loader
Picha

TEC, Bakwata, CCT mmefanya vyema kuiunga mkono serikali

TANGU aingie madarakani, Rais John Magufuli ameweka msisitizo mkubwa kwa Watanzania kutumia juhudi na maarifa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati unaochochewa na nguvu ya viwanda.

Mara kwa mara Rais Magufuli anatumia nguvu nyingi kuelimisha na kuhamasisha Watanzania kutumia nguvu na akili zao kushiriki kikamilifu juhudi za kuelekea uchumi wa kati kupitia viwanda.

Kwa kutambua umuhimu wa viwanda, Serikali ya Awamu ya Tano imekuja na dhamira mpya ya kufufua viwanda na kuanzisha vipya. Lengo la mpango huo limetajwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ili kuwaletea wananchi maisha bora na kujenga uchumi imara wenye uwezo wa kukabiliana na ushindani.

Profesa Kitojo Wetengere katika moja ya machapisho yake katika gazeti hili anasema, ili kutimiza azma hii, Watanzania wanahitaji kujenga viwanda vya kuongeza thamani rasilimali walizo nazo yakiwamo mazao ya shambani; wawe na viwanda vitakavyoajiri watu wengi; viwanda vya kuzalisha bidhaa na huduma zenye faida linganifu; na vinavyotumia teknolojia ya kisasa na ubunifu.

Rais anasisitiza watu kufanya kazi kwa juhudi na maarifa na kiadilifu tangu ngazi ya mtu mmoja mmoja, familia, vikundi na hata taifa ili kuzalisha shambani na viwandani kwa matumizi ya ndani na hata kuzalisha kibiashara kwa ajili ya kuuza mazao nje ya nchi. Lengo la mkuu wa nchi kama linavyoonekana hata katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ni kuhakikisha Watanzania kwa kutumia juhudi na maarifa yaliyopo, wanatumia na kufaidi fursa za kiuchumi zilizopo.

Ndiyo maana hata katika suala la ajira, wazawa wanapewa kipaumbele cha kwanza ili Watanzania wazidi kutumia fursa hizo na kumiliki uchumi sawia, hivyo kuliepusha taifa dhidi ya hatari ya kutegemea misaada ambayo mingine ni hatari kwa usalama wa taifa.

Wanahimizwa kuzalisha kwa kiwango kikubwa na kwa ubora unaotakiwa kitaifa na hata kimataifa ili kumudu ushindani. Inatia moyo kuona viongozi wa dini wameziona juhudi chanya za serikali na kuamua kuziunga mkono kwa kuzindua mkakati wa Mfumo wa Uchumi wa Soko Jamii ili kuchochea kasi ya Tanzania kuelekea uchumi wa viwanda.

Izingatiwe kuwa, nchi huyumba kiuchumi na kiusalama kama muda wote inaagiza bidhaa nyingi nje ya nchi kuliko inavyouza nje; kama inategemea misaada zaidi ya wafadhili, kuliko makusanyo yake ya ndani na pia, kama muda wote inauza malighafi, badala ya hasa kuuza bidhaa.

Katika kuunga mkono juhudi za rais zinazolenga kuwafanya Watanzania kumiliki uchumi tangu ngazi ya mtu mmoja mmoja hadi taifa, hivi karibuni Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) walizindua mkakati wa Mfumo wa Uchumi wa Jamii wa Soko Jamii (Smet).

Katika uzinduzi huo uliofanyika Dar es Salaam, viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu nchini, walisema wanapendekeza mfumo huo wa uchumi utumike miongoni mwa jamii ili kuongeza ukuaji wa uchumi shirikishi na endelevu na kuhakikisha ustawi wa nchi.

Katika chapisho liitwalo: “Mfumo wa Uchumi wa Jamii wa Soko Jamii kwa Tanzania: Kuelekea Maendeleo Shirikishi na Endelevu ya Kiuchumi,” wanataja tunu za mfumo huo ambazo kifupi chake kwa maneno ya Kiingereza kinaunda maneno: “KWA NCHI YETU” kuwa ni: Knowledge (Ufahamu), Wisdom (hekima), Accountability (uwajibikaji), Nation first (taifa kwanza), Community (jumuiya), Human dignity (utu wa mtu), Integrity (uadilifu), Youth (vijana), Evaluation (tathmini ya sera za maendeleo), Transparency (uwazi) katika kufanya maamuzi na utekelezaji wake na Unity (umoja/mshikamano).

Katika uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Uhusiano wa Dini mbalimbali ambaye pia ni Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Steven Munga, anasema umefika wakati Watanzania kumuunga mkono Rais John Magufuli kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kuongeza tija na kukuza uchumi.

Anasema: “Sasa tuhame kutoka kwenye maneno kwenda kwenye vitendo….” Kaimu Mufti wa Tanzania, Shehe Ali Muhidin Mkoyogore aliyefanya uzinduzi huo kwa niaba ya Waislamu anasema: “Mfumo huu tuusome kwa makini na kuufanyia kazi sawasawa.” Katibu Mkuu wa TEC, Padri Dk Charles Kitima anasema: “Mfumo huu pia utazalisha walipa kodi wengi kupitia ajira mbalimbali na biashara na watu watakwenda katika kilimo shambani kwa vile wanajua wana uhakika wa soko na kupata pesa….”

“Huu ni mfumo unaolenga utu wa mtu bila kunyanyasa wengine; unaolenga kumfaa binadamu na siyo kumwangamiza; ni mfumo unaolenga kutunza mazingira na siyo kuyaharibu na yote haya yanakuwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.”

Kwa mujibu wa Dk Kitima, Watanzania wanapaswa kushirikishwa na kuelewa zaidi umuhimu wa uzalishaji na uendeshaji biashara adilifu katikati ya uchumi ili Mtanzania ampende Mungu na wakati huohuo pia, apate maendeleo ya kweli. “Mfumo wa kodi au sera ya fedha ni muhimu katika uzalishaji na uendeshaji wa shughuli za serikali. Uzalishaji na uendeshaji biashara adilifu lazima uambatane na ulipaji kodi kwa serikali na hivyo, ni muhimu kuwapo kiwango na aina za kodi zitakazosaidia serikali kujiendesha bila kutegemea misaada kutoka nje,” alisema.

Katika mazungumzo ya awali, Dk Kitima anasema: “Kama anavyosisitiza Rais, kodi hizo hazipaswi kuwa kubwa mno kiasi cha kumwathiri mlipakodi na ndiyo maana mfumo wa uchumi jamii unapendekeza mfumo wa kodi ambao ni rafiki kwa biashara na ni mfumo unaosaidia wananchi wazawa.”

Anasema Watanzania wanapaswa kushirikishwa na kuelewa zaidi umuhimu wa uzalishaji na uendeshaji biashara adilifu katikati ya uchumi ili Mtanzania ampende Mungu na wakati huohuo pia, apate maendeleo ya kweli. “Tunataka tuwajenge watu wawe na ushindani na uzalishaji shirikishi katika uchumi hata kupitia Watanzania kumiliki kampuni mbalimbali na kubwa hata kupitia hisa ndiyo maana tunahimiza pia watu wafundishwe kuzalisha kiadilifu na kulipa kodi.”

Katika hafla hiyo ya uzinduzi, viongozi mbalimbali wa dini kwa nyakati tofauti wanasema wanapenda kuona matamanio ya Rais Magufuli ya kuiacha Tanzania ikiwa na mabilionea wapatao 100 atakapostaafu, yanatimia na hata kuzidi huku kukiwa hakuna Mtanzania anayeachwa nyuma kiuchumi. Kitima akaongeza: “Huu ni uchumi unaolenga kuwafanya watu waone fursa kutengeneza uchumi wa mtu binafsi, familia na uchumi wa taifa ili serikali ipate pato lake na hata kwenye kilimo, mtu zalishwe vizuri, lakini pia alipwe vizuri na kupata mapato mazuri,” alisema kasisi huyo wa Kanisa Katoliki.

“Tunataka tuwajenge watu wawe na ushindani na uzalishaji shirikishi katika uchumi hata kupitia Watanzania kumiliki kampuni mbalimbali na kubwa hata kupitia hisa ndiyo maana tunahimiza pia watu wafundishwe kuzalisha kiadilifu na kulipa kodi,” alisema. “Tunataka watu wenyewe watambue kuwa biashara siyo tu kununua simu kutoka China kwa mfano na kuja kuziuza hapa Tanzania, bali kila mmoja afikirie na kuweka juhudi za kuzalisha simu hizo hapa nchini na hii, itaepusha kasumba ya vijana wengi wanapohitimu masomo, kutaka kuajiriwa badala ya kujiajiri na kuajiri wengine.”

Alisema umefika wakati Watanzania waepuke kuwa na mfumo wa uchumi usiowafanya kuwa soko la bidhaa na huduma za wengine. “Hatutaki kumzuia wala kumfukuza mtu mwingine asifanye biashara wala kuwekeza Tanzania, lakini lazima na sisi wenyewe tufanye na tulenge kuwa wawekezaji wa kwanza na muhimu zaidi nchini tunaozingatia uzalishaji mkubwa na wa bidhaa bora,” anasema Dk Kitima.

Shehe wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke, anasema umefika wakati sasa hata viongozi wa dini kuelewa kuwa, wanao wajibu mkubwa kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa watu wao na kwamba, siyo jukumu la serikali pekee. “Lazima tuungane na Rais Magufuli kuongeza manufaa na kipato kwa kila mtu kukuza uchumi na kulinda amani maana amani ya nchi haiwezi kupatikana kama kuna watu wamekata tamaa hivyo, lazima tuunganishe nguvu zetu na serikali na hapa, lazima tufundishe watu kutafuta riziki kwa njia halali,” anasema. Ndiyo maana ninasema: “TEC, Bakwata, CCT mmefanya vyema kuiunga mkono serikali katika masuala haya ya uchumi.”

KATIKA toleo hili, tunaangalia namna utamaduni uliopo katika utumishi wa ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi