Kiswahili ambayo imeendelea kuwaunganisha Watanzania, umewezesha vijana katika nchi kuwa na ari ya kujitolea. Inaaminika kuwa kuundwa kwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ni baada ya kuanzishwa kwa mbio za mwenge kazi iliyofanywa na Mwalimu Nyerere.

Nyerere alitumia Mwenge wa Uhuru kuimarisha muungano na umoja wa kitaifa. Baada ya kuanzishwa kwa mbio za mwenge, ulikuwa unakimbizwa Tanzania Bara na baada ya Mapinduzi ya Zanzibar, ulikimbizwa mikoa ya Unguja na Pemba. Nyerere aliutumia Mwenge kama chombo cha kuwakumbusha wananchi kuulinda uhuru, umoja na mshikamano ambao uhuru huo kwa sasa ni uwajibikaji na kufanya kazi kwa bidii.

Ukimbizaji wa mwenge huo hufanyika kila mwaka hapa nchini kwa Tanzania Bara na Visiwani ukiwa hasa na lengo la kuujenga uzalendo kwa kuwakumbusha Watanzania jukumu la kulinda uhuru, umoja, amani na na utulivu. Sababu nyingine ni kuimarisha uwajibikaji miongoni mwa viongozi na watendaji wa Serikali na kujenga uzalendo kwa Watanzania kushiriki kikamilifu kwenye ujenzi wa taifa kupitia kwenye miradi wanayoibuni kwenye maeneo yao, ambayo baadae huzinduliwa, kufunguliwa na Mwenge huo kwa shamrashamra kubwa kwenye maeneo yao.

Jambo la msingi hapa ni kuwa kabla ya uzinduzi wa miradi hiyo ya maendeleo inayohusisha ujenzi wa barabara, visima, nyumba za walimu, miradi ya kijamii na mingine inayofanana na hiyo, husomwa taarifa za utekelezaji na ujenzi wa miradi hiyo inayohusisha ushiriki mpana wa wananchi kwenye maeneo yao. Hapa viongozi ambao ni wasimamizi wa Mwenge huo katika ngazi ya wilaya, wakuu wa wilaya na ngazi ya mkoa makatibu tawala wa mikoa kabla ya uzinduzi wa miradi hiyo, hupata fursa ya kutembelea miradi na kuona kama inakidhi thamani halisi ya fedha kwa miradi inayotarajiwa kuzinduliwa.

Ikitokea miradi hiyo imekamilika chini ya kiwango au ikashindwa kukamilishwa kabisa, waliohusika katika utekelezaji wa miradi hiyo huwajibishwa na serikali. Kwa namna hii, wanaoubeza mwenge ni sawa na wenye macho, lakini hawataki kuona. Kadhalika, Mwenge wa Uhuru unasimama kama sauti za wananchi katika kuhoji utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia mikutano ya mitaa na vijiji husikika kwenye maeneo yao, wananchi hupata fursa ya kutoa maoni yao jambo ambalo ni muhimu katika ukuaji wa demokrasia na maendeleo.

Kuwepo kwa Mwenge kwa mazingira ya sasa ni kama kuwa na mdhibiti au mkaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayojengwa na serikali na ile inayoibuliwa na wananchi wenyewe. Haya yanalenga kuangazia palipo na shida na kuangalia uhalisia wa miradi na fedha zinazotolewa na serikali katika utekelezaji wa miradi hiyo. Kiongozi wa mbio za mwenge ambaye ni mteule wa Rais, kwa wasiofahamu, anamwakilisha Rais katika kukimbiza Mwenge wa Uhuru.

Hivyo basi kwa wale wanaobeza na kukejeli Mwenge wa Uhuru, ambao pia ni alama muhimu katika kujenga na kulinda historia ya nchi, wanamkejeli Rais wa nchi na wanakinzana na Watanzania ambao kwa moyo wa shukurani na nia njema, wanamuenzi kwa dhati, Mwalimu Nyerere.

Jambo jema kupitia Mwenge huo ni kuwa, miradi inayoonekana kutokidhi viwango ama thamani halisi ya fedha haizinduliwi na badala yake, viongozi na wote walioshiriki kuisimamia wanawajibishwa kwa manufaa ya umma.

Hii ndiyo inanifanya niseme kuwa, Mwenge wa Uhuru ni chombo kinachodhibiti na kuangalia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya wananchi ili ilete tija, wanaobeza shughuli zake siyo wazalendo maana hii ni tunu ya taifa isiyopaswa kubezwa. Hali kadhalika, miradi mbalimbali inayozinduliwa na mbio za mwenge inatumiwa na Watanzania wote bila ya kujali rangi, cheo, dini, chama chake cha siasa, kabila wala kiwango cha elimu aliyo nayo mtu.

Miradi hiyo hutumiwa na wanasiasa kuelezea sera zao, kusomesha watoto wao, kupata mahitaji ya jumla kama maji, matibabu, umeme na mengine mengi bila ya kujua wanapokejeli mbio hizo, wanakuwa kama mtu anayekata mti alioukalia maana ukianguka utaanguka naye!

“FISI ni mnyama muhimu sana katika hifadhi yetu (Hifadhi ya ...

foto
Mwandishi: Nashon Kennedy

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi